Header Ads Widget

WATUMISHI 11 SHINYANGA WAREJESHWA KAZINI BAADA YA KUSIMAMISHWA KWA UTORO, DED AFAFANUA ZAHANATI KUKOSA MTUMISHI KWA MIEZI 3

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba akijibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa madiwani wakati wa kikao cha robo ya tatu ya barza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika Mei 7, 2021

Na Damian Masyenene, Shinyanga
WATUMISHI 11 wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa wamerejeshwa kazini na kupewa onyo kali baada ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na utovu wa nidhamu wakikabiliwa na makosa ya utoro kazini.

Uamuzi wa kuwarejesha watumishi hao umefikiwa leo Mei 7, 2021 na madiwani wa halmashauri hiyo katika kikao cha robo ya tatu kilichofanyika leo, huku changamoto ya uhaba wa watumishi katika halmashauri hiyo ukielezwa kuwa ndiyo sababu kuu iliyofanya warejeshwe.

Akitangaza uamuzi huo wakati wa kufunga kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Ngasa Mboje amesema kuwa watumishi hao kamati maalum ya baraza la madiwani imeridhia kuwarejesha watumishi hao 11 kwa maslahi ya halmashauri na wengine watatu mashauri yao yaanze upya ili nao wajue hatma yao.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba amesema kuwa watumishi hao walikuwa wanakabiliwa na makosa ya utoro kazini kwa muda mrefu uliotokana na kuhamishwa kwa makao makuu ya halmashauri hiyo kutoka mjini Shinyanga kwenda Iselamagazi.

“Kwahiyo walisimamishwa na wengine kufukuzwa. Lakini kutokana na changamoto ya uhaba wa watumishi katika halmashauri yetu imebidi wapewe onyo la kutorudia kosa na kurejeshwa kazini, kwa maana kwamba watarudi kazini na endapo watarudia tena basi wataondoshwa moja kwa moja,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mahiba ametolea ufafanuzi wa Zahanati tatu katika halmashauri hiyo kuwa na mtumishi mmoja tu, huku zahanati ya Mendo ikiwa haina mtumishi hata mmoja, ambapo ameeleza kuwa changamoto hiyo inatokana na uhaba wa watumishi unaoikabili halmashauri yake.

Mahiba ametoa ufafanuzi huo kufuatia swali la papo hapo kutoka kwa Diwani wa Kata ya Ilola, Amos Mshandete aliyetaka kufahamu ni kwanini Zahanati ya Mendo iliyopo katika kata hiyo haina mtumishi tangu Machi, mwaka huu baada ya aliyekuwepo kustaafu kazi.

“Zahanati hiyo ilikuwa na mtumishi mmoja na ni miongoni mwa zahanati tatu ambazo zina mtumishi mmoja mmoja, tunafanya taratibu za upata mtumishi mpya,” alifafanua Mkurugenzi huyo.
Diwani wa Kata ya Ilola, Amos Mshandete akihoji ni kwanini zahanati ya Mendo iliyopo kwenye kata yake haina mtumishi hata mmoja baada ya aliyekuwepo kustaafu


Post a Comment

0 Comments