Header Ads Widget

DPP MWAKITALU ATEMBELEA NA KUKAGUA HALI YA MAGEREZA UKONGA NA KEKO JIJINI DAR ES SALAAM, AAHIDI KUZITAFUTIA UFUMBUZI CHANGAMOTO

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw.Sylvester Mwakitalu (mwenye suti nyeusi) akiwa ameongozana na Mkuu wa Gereza la Ukonga SSP Hamis Lissu (kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Magereza na kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakitembelea Maeneo mbalimbali ya gereza la Ukonga kujionea hali halisi ya gereza hilo.

Na Rebeca Kwandu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amefanya ziara ya ukaguzi  katika Magereza ya Keko na Gereza Kuu Ukonga ya jijini Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya magereza hayo, kuzugumza na mahabusu pamoja na wafungwa na kuahidi kushirikiana na vyombo vingine kutatua changamoto zinapelekea kuwepo kwa msongamano  ndani ya magereza hayo.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo aliyoongozana na baadhi ya  watendaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dar es Salaam , Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Mwakitalu amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi ya magereza, kuwasikiliza mahabusu  na wafungwa ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili  mahabusu na wafungwa kufuatia kesi mbalimbali zilizoko mahakamani.

“Ujio wangu hapa ni kwa ajili ya kujionea hali halisi ya msongamano  pamoja na kusikiliza kero za mahabasu, wafungwa na magereza kwa ujumla ili niweze kufanyia kazi maeneo yale yanayohusu ofisi yangu  “Alisema DPP Mwakitalu.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema Magereza mengi nchini yanakabiliwa na msongamano mkubwa wa  wafungwa na mahabusu kutokana na sababu mbalimbali  ikiwemo kuongezeka kwa hali ya  uhalifu nchini.

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu amewataka watanzania kuacha kujihusisha na uhalifu hali ambayo inachangia kuongezeka kwa msongamano magerezani huku akiahidi kufanya kazi kwa nguvu na bidii ili mashauri yaweze kusikilizwa kwa haraka na wakati.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Mashtaka ametembelea na kujionea uzalishaji mkubwa wa Bidhaa (Fanicha) zinazotengenezwa na wafungwa katika gereza kuu Ukonga

Ziara hiyo ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini  imelenga katika  kusikiliza, kupokea malalamiko na changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya mashtaka ili ofisi yake iweze kuyatafutia ufumbuzi ili kupunguza changamoto na  msongamano magerezani.

Katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka ameambatana na  Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa  Shughuli za Mashtaka  na Upelelezi  Bw. Oswald Tibabyekomya, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam  Bi. Mkunde Mshanga na Wakuu wa Mashtaka Wilaya zote za  Dar es Salaam. 

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu akiwa ameambatana na Viongozi wengine wakati wa zoezi la kutembelea magereza ya Ukonga na Keko Jijini Dar es Salaam mapema leo Juni 12,2021.


Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam SSP Hamis Lissu akimuongoza Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu pamoja na timu yake wakati walipotembelea Gerezani hapo Mapema leo Juni 12,2021
Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam SSP Hamis Lissu akimueleza jambo  Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester juu ya hali ilivyo katika gereza hilo.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu akipokea maelezo ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali unaofanywa na Jeshi la Magereza Ukonga kutoka kwa Mkuu wa kiwanda SP Edger Kaiza leo Juni 12,2021.
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester akiwa katika picha ya Pamoja na Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam SSP Hamis Lissu mara ya Kutembelea na Kukagua Magereza hiyo. 

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu  akiwaaga Maafisa wa Jeshi la Magereza Nchini katika Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika gereza hilo. 

Post a Comment

0 Comments