Header Ads Widget

WACHIMBAJI WADOGO SHINYANGA WAPEWA MAFUNZO UTUMIAJI TEKNOLOJIA NA KUACHA UCHIMBAJI HOLELA

Afisa Madini Mkazi mkoa wa Shinyanga, Joseph Kumbulu akizungumza kwenye mafunzo ya wachimbaji wadogo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa CCM mkoaa Shinyanga

Na Suzy Luhende, Shinyanga
WACHIMBAJI wadogo wa madini mkoani Shinyanga wametakiwa kuacha kutumia dhana potofu badala yake watumie sampuli rahisi ya kitaalamu ya kubaini madini yalipo ili kuepusha uchimbaji holela na uharibifu wa mazingira.

Hayo yameelezwa leo na mratibu wa mafunzo kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), John Kalimenze kwenye mafunzo ya wachimbaji wadogo wa mkoa wa Shinyanga, ambapo aliwataka waache kutegemea dhana potofu badala yake wategemee utafiti wa maabara ambao utawaongezea uchumi.

Mratibu wa mafunzo hayo, John Kalimenze kutoka GST alisema lengo la kufanya mafunzo hayo ni kuwasaidia wachimbaji wadogo waweze kutambua aina mbalimbali za miamba inayobeba madini na kujua njia za utafiti wa madini kwa urahisi kuliko kutumia nguvu.

"Tuacheni kutumia dhana potofu ndugu zangu, kwani madini hayana uchawi yanatakiwa utaalamu fanyeni kazi zenu kwa utafiti mtafanikiwa zaidi na kipato chenu kitaongezeka bila kutumia nguvu kama mnavyofanya sasa",alisema Kalimenze.

Alisema lengo la (GST) ni kumkwamua mchimbaji mdogo aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi na kwa tija kwa kutumia utafiti wa madini bila kutumia nguvu na kupoteza Muda, pia wasipoteze fedha nyingi.

Mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Ishinabulandi wilayani Shinyanga Kashi Salula alisema anaipongeza taasisi ya (GST) kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kufanya uchimbaji wa kitaalamu kwa kutumia sampuli na marudio.

"Tunashukuru sana kwa kutukumbuka (GST) tukitumia sampuli itatusaidia kutunza mazingira kwa sababu tutakuwa na kipimo cha kueleweka, Ila tunaiomba serikali kupitia taasidi hii itusaidie kutupatia mashine za kisasa za kuchimbia dhahabu kwani tunatumia nguvu kubwa sana",alisema Salula.

Mgeni rasmi wa mafunzo hayo, Gwalugano Mwakanyamala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack alisema GST kwa kushirikiana na tume ya madini imekuwa ikijitahidi kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu na mpaka sasa kuna vikundi 23 vimepatiwa leseni za kuchimba madini.

Mwakanyamala alisema hadi kufikia Aprili30 2021 kiasi cha Gm. 685,132.23 za dhahabu zenye thamani ya Sh 82,279, 734,969.14.ambazo zilizalishwa na kulipa mrahaba na ada ya ukaguzi Sh 5, 759,581, 447.64 na kiasi cha karati 14,354.58za madini ya almasi yenye thamani ya Sh 3, 417,456,306.24.

Alisema changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo ni kuhusu namna bora ya uchukuaji wa sampuli kwa ajili ya uchunguzi na uchenjuaji wa madini ambao ndio nguzo kuu ya utafutaji na uchimbaji wa madini wenye tija.

Kwa upande wake Afisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Joseph Kumbulu alisema tume ya madini kwa kushirikiana na GST wameanza kutoa mafunzo namna ya usomaji wa sampuli ili kuondokana na udanganyifu wa marudio ya udongo, kwani wakitumia sampuli na kupeleka maabala, kutakuwa hakuna udanganyifu wowote.
Mchimbaji mdogo wa madini ya Dhahabu mkoani Shinyanga, Kashi Salula akieleza namna ambavyo mafunzo hayo yatakavyokuwa msaada katika shughuli zao, kwani awali walikuwa wanatumia nguvu kubwa na fedha nyingi katika uchimbaji huo
Mratibu wa mafunzo hayo, John Kalimenze kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) akizungumza na wachimbaji wadogo
Viongozi wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wachimbaji wadogo waliohudhuria mafunzo hayo
Post a Comment

0 Comments