Header Ads Widget

WAZAZI SHINYANGA WANAOTUMIA MIMBA ZA UTOTONI KAMA FURSA YA KIPATO WAONYWA


Katibu wa Shirika la Young Women's Association (YWCA) la mkoani Shinyanga ambalo linatekeleza mradi wa kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, Marysiana Makundi akizungumza kwenye kikao na wajumbe wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwenye kata hiyo.

Na Marco Maduhu, Shinyanga
BAADHI ya Wazazi na Walezi mkoani Shinyanga, wameonywa tabia ya kutumia mimba za utotoni kama fursa  kwa kumaliza kesi kimya kimya na watuhumiwa, kwa kupewa pesa ama mifugo na kusababisha wahalifu kutofungwa jela, hali ambayo inachochea vitendo hivyo kuendelea ndani ya jamii mkoani humo na kuzima ndoto za wananafunzi wa kike.

Onyo hilo limetolewa leo na Katibu wa Shirika la Young Women's Association (YWCA) la mkoani Shinyanga ambalo linatekeleza mradi wa kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, Marysiana Makundi, kwenye kikao chao na wajumbe wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya kata hiyo.

Merysiana amesema kwamba baadhi ya wazazi mkoani humo wamekuwa kikwazo kikubwa cha kumaliza tatizo la mimba za utotoni, kutokana na kugeuza mimba hizo kama fursa za kujipatia mali, ambapo kesi inapokuwa ikiendelea mahakamani wao huenda kumalizana na upande wa mtuhumiwa, kwa kupewa pesa ama mifugo na kisha kuacha kuhudhuria mahakamani kutoa ushahidi na baadae kesi kufutwa.

“Mimi nilishakutana na kitu kama hiki, kuna kesi moja nilikuwa naishughulikia ya mwanafunzi kupewa ujauzito, lakini cha ajabu wazazi wa huyo binti wakakutana na upande wa mtuhumiwa wakamailizana kwa kupeana fedha, Wakati huo nilikuwa sijui, nikashangaa nikaanza kukosa ushirikiano kutoka kwao hadi kesi ikafutwana mtuhumiwa akachiwa huru.

“Niwaambie tu wazazi wa Shinyanga, tuache hii tabia ya kugeuza fursa mimba hizi za utotoni kwa malengo ya kujipatia pesa ama mifugo, wanaoumia ni watoto sababu wanazima ndoto zao na kuingia kwenye majukumu ya kiutuuzima ambayo hawayawezi, hivyo naomba tuungane kwa pamoja kutokomeza huu ukatili dhidi ya watoto,” ameeleza.

Katika hatua nyingine, Merysiana amewasihi wazazi na walezi kuacha kuendekeza mila na desturi kandamizi ambazo zimeshapitwa na wakati, ambazo ndio zimekuwa chanzo cha kuendelea kuwepo kwa matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Kat ya Ibadakuli, Mwijage Patrick, amewaomba wazazi kujenga utamaduni pia wa kuzungumza na watoto wao juu ya makuzi yao pamoja na kuwapatia elimu ya afya ya uzazi, sambamba na kufuatilia mienendo yao ili kuwaepusha dhidi ya matukio ya ukatili.

Kwa upande wake Polisi Kata wa Ibadakuli, Emmanuel Maganjila, amewahimiza watoto kupaza sauti dhidi ya matukio ya ukatili, kwa kutoa taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria, huku akiwataka wadau waendelea kutoa elimu ya ukatili kwa wananchi na kuwaeleza madhara yake.

Mmoja wa waelimishaji masuala ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii, Mary John, amesema jamii inapaswa kubadilika na kuwaona watoto wa kike wapo sawa na wakiume, na kuacha kuwafanyia matukio ya ukatili ambayo huaribu ndoto zao pamoja na wengine kuathirika kisaikolojia.

Afisa Miradi wa Shirika la YWCA, John Eddy akiongoza mjadala kwenye kikao hicho.
Mtendaji wa Kata ya Ibdakuli, Sara Wamkuru akizungumza kwenye kikao hicho.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Ibadakuli, Mwijage Patrick akizungumza kwenye kikao hicho.
Polisi Kata ya Ibadakuli, Emmanuel Maganjila, akizungumza kwenye kikao hicho
Wajumbe wakiwa kwenye kikao.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao.


Post a Comment

0 Comments