Header Ads Widget

MRADI WA PAMOJA WA VYAMA VYA USHIRIKA VYA PAMBA KULETA MATUMAINI KWA WAKULIMA

Mwenyekiti wa chama cha ushirika mkoa wa Shinyanga, (SHIRECU) akizungumza kwenye mkutano huo.

Na Suzy Luhende, Shinyanga
Mwenyekiti wa Bodi anzilishi wa mradi wa pamoja wa Vyama Vikuu vya Ushirika vya Pamba Tanzania Cotton Cooperatives Joint Enterprise Limited (TANCCOPS) Benjamin Mikomangwa amesema mradi huo unatarajia kutoa huduma bora kwa wanachama na kwa wakulima wa zao la pamba chini ya dhana ya umoja ni nguvu na kuimarisha sekta ya ushirika nchini.

Hayo ameyasema jana kwenye Mkutano Mkuu wa kwanza uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa SHIRECU mjini Shinyanga, ambapo amesema lengo la mradi huo ni kuimalisha sekta ya ushirika wa pamba nchini na kutoa huduma kwa wakulima na wanachama wote chini ya umoja ni nguvu.

Mikomangwa amesema bodi hiyo ambayo imesajiliwa na Mrajis wa vyama vya ushirika Februari 26,2020 kwa hati ya usajili namba 5618 kuwa taasisi ya kisheria chini ya sheria ya vyama vya ushirika namba sita ya mwaka 2013 ambayo makao makuu yake ni Shinyanga mjini.

"Mpaka sasa kuna vyama vikuu vya ushirika vya pamba 17,ambapo 12 vimekwishatoa viingilio na kununua hisa na viwili vinaendelea kukamilisha mchakato huo, na uanachama wa (TANCCOPS) ni kwa vyama vikuu vyote vya pamba nchini," amesema Mikomangwa.

Naye Meneja Mkuu Chama cha Ushirika Geita, Venance Msiba amesema bodi hiyo itahakikisha AMCOS zote za pamba zinatumia mizani sahihi ambayo itanunuliwa mipya kwa bei nafuu, na kuhakikisha bodi hiyo inatoa elimu sahihi kwa wakulima wa zao la pamba.

Mwenyekiti wa chama cha ushirika Singida, Yahaya Hamis lengo letu la kuwa na bodi hii ni kuendelea kumhamasisha mkulima wa zao la pamba aendelee kulima na kuhakikisha anapata bei nzuri na pembejeo na alime kwa wakati unaotakiwa kulingana na mvua.

Naye makamu mwenyekiti wa Igembesabo-Tabora, Samwel Ibrahimu amesema wakulima wengi wa zao la pamba wamekata tamaa kutokana na bei elekezi ilikuwa haieleweki ambapo ilianzia 600, 810 na mwaka 2020/ 2021ilikuwa 940, hadi 1,050.hivyo bodi hiyo inaendelea kuhamasisha wakulima ili waendelee kulima zao hilo kwa sababu linategemewa kwa ajili ya kutengenezea nguo na kutoa ajira vijana.

Katika mkutano huo ambao ulisimamiwa na Mwenyekiti wa muda, Kwiyolecha Nkilijiwa ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) amesema lengo lao baada ya kumaliza majadiliano yao walitakiwa kufanya uchaguzi wa viongozi lakini ilishindikana kutokana na majina ya wagombea yalipokelewa lakini hayakujadiliwa na serikali.

Kwa upande wake Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniface alisema baada ya kumaliza majadiliano ilitakiwa kufanyika uchaguzi wa viongozi wa bodi lakini umeahirishwa mpaka pale serikali itakapoyapitia majina ya wagombea ndipo utafanyika.

Bodi hiyo imeunda umoja wa viongozi wa vyama vya ushirika kutoka Mwanza, Geita, Mara, Singida, Tabora, Simiyu, Chato na Shinyanga.
Mshauri Mwelekezi wa mkutano wa
bodi hiyo, Joseph Mihangwa akizungumza wakati wa mkutano huo
Meneja Mkuu wa Chama cha Ushirika Mkoa wa Geita, Venance Msiba (kushoto) akifafanua jambo kwenye mkutano huo
Wajumbe wa chama hicho wakipitiia nyaraka mbalimbali wakati wa mkutano huo


Post a Comment

0 Comments