Header Ads Widget

WAFANYABIASHARA MASHINE ZA KUSAGA NA KUKOBOA NAFAKA IBINZAMATA WALIA KUKOSA UMEME SIKU 7

 

Baadhi ya wafanya biashara wa Ibinzamata, Manispaa ya Shinyanga wamelalamikia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Shinyanga kwa kukosa nishati ya umeme kwa muda wa siku saba na kukwamisha shughuli zao za kiuchumi huku wakihoji Rais Samia amesema Kazi Iendelee, inaendeleaje bila umeme?.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 25 ,2021maeneo ya Ibinzamata kwenye eneo la viwanda vidogo vya kusaga wa nafaka,baadhi ya Wafanya biashara hao akiwemo Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mashine za kukoboa na kusaga nafaka Ibinzamata Josephat Michael  wamesema licha ya kufika Ofisi za Tanesco kueleza kero hiyo wafanyakazi wa Tanesco  wamekuwa wakiambiwa suala hilo litashughulikiwa. 

Josephat Michael ambaye ni Mmiliki wa mashine za kusaga eneo la Ibinzamata amesema wameathirika kiasi kikubwa kibiashara kutokana na kwamba wana mikopo kwa ajili ya kurejesha kwa taasisi husika.

“Tuna tatizo la umeme, tumeshindwa kufanya kazi na Tanesco imeshindwa  kutujulisha kuna tatizo gani.Tulifika ofisi ya Tanesco kitengo cha Dharura 'Emergency' na tukapatiwa namba ya Injinia lakini kila tukifanya mawasiliano na Injiania naye anasema tuwasiliane na kitengo cha emergency",amesema.

“Tunashindwa kufanya kazi na kupata fedha za kujikimu kwa ajili ya matatizo yetu,Tanesco wamekuwa wakifika hapa mara kwa mara lakini hakuna ufumbuzi wa tatizo letu. Tunashindwa kuelewa hii Transformer ina tatizo gani. Tunaiomba serikali itusaidie kuibadilisha hii transformer ili tuweze kufanya biashara zetu kama hapo awali", amesema Grace Malembeka.

 “Tatizo la umeme imekuwa ni changamoto hapa mara kwa mara na tuna familia zinatutegemea na ukizingatia tuna familia na sisi ndiyo Tegemezi wa familia zetu. Tunaomba watulete Transfoma mpya kuliko hii ambayo  imekuwa inaharibika mara kwa mara licha ya kutengenezwa na mafundi wa Tanesco",ameongeza Sara Charles.

Naye Elias Kajiba mmiliki wa kiwanda cha uchomeleaji vyuma amesema kero ya umeme imekuwa kikwazo cha maendeleo Ibinzamata hivyo kumuomba Waziri wa Nishati kusikia na kutatua kilio chao.

"Hii kero ya umeme imekuwa kero, ni vyema limfikie Waziri wa nishati kwa kuwa sisi tunaishi kwa kutegemea umeme kwa shughuli zetu na kuendesha familia ,kulipa ada shuleni  na pia tuna mrejesho ya mikopo, sasa Kama Rais anasema Kazi iendelee unadhani itaendeleaje bila umeme?”, amesema.

Kero hiyo ya umeme, pia imekuwa kikwazo kwa wabeba mizigo wa Ibinzamata  ambao wamesema kuwa ukosefu wa umeme umeathiri mzunguko wa pesa kwa kuwa uzalishaji katika mashine umekosekana na kuwafanya kuishi bila kupata riziki kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.

 Wabeba mizigo hao wamesema wao wanaishi kwa kutegemea ubebaji wa mizigo inayozalishwa kutoka katika mashine za nafaka.

Wafanyabiashara na wadau wameuomba uongozi wa Tanesco kuchukua hatua za kubadilisha Transformer  iliyopo Ibinzamata ili waweze kupata huduma ya umeme yenye uwezo wa kuendesha mashine zilizopo katika maeneo yao ya shughuli za ukoboaji na usagaji wa nafaka.

Wafanyabiashara hao wamesistiza kuwa eneo hilo limekuwa na tatizo la sugu kwa kuwa mara kwa mara wanakosa huduma ya umeme na licha ya kuripoti katika Shirika la Tanesco mkoa wa Shinyanga.

Hata hivyo, Meneja wa Tanesco mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi amesema anatambua tatizo la Wafanya biashara hao na kwamba tayari amefika katika eneo husika ili kutoa majibu ya Tanesco juu ya ukosefu wa umeme katika eneo hilo.

Meneja huyo wa Tanesco amesema amewaeleza Wafanya biashara hao kuwa, Ofisi yake imejipanga kushughulikia tatizo hilo na kulikalimilisha ifikapo Ijumaa tarehe 29, Oktoba 2021.

 “Ofisi ya Tanesco imepokea kero hii na tunajipanga na wataalam wetu kutatua tatizo hili kabla ya Ijumaa  Oktoba,29, 2021 kwa ubovu wa Transforma  hii umeleta tatizo kukosekana kwa umeme kwa wazalishaji wa nafaka katika eneo hili”,amesema Mhandisi Ntungi.

"Tumeongea na wamiliki wa mashine kuwa kwa kipindi hiki watapaswa kuwasha mashine zao za kusaga kwa kupeana zamu ili kuweza kuhimili kiwango cha umeme unaozalishwa ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku kuliko kukaa bila kufanya kazi wakati Tanesco ikiendelea na juhudi za kushughulikia tatizo hilo",ameeleza.

Amefafanua kuwa tangu tarehe 23.10.2021 walipata tatizo la Transformer na kulazimika kuwapa umeme kupitia transformer nyingine ambayo pia haina uwezo zaidi na kusababisha mashine saba kupata tatizo la ukosefu wa umeme kwa Wafanya biashara wa mashine za kusaga eneo la Ibinzamata.

"Ibinzamata ni eneo lenye mashine nyingi za kusaga  na kuna  Transfomer tatu za Tanesco  zinazohudumia mashine mbalimbali za Wafanyabiashara mashine za kusaga  na changamoto kubwa ni kuwa transformer moja imekuwa ikipata vumbi na kusababisha hitilafu ya umeme kuwepo eneo hilo mara kwa mara",amesema.
Meneja wa Tanesco mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi  akizungumza na waandishi wa habari
Wafanyabiashara wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka Ibinzamata wakizungumza na waandishi wa habari kuelezea kero ya umeme
Wafanyabiashara wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka Ibinzamata wakizungumza na waandishi wa habari kuelezea kero ya umeme
Transfoma inayoelezwa kuharibika mara kwa mara na kusababisha kero ya kukosa umeme kwa Wafanyabiashara wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka Ibinzamata 
Wafanyabiashara wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka Ibinzamata wakiwa wamebeba bango


Post a Comment

0 Comments