Header Ads Widget

ACT-WAZALENDO WALAANI MGOMBEA WAO ALIYETEULIWA KUGOMBEA UDIWANI NDEMBEZI,, KUENGULIWA GHAFLA


Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha ACT-Wazalendo Jimbo la Shinyanga Mjini Omari Gindu akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za ACT- Wazalendo Shinyanga Mjini.

Na Marco Maduhu- SHINYANGA.

CHAMA Cha ACT-Wazalendo Jimbo la Shinyanga Mjini, kimesikitishwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi Timothy Andrew, kumuengua ghafla Mgombea wao wa nafasi ya udiwani Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Mvano Iddy, na wakati awali alimtangaza na kumbandika kwenye ubao wa matangazo, kuwa amepitishwa kugombea udiwani na Tume ya Taifa ya uchaguzi NEC.

Katibu Mwenezi wa Chama hicho Jimbo la Shinyanga Mjini Omary Gindu, akizungumza na waandishi wa habari, leo, mara baada ya kupokea barua ya mgombea wao kutenguliwa uteuzi wake, na  kutokuwa mgombea tena wa nasafi ya udiwani Kata hiyo ya Ndembezi, amesema anasikitika sana kufanyiwa hujuma hizo.

Anasema Mgombea wao Mvano Iddy, alifuata taratibu zote za ujazaji fomu za kuteuliwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kugombea udiwani Kata ya Ndembezi kupitia chama chake cha ACT- Wazalendo, na akapitishwa na kutangazwa kuwa ni miongoni mwa wagombea ambapo wamepita, akiwamo yeye na Mgombea wa CCM Victor Mmanywa, lakini wanashangaa leo majira ya saa 9 alasiri, kupokea barua ya kutenguliwa.

“Leo majira ya saa 9 alasiri tumepokea barua kutoka kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Ndembezi, ikieleza kuwa mgombea wetu ametenguliwa kugombea udiwani, kwa sababu hakujaza fomu vizuri, sasa swali la kujiuliza kama hakujaza fomu vizuri, kwanini walmpitisha na kumtangaza kuwa ameteuliwa kugombea udiwani, na kumbandika kwenye ubao wa matangazo,”alihoji Gindu.

“Sisi tumepokea barua yao na tayari tumechukua fomu ya kukata Rufaa, lakini tunataka umma wajue uchafu ambao unafanywa na huyu msimamizi msaidizi wa uchaguzi, hatuna imani naye na huenda labda ametishwa na viongozi wa chama Tawala, ili kumuengua mgombea wetu, ili wakwao apite bila kupingwa, sababu wagombea wengine Tisa wameshawatoa Tayari, ambapo tulibaki ACT na CCM,”alisema Gindu.

Aidha aliiomba Tume ya Taifa ya uchaguzi NEC Makao makuu, kuingilia Kata suala hilo ambalo linaweza kutia doa uchaguzi huo mdogo wa udiwani, sababu ya figisufigisu ambazo zimeanza kufanyika, na wakati mgombea wao alikidhi vigezo akapitishwa na kutangazwa, lakini ghafla ameondolewa kwa sababu zisizo na msingi, na wakati wao walijiridhisha na ndiyo maana wakamteuwa.

Naye Mgombea huyo wa Udiwani Kutoka Chama cha ACT-Wazalendo Mvano Iddy, amesema amesikitishwa kufanyiwa rafu hizo, na kuitaka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC)kutenda haki, na kuimarisha demokrasia hapa nchini, na kama wataendelea hivyo ni bora wafute mfumo wa vyama vingi, na kibaki chama kimoja tu cha CCM.

Kwa upande wake msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika uchaguzi huo mdogo wa Kata ya Ndembezi Timothy Andrew, alikiri mgombea huyo kupitishwa na kutangazwa kugombea udiwani kwenye Kata hiyo, na kueleza kuwa baada ya kumbandika kwenye mbao za matangazo, mgombea mwezake wa CCM Victor Mmanywa, akatoa pingamizi kuwa hakujaza fomu ya maadili, na walipopitia fomu zake ndipo wakabaini dosari hiyo na kuamua kumuengua, na kubaki mgombea pekee wa CCM kuwa ndiye aliyekidhi vigezo.

Aidha amesema hata hivyo wameshatoa nafasi ya kukata Rufaa kwa chama hicho, na wataipitia Rufaa yao ili kujiridhisha zaidi, ndipo watatoa maamuzi ya mwisho kama wamrudishe au mgombea wa CCM apite bila ya kupingwa.

Aidha jana msimamizi huyo msaidizi wa uchaguzi, alimtangaza Mvano Iddy wa ACT-Wazalendo kuwa amepitishwa kugombea udiwani na Tume ya Taifa ya uchaguzi, pamoja na Victor Mmanywa wa CCM kuwa wao ndiyo wamekidhi vigezo, na kuondolewa wagombea wengi Tisa kuwa hawajakidhi vigezo, ikiwa ujazaji wa fomu vibaya, pamoja na kutorudisha fomu.

Uchaguzi huo mdogo Kata ya Ndembezi, unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa Kata hiyo David Nkulila, ambaye pia alikuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga, na alifariki Agost mwaka huu, kwa matatizo ya ugonjwa wa Moyo.


Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha ACT-Wazalendo Jimbo la Shinyanga Mjini Omari Gindu akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za ACT- Wazalendo Shinyanga Mjini.

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Mdogo Kata ya Ndembezi Timothy Andrew, akipitia vifungu ya kanuni vya uchaguzi, na kueleza sababu za Mgombea huyo kuenguliwa licha ya hapo awali kumtangaza kuwa amepita kuwania nasafi hiyo ya udiwani Kata ya Ndembezi kupitia ACT-Wazalendo.

Mgombea Udiwani Kata ya Ndembezi Mvano Iddy, kupitia chama cha ACT-Wazalendo, akitoa masikitiko yake ya kuenguliwa jina lake ghafla, ili abaki Mgombea wa CCM peke yake na kupitia bila ya kupingwa.

Muonekano wa Fomu ya uteuzi wa Mgombea huyo wa ACT-Wazalendo Mvano Iddy kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC ,kuwa ameteuliwa kugombea nafasi ya Udiwani Kata ya Ndembezi.


Muonekao wa barua ya kutenguliwa leo Saa 9 alasiri.

Na Marco Maduhu- SHINYANGA.

Post a Comment

0 Comments