Header Ads Widget

WANACHAMA 'WHATSAPP GROUP' WATOA MSAADA MITUNGI YA OKSIJENI HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA


Mratibu wa Whatsapp Group ya ‘Okoa Uhai Nunua Mitungi’ Shinyanga bw. Gwakisa Mwasyeba (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kushoto)  Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wa UVIKO -19 wanaopata changamoto ya upumuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga leo Jumatano Septemba 22,2021.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp ‘Okoa Uhai Nunua Mitungi’ wametoa msaada wa Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni yenye thamani ya shilingi 695,000/= kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wa UVIKO -19 wanaopata changamoto ya upumuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Hafla fupi ya makabidhiano ya Mitungi hiyo ya Gesi ya Oksijeni imefanyika leo Jumatano Septemba 22,2021 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko.

Akipokea mitungi ya Gesi ya Oksijeni, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amewapongeza wanachama wa Kundi la Whatsapp la Okoa Maisha Nunua Mitungi kwa upendo mkubwa waliouonesha kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa.

“Nawapongeza sana mmetumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kusaidia jamii. Watu wengi wanatumia Mitandao ya Kijamii kusogoa tu stori na kupost picha lakini nyinyi mmeamua kutumia Group la Whatsapp kuhamasishana na kuchangishana fedha kwa ajili ya kununua mitungi ya Gesi ya Oksijeni ili kuokoa maisha ya wagonjwa. Hongereni sana na endeleeni na moyo huu na watu wengine waige kutoka kwenu”,amesema Mboneko.

Mkuu huyo wa wilaya amewaomba watumiaji wa mitandao ya kijamii kutumia mitandao kwa manufaa kwa kusaidia watu wenye uhitaji na kushiriki katika shughuli za maendeleo kwani maendeleo yanaletwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali.

Mboneko amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa UVIKO 19 huku akiwahamasisha kujitokeza kupata chanjo ya Corona na watoa huduma za afya kuendelea kuhudumia vizuri wagonjwa huku wakichukua tahadhari dhidi ya Uviko – 19.

“Tunashukuru sasa Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga tuna mitungi ya kutosha ya Gesi ya Oksijeni lakini tunaomba wadau waendelee kujitokeza kusaidia kwa kujaza gesi ya Oksijeni kwenye mitungi hii ili tuendelee kuwasaidia wagonjwa”,amesema.

Akikabidhi Mitungi ya Gesi ya Oksijeni, Mratibu wa Whatsapp Group ya ‘Okoa Uhai Nunua Mitungi’ Shinyanga bw. Gwakisa Mwasyeba amesema mnamo mwezi Julai 2021 walianzisha Kikundi hicho na kuanza kuchangishana fedha kwa ajili ya kununua mitungi ya Gesi ya Oksijeni ili kusaidia kutatua changamoto ya upungufu wa mitungi ya gesi hiyo kwa ajili ya upumuaji kwa wagonjwa wa UVIKO 19 kwa baadhi ya maeneo katika mkoa wa Shinyanga.

“Tulianzisha Group la Whatsapp lenye wanachama 83 na kati yao wanachama 21 waliweza kutoa mchango na ahadi na hadi kufikia Septemba 22,2021 kiasi cha shilingi 695,000/= kimekusanywa kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu na kufanikiwa kununua mitungi hii ya Gesi ya Oksijeni”,amesema.

“Mhe. Mkuu wa wilaya kilichotolewa ni kidogo lakini kinaweza kusaidia maisha ya watu kwa kiasi kikubwa. Lakini kutoa ni moyo wala siyo utajiri.Pia katika hospitali zetu mambo mengi yanahitajika ikiwemo utoaji wa damu kwa ajili ya wagonjwa na kufanya usafi hivyo Watanzania wenzangu naomba tujitokeze kuokoa maisha yaw engine kwa kile ulichojaliwa bila kuangalia uchache wake”,amesema Mwasyeba.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Richard Mhangwa amekishukuru kikundi hicho cha Whatsapp kwa msaada huo akisema mitungi hiyo ya Gesi ya Oksijeni itasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa.

“Asanteni sana mmetumia vizuri mitandao ya kijamii na mmekuwa marafiki wa hospitali yetu. Mitungi hii 10 ya Gesi ya Oksijeni ni mingi na itasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa na itaturahisishia kutoa huduma kwa wagonjwa. Mwezi Julai 2021 tulikuwa na changamoto kubwa ya uhaba wa Mitungi ya Gesi ya Oksijeni”,amesema Dkt. Mhangwa.
Mratibu wa Whatsapp Group ya ‘Okoa Uhai Nunua Mitungi’ Shinyanga bw. Gwakisa Mwasyeba (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wa UVIKO -19 wanaopata changamoto ya upumuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga leo Jumatano Septemba 22,2021. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kulia) akimkabidhi Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Richard Mhangwa Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni iliyotolewa na Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi'
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kulia) akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni iliyotolewa na Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi'.
Muonekano wa Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni iliyotolewa na Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi'.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni iliyotolewa na Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi'.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni iliyotolewa na Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi'.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko  akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni iliyotolewa na Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi'.
Mratibu wa Whatsapp Group ya ‘Okoa Uhai Nunua Mitungi’ Shinyanga bw. Gwakisa Mwasyeba akitoa taarifa ya ununuzi wa mitungi ya gesi ya Oksijeni kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kulia)
Mratibu wa Whatsapp Group ya ‘Okoa Uhai Nunua Mitungi’ Shinyanga bw. Gwakisa Mwasyeba akitoa taarifa ya ununuzi wa mitungi ya gesi ya Oksijeni kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko
Watoa huduma za afya na wanachama wa  Whatsapp Group ya ‘Okoa Uhai Nunua Mitungi’ Shinyanga wakiwa katika hafla fupi ya makabidhiano ya mitungi ya gesi ya Oksijeni
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akikishukuru  Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi' kusaidia Mitungi 10 ya Gesi ya Oksijeni.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (mwenye nguo nyekundu)  akipiga picha na Watoa huduma za afya na Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi'.
Sehemu ya Wanachama wa Kikundi cha Whatsapp 'Okoa Uhai Nunua Mitungi' wakipiga picha ya kumbukumbu.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Post a Comment

0 Comments