Header Ads Widget

WAKAZI WA VIWANJA VYA MWADUI WAKUBALI KUCHANGA KURASIMISHA ENEO LAO… WANAOWATUMA ‘HOUSE GIRL’ KWENYE UPIMAJI MAENEO WAONYWA

Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Emmanuel Mitinje akizungumza na baadhi ya wakazi wa mtaa wa Viwanja vya Mwadui Kata ya Ngokolo juu ya zoezi la urasimishaji wa eneo lao na taratibu zake, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 15, 2021 shule ya msingi Mwadui.

Na Damian Masyenene, Shinyanga
WAKAZI wa Mtaa wa Viwanja vya Mwadui Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga wamekubali kuhamasishana kuchanga Sh 130,000 kila mmoja mwenye kiwanja katika eneo hilo kwa ajili ya kufanyiwa urasimishaji katika eneo lao ili kuepuka migogoro ya ardhi.

Uamuzi huo umefikiwa jana Juni 15, 2021 katika mkutano wa hadhara wa serikali ya mtaa huo uliofanyika katika Shule ya Msingi Mwadui ukihudhuriwa na Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu (CCM), Afisa Ardhi wa Manispaa ya Shinyanga, Mussa Makungu pamoja na Mratibu wa zoezi la urasimishaji makazi katika manispaa hiyo, Emmanuel Mitinje ambaye pia ni Afisa Mipango Miji wa manispaa hiyo.

Mtaa wa Viwanja vya Mwadui una takribani wakazi 30,000 na kaya 800, ambapo Wakazi hao wamekubaliana kuchangia kiasi hicho cha fedha kuanzia Juni 15, mwaka huu hadi Novemba mwaka huu uchangishaji ukamilike na zoezi la urasimishaji lifanyike Desemba, mwaka huu, ambapo pia waliunda kamati ya watu watano itakayosimamia zoezi hilo la uhamasishaji na urasimishaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Viwanja vya Mwadui, Nuru Magohe alisema kuwa mtaa huo unazidi kukua na eneo la shule linavamiwa na shule hiyo ina wanafunzi wengi kuliko shule zote kwenye manispaa ya Shinyanga, hivyo akaomba maofisa wa idara ya ardhi wasaidie mchakato wa kurasimisha eneo jipya kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya itakayopewa jina la Mwadui B.

“Mtaa wetu unakua wafanyabiashara ni wengi, ni vyema sasa tukaambiwa eneo letu la Soko lililotengwa ni lipi,” alisema.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Mwidini Hamza alihoji kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya wizara juu ya punguzo la urasimishaji, huku akiomba halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kutoa ramani ya eneo hilo ili kupunguza migogoro ya ardhi na uvamizi wa maeneo ya watu na ujenzi holela kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.

Naye Ignas Banyemaa alitaka kufahamu hatma ya eneo la Shule ya sekondari Town ambalo wakazi wake walipimiwa maeneo yao mwaka 2014 na wakalipia wakiahidiwa kuletewa hati za urasimishaji lakini hadi leo zoezi hilo halijafanikiwa, hivyo akataka kufahamu kama kwenye zoezi hili jipya nao watalipia tena.

Akitolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali, Afisa Mipango Miji Manispaa ya Shinyanga, Emmanuel Mitinje amesema kuwa lengo kubwa la Serikali ni kuboresha makazi ili yaweze kupata huduma muhimu na kila mwananchi aweze kupata hatimiliki, huku akiwaomba washirikiane kwa pamoja ili zoezi lifanikiwe.

Akielezea kuhusu eneo la Kashuwasa linalomilikiwa na mtu anayefahamika kwa jina la Mama Salamba, alisema kuwa hawawezi kuingilia maamuzi ya Mahakama kwa sababu lile eneo shauri lake bado lipo mahakamani, huku akieleza kuwa upimaji eneo la Town School uliofanyika mwaka 2014 ulifanywa na mpimaji binafsi na upimaji wake haukukamilika, na kwakuwa hawajui changamoto gani alizokutana nazo kwa sasa wanaweka utaratibu mzuri ili kukamilisha upimaji huo, ambapo aliwaomba wakazi wa eneo hilo kuwa wavumilivu wakati mchakato unakamilishwa.

Mitinje ambaye pia ni Mratibu wa zoezi la Urasimishaji Manispaa ya Shinyanga alieleza kuwa lengo ni kutoa elimu ya urasimishaji wananchi waandaliwe hatimiliki ili kuboresha makazi yao waweze kufikiwa na huduma muhimu na wanufaike na ardhi yao, ambapo mazoezi hayo yamenufaisha wananchi wengi na tayari katika halmashauri hiyo wameshazifikia kata 10 kati ya 17 na lengo ni kabla ya mwaka 2023 Kata zote zifikiwe wananchi wapate hatimiliki.

“Nawaomba mchangie kwa wingi ili upimaji ufanyike haraka, kasi ndogo ya uchangaji pesa za upimaji itachelewesha zoezi. Zoezi hili ni la kwenu mwitikio wenu ndiyo utakaofanikisha hili. Katika uundaji wa kamati ya urasimishaji wa eneo lenu, kamati inapaswa kuwa na watu watano lakini isihusishe viongozi wa serikali ya Mtaa, iwe ni kamati ya wananchi, wawe wakazi na walau wawe na kiwanja hapa na iyafahamu maeneo ili itusaidie na wajumbe wawe wanajua kusoma na kuandika,” alifafanua Mitinje.

Awali Afisa Ardhi wa Manispaa ya Shinyanga, Mussa Makungu alibainisha kuwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na migogro ya ardhi ni mtaa wa Viwanja vya Mwadui kutokana na baadhi ya wamiliki wa ardhi wamekuwa wakiwatuma wasaidizi wa kazi za ndani kuwawakilisha kwenye zoezi la upimaji wakati hawana ufahamu wa mipaka ya maeneo hayo.

Makungu aliwaomba wamiliki wa viwanja kuhudhuria wenyewe kwenye upimaji wa maeneo yao, huku akieleza kuwa upimaji shirikishi ndiyo mzuri kuliko ule wa mtu mmoja mmoja.

“Zoezi la urasimishaji kwa Manispaa ni Sh 130,000 kwa kiwanja kimoja kwa mtu binafsi, kwa taasisi ni Sh. 500,000 kutokana na ukubwa wa eneo na mahitaji yake. Watu wengi hawana hati miliki hivyo wanakuwa na hofu muda wote, faida za hatimiliki ni kupata mkopo, kumdhamini ndugu anapohitaji dhamana kwahiyo hatimiliki ina faida nyingi,” alieleza.

Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu alieleza kuwa zoezi hilo ni moja ya ahadi zake kwa wananchi kuhakikisha wanaondoa migogoro ya ardhi, ambapo amewahimiza wananchi hao kutoa ushirikiano kwa maofisa wa idara ya ardhi na wachangamkie fursa hiyo ili kupimiwa maeneo yao na kurasimishiwa waweze kuyamiliki kihalali.
Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Emmanuel Mitinje akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za wakazi wa eneo la Viwanja vya Mwadui Kata ya Ngokolo juu ya zoezi la urasimishaji wa eneo lao, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 15, 2021 shule ya msingi Mwadui.
Afisa Ardhi wa Manispaa ya Shinyanga, Mussa Makungu (kushoto) akiwaeleza wananchi hao taratibu zinazopaswa kufuatwa kurasimishiwa eneo lao.
Wakazi wa eneo la Viwanja vya Mwadui kata ya Ngokolo wakimsikiliza Afisa Ardhi wa Manispaa ya Shinyanga, Mussa Makungu (kulia) akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali
Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu (katikati) na Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwanja vya Mwadui, Nuru Magohe (wa tatu kushoto) wakisikiliza hoja za wananchi wakati wa kikao hicho)
Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu akiwaeleza wananchi manufaa ya zoezi la urasimishaji makazi yao pamoja na kuwataka wachangamkie fursa hiyo
Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwanja vya Mwadui, Nuru Magohe akieleza kero mbalimbali za ardhi zinazoukumba mtaa wake
Kikao kikiendelea na wananchi wakitoa maoni mbalimbali juu ya zoezi hilo
Wananchi wakisikiliza kwa umakini ufafanuzi na maelekezo kutoka kwa viongozi wao
Wananchi wakisikiliza ufafanuzi wa hoja mbalimbali wakati wa kikao hicho
Kikao kikienddelea
Wananchi wakisikiliza ufafanuzi kutoka kwa viongozi wao
Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea
Wananchi wakifuatilia kikao hichoPost a Comment

0 Comments