Header Ads Widget

DC MACHA AONYA WANAOENEZA UZUSHI KUWA KINGATIBA YA KICHOCHO NA MINYOO WANAYOPEWA WANAFUNZI NI CHANJO YA CORONA

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha

Na Neema Sawaka, Kahama
MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Anamringi Macha amewataka wananchi kuacha kuzusha uvumi kuwa kinga tiba ya minyoo na kichocho dawa wanazonyweshwa wanafunzi wa shule za msingi ni chanjo ya Virusi vya Korona (COVID-19), kitendo ambacho kinachokwamisha utekelezaji wa zoezi hilo.

DC aliyasema hayo wakati alipokuwa akizindua mpango rasmi wa Serikali wa dawa za kichocho na minyoo kwa Wanafunzi wa shule za Msingi Majengo iliyopo Manispaa ya Kahama mkoani hapa.

Aidha alisema kuwa wapo watu wanaoongoza uvumi kwamba hiyo ni dawa ya Virusi vya Corona na kuongeza kuwa serikali ipo makini na haiwezi kuangamiza watu wake, ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaonya na kuahidi kuchukua hatua dhidi ya wanaoeneza uvumi kuwapotosha wenzao.

“Ndugu zangu dawa hizi ni kwaajili ya kuhakikisha kuwa watoto wetu wanajikinga na magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi uhumimu ama kipaumbele wakati mwingine wanaweza kukondeana ambapo mtoto anakula chakula na minyoo nayo inakula, kwa hiyo unaweza kudumaa ukadumaza akili wataalamu wanasema inaweza hata kukusababishia kifo,” alisema Macha.

Shule ya msingi Majengo ni miongoni mwa shule 114 yenye jumla ya wanafunzi 3510 kati yao 3424 watapata dawa hizo za minyoo na kichocho, kwa mana hiyo hatuna sababu yoyote ya kupata matatizo ya magonjwa ambayo uwezo wa kuyatibu tunao.

Pia Mkuu wa Wilaya aliwaeleza wazazi kuwa ili kudhibiti magonjwa hayo wazazi wanapaswa kuzingatia watoto kuvaa viatu kwakuwa kutovaa viatu ni jia hatarishi ya maambukizi hayo na kuwasisitiza walimu nao kuzingatia suala la usafi katika vyoo vinavyotiririsha hovyo maji machafu na kuhakikisha watoto hao wanavaa viatu ili kuepuka maradhi ya kichocho na minyoo.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dkt. Lucas David alisema kuwa siku hiyo ni maalumu ya kuadhimisha utoaji wa dawa za minyoo na kichocho kwa watoto katika shule za msingi katika manispaa hiyo huku akibainisha kuwa lengo katika halmashauri ya manispaa ni kuwafikia walengwa 88,907 wanaostahili kupata dawa za minyoo na kichocho katika shule 114.

“Kwa ushirikiano wa walimu na wahudumu wa afaya waliopo zoezi litakwenda vizuri kama lilivyo agizo la serikali, niwaombe wazazi tuendelee kuruhusu watoto wetu waje kupata kinga na tiba hii muhimu sana,” alisema Dkt. Lucas David.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu msingi Mkoa wa Shinyanga Dekan Lutanziga alieleza kuwa kwa mwanafunzi ambaye hatakunywa dawa za minyoona kichocho maradhi hayo yakimkumba ukuaji wake ni wa udumavu, pia masomo darasani hawezi kuyazingatia vizuri.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa utoaij wa kingatiba hiyo katika halmashauri ya msalala, Mwakilishi wa ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk. Peter Mlacha alisema kuwa zoezi hilo ni la kiserikali na kwa mkoa wa shinyanga wanategemea kuwafikia walegwa 460,075 kuanzia umri wa miaka 5 hadi 14 na kwa halmashauri ya msalala ni walengwa 83,071.

Dk. Mlacha aliongeza kwa kueleza kuwa kinga tiba hiyo itawasaidia kuwatibu wale ambao watakutwa na kichocho na minyoo na wale ambao hawatakuwa na kichocho na minyoo itatumika kuwakinga dhidi ya magojwa hayo kwani yasipotibiwa yanaweza kuleta madhara kwenye ini, utumbo, haja kubwa na ubongo.

Mmoja wa wakazi wa Kata ya Kakola katika halmashauri ya Msalala, Sabina Joachimu aliwahimiza wazazi kuwaruhusu watoto wapate huduma hiyo kwani minyoo na kichocho ni hatari zaidi kuliko wanavyodhani.

“Kwa kweli mimi naunga na Mkuu wa Wilaya sisi wengine tulishakumbana na maradhi hayo, sasa serikali inapojitokeza kusaidia wananchi nao wakubali kusaidiwa kwani hii dhana potofu iliyojengeka miongoni mwao siyo sahihi, ndiyo maana watoto wanapougua tunaingiza masuala ya imani za ushirikina kwamba amerogwa wakati ni minyoo,” alisema Sabina.


Post a Comment

0 Comments