Header Ads Widget

JE, WANAHABARI NI TISHIO KWA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI?


Na Kadama Malunde
Uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari katika nchi nyingi duniani bado ni changamoto. Kuwepo kwa sheria mbalimbali na mfumo kandamizi wa utawala usiofuata misingi ya demokrasia na haki za binadamu ni kichocheo kikuu cha kukosekana kwa uhuru huu. 

Mwanazuoni Hans (2009) anabainisha kwamba zaidi ya asilimia 30 ya watu duniani wanaishi kwenye nchi zinazovunja uhuru wa vyombo vya habari.

 Ingawa tafiti zinahusianisha kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza na tawala za mabavu zinazothibiti utoaji na upatikanaji wa taarifa, pia zipo Serikali zinazofuata demokrasia ilihali zinaminya uhuru huu. 

Hii inatokana na namna ya kila tawala zinavyotafsiri maana ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari katika nchi husika.

Kwa ujumla, mwanazuoni Dave (2007) ametafsiri maana ya uhuru wa vyombo vya habari kama haki na uhuru wa kutafuta, kuchakata na kutoa habari na taarifa bila kuingiliwa na mtu, kikundi cha watu, au Serikali. Maana yake ni kwamba, ili chombo cha habari kitekeleze wajibu wake ipasavyo kinapaswa kuwa huru.

Hata hivyo, kwa Tanzania, kumekuwepo na jitihada za wadau mbalimbali wa haki za binadamu na vyombo vya habari vinavyofanya uragibishaji unaolenga kuwepo kwa mazingira chanya yatakayochochea vyombo vya habari kufanya kazi zake za kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha, kukosoa na kuilinda jamii kwa uhuru bila kuingiliwa na Serikali ama taasisi yoyote.

 Wakati jitihada hizi zikiendelea, kumejitokeza matukio ya baadhi ya waandishi wa habari kukiuka misingi ya uweledi wa kazi zao.

Hivi karibuni waandishi wa habari wameutumia uhuru visivyo kwa kuripoti matukio kwa kupotosha taarifa dhidi ya mamlaka za Serikali ikiwemo viongozi wa juu wa Serikali za mikoa na jeshi la polisi kwa ngazi hizo. 

Bahati mbaya, pamoja na makosa ya kiuweledi ya waandishi hawa wachache bado baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wamekuwa wakisambaza upotoshaji kuwa waandishi wao wamekamatwa na polisi ilhali sio kweli.

Matukio yaliyojiri Tanga mjini na Korogwe mkoani humo yaliyowahusisha waandishi wawili wa vyombo vya habari vikubwa hapa nchini ni baadhi ya mifano michache ya waandishi wa habari wasiofuata weledi na maadili ya kazi na kupelekea sintofahamu.

Aidha, baadhi ya vyombo vya habari hususan magazeti likiwemo gazeti la Uhuru lilifungiwa kwa kupotosha taarifa kuhusu kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kama hio haitoshi, hivi karibuni kabisa mojawapo wa magazeti makubwa nchini yameripoti visivyo kauli ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu juu ya kampeni ya chanjo.

 Kuendelea kwa matukio haya kunatoa taswira kuhusu matumizi mabaya ya uhuru wa vyombo vya habari. 

Makosa ya kiuweledi yanayoendelea kufanywa na vyombo vyetu yanafifisha uhalali wa kudai uhuru kwa kuwa wahusika hawajui namna ya kuutumia.

Hakuna uhuru wa vyombo vya habari usio na wajibu. 

Chombo cha habari kiwajibike kabla ya kudai uhuru.

 Aidha, ni wajibu wa taasisi za kihabari ikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Chama cha Waandishi Wanawake Tanzania (TAMWA), na uongozi wa vyombo vya habari mbalimbali kuhimiza kuzingatia weledi na miiko ya uandishi wa habari miongoni mwao. 

Kwa sasa kuna matumaini ya kuimarika kwa mazingira mazuri yatakayochochea kushamiri kwa uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yake. 

Hivyo, ni wajibu wa vyombo hivi kujiimarisha kuwekeza zaidi katika weledi ili kuutendea haki uhuru vinavyoupigania.

Post a Comment

0 Comments