Header Ads Widget

SPC YAADHIMISHA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI, DC MACHA AWAHIMIZA KUWAONDOA 'WAHUNI' WANAOHARIBU FANI

Mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Anamringi Macha (katikati waliokaa msitari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waandishi wa habari mkoani humo wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari, iliyofanyika leo kwenye ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga

Na Damian Masyenene, KAHAMA
masyenenedamian@gmail.com

KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) leo imeungana na wanahabari kote ulimwengu kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari (Media Day) ambayo hufanyika kila mwaka Mei 3, ambapo mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya 'Habari kwa manufaa ya umma'.

SPC imeadhimisha siku hiyo katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kwa kuwakutanisha wanachama wa klabu hiyo, waandishi wa habari mkoani hapa pamoja na wadau mbalimbali wa habari na kubadilishana mawazo pamoja na mijadala na kupata chakula cha pamoja.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau na wawakilishi wa taasisi na mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali, viongozi wa dini na kisiasa pamoja na Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba.

Akifungua maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha ameipongeza SPC kwa hafla hiyo na waandishi wa habari kwa ujumla kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kuuhabarisha umma na kuchochea maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, Macha ameziasa taasisi, wadau na watendaji wa Serikali kutumia vyema vyombo vya habari katika kutoa taarifa kwa umma na wananchi ili kutoacha mwanya wa watu kujitungia majibu na taarifa za upotoshaji.

Mbali na kuwapongeza waandishi wa habari kwa kazi kubwa wanayoifanya, amewahimiza kuhakikisha kuwa wanawaondoa baadhi yao wasiozingatia miiko na maadili ya taaluma hiyo, kwa kuzusha taarifa za uongo na kuleta taharuki kwenye jamii.

"Mnafanya kazi nzuri lakini kuna wakati baadhi wanakengeuka wanatoa taarifa zisizo sahihi ambazo hazina ufafanuzi kutoka pande tajwa. Ndani mwenu wapo vishoka ambao wanasababisha taarifa kuvumishwa na zisizo sahihi, kwahiyo ni vyema hilo likadhibitiwa tuwe na watu makini ambao ni sahihi.

"Vyombo vya habari visiwe tu vya kutoa taarifa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, ama taasisi moja kwenda nyingine, wafanye shughuli za uchunguzi na waongeze uelewa. Isiwe kwamba tu ni kazi ambayo inakimbiliwa na walioshindwa maisha.

"Ili kuleta maana ya waandishi wa habari kwa manufaa ya umma ni vyema sasa tukaacha kujikita tu kwenye kuripoti kilichojiri, bali tuwatafute wataalam wa uchumi na fursa waeleze uchumi na fursa za maeneo yetu, kwani waandishi wa Habari ni kipaza sauti cha wananchi," amesisitiza.

Vilevile, amewaomba waandishi wa habari kufanya uandishi unaojenga na wenye staha kwa kutoa taarifa na kukosoa kwa lugha ya staha na kwa namna ambayo hailengi kumdhalilisha ama kumuangusha mtu, bali kwa namna ambayo itamjenga na kumrekebisha mtu.

“Tasnia yenu imeingiliwa, na sasa hivi inataka kufanya isiaminiwe. Na watu wa kuilinda ni nyie, na sisi serikali tuko Pamoja nanyi kuhakikisha tunakomesha hili.

“Ndugu zangu waandishi wa habari siku hii ya leo, pamoja na uhuru ulioahidiwa na serikali, tunawaomba mtusaidie vishoka waliopo kwenye tasnia ya habari, ambao wanapotosha, kuzusha na kutoa taarifa zisizo sahihi,” amesema.

Akiwasilisha taarifa ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga, Mwenyekiti wa SPC, Greyson Kakuru amesema kuwa klabu hiyo inao wanachama 46 kati ya waandishi 126 wanaofanya shughuli zao katika mkoa huo, huku akiwaomba wadau kuendelea kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari ili kuweza kufikisha taarifa muhimu kwa umma kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Kakuru ameahidi kulifanyia kazi ombi la DC Macha na wadau wengine la kuwadhibiti baadhi ya waandishi wasiofuata misingi ya taaluma hiyo, ambapo amewasihi wadau kuwa na uwiano wenye tija katika uchaguzi wa mahitaji ya vyombo vya habari ili kuwapa fursa wananchi kupata taarifa sahihi na muhimu.

"Tunayo furaha kubwa kuona namna mnavyothamini mchango wetu, SPC ni kichwa cha mkoa wa shinyanga, kwani ni macho na masikio ya wananchi wa mkoa huo, na wadau ni shingo inayobeba kichwa hicho, hivyo ushirikiano mkubwa unahitajika katika kuuletea na kuzitangaza fursa mkoa wetu," ameeleza.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amewashukuru waandishi wa Habari kwa mchango mkubwa katika kutoa taarifa na kukomesha uhalifu wa aina mbalimbali mkoani humo, huku akiwasihi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo na kufichua vitendo vya kihalifu

“Vyombo vya habari vimetoa msaada mkubwa kwa jeshi letu kwa kutoa vipindi bure vya kuelimisha jamii, kutoa taarifa na kushiriki kampeni mbalimbali za kutokomeza ukatili na unyanyasi pamoja na kuzuia uhalifu,” amebainisha.

Wakichangia mawazo kwenye mjadala uliohusu mada mbalimbali ikiwemo ‘thamani sawa ya vyombo vya habari kwa umma’ na ‘nguvu ya vyombo vya Habari katika shughuli za wadau na umma’, baadhi ya waandishi wa habari akiwemo Kareny Masasi, Sam Bahari na Moshi Ndugulile wamewaomba wadau kutobagua vyombo vya habari katika kutoa taarifa zao, wadau kutowakimbia waandishi wa habari pale wanapohitajika kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali, huku wakiwataka waandishi vijana wanaochipukia kuacha mihemko na badala yake wazingatie maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kulisaidia taifa.

Nao baadhi ya wadau akiwemo Mkuu wa Kanisa la KKKT Jimbo la Kahama, Mchungaji Dk. Daniel Mono, Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga, Anderson Lyimo wakitoa maoni yao juu ya mijadala hiyo na kutoa ushauri mbalimbali kwa waandishi wa habari, wamewa kupendana na kufanya kazi kwa ushirikiano, kuondoa makundi, kutoa habari kwa haki, kuwa wazalendo, kuacha kutoa vitisho na kujipatia fedha kwa nguvu (isivyo halali).

“Vyombo vya Habari vitoe fursa pana kwa taasisi za dini visisubirie tu sikukuu za pasaka na krismasi. Pia visitoe tu fursa kwenye siasa,” amesema Mchungaji Mono.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho hayo
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru akizungumza kwenye maadhimisho hayo
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akieleza mchango wa waandishi wa habari mkoani humo katika kutokomeza vitendo vya kihalifu
Makamu Mwenyekiti wa SPC, Patrick Mabula akitoa neno la shukrani katika maadhimisho hayo
Katibu Mtendaji wa SPC, Ali Lityawi akizungumza kwenye maadhimisho hayo
Mratibu wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC), Estomine Henry akieleza mambo mbalimbali kuhusu klabu hiyo
Viongozi wa meza kuu wakifuatilia majadiliano katika maadhimisho hayo
Waandishi wakifuatilia mijadala kwenye maadhimisho hayo
Waandishi wakiendelea kufurahis maadhimisho hayo
Mwandishi na Mkurugenzi wa Malunde1 Blog, Kadama Malunde akichangia mada kwenye maadhimisho hayo
Mtangazaji wa kituo cha Faraja FM cha mjini Shinyanga, Josephine Charles akichangia maoni kwenye moja ya mijadala katika maadhimisho hayo
Mwandishi wa habari mkongwe mkoani Shinyanga, Sam Bahari akitoa ushuhuda wa mambo mbalimbali kuhusu tasnia ya habari na kutoa ushauri kwa waandishi wa habari chipukizi
Mwandishi wa habari Mwandamizi na Mhariri wa habari kituo cha Faraja FM, Moshi Ndugulile akieleza mchango wa vyombo vya habari katika shughuli za wadau
Waandishi wa habari, Suzy Butondo na Marco Maduhu wakifuatilia kwa ukaribu mijadala katika maadhimisho hayo
Maadhimisho yakiendelea
Waandishi wa habari wakiendelea kufuatilia mijadala mbalimbali
Shughuli zikiendelea
Waandishi wakiendelea kufuatilia mjadala
Waandishi wa habari na wadau wakiendelea kubadilishana mawazo na kutoa maoni juu ya thamani ya vyombo vya habari
Baadhi ya viongozi wa baraza na umoja wa wazee wakiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo
Baadhi ya viongozi wa dini nao walikuwa sehemu ya maadhimisho hayo
Mwakilishi wa Meneja wa TRA Kahama, January Gabriel akizungumza katika maadhimisho hayo
Afisa Habari wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Helga Mfuruki akizungumza kwa niaba ya taasisi hiyo
Mkuu wa Takukuru Kahama,  Abdullah Urari akieleza mchango na nguvu ya vyombo vya habari wilayani humo
Mjumbe wa baraza la mashekhe wilaya ya Kahama, Muhsin Juma akieleza mchango wa vyombo vya habari kwa dini ya kiislam
Mkuu wa Kanisa la KKKT Jimbo la Kahama, Mchungaji Dk. Daniel Mono akieleza mchango wa vyombo vya habari kwa kanisa hilo
Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga, Anderson Lyimo akieleza namna vyombo vya habari vilivyosaidia na kupaza sauti kuhusu haki za wazee na kukomesha mauaji ya vikongwe
Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee wilayani Kahama, Paul Ntelya akitoa maoni kwenye maadhimisho hayo
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Yahya Bundala akishiriki kwenye maadhimisho hayo
Afisa Mikopo wa benki ya NMB, Victor Mungereza akizungumza kwa niaba ya benki hiyo
Meneja Biashara na Mikopo wa benki ya CRDB, Dorcas Ngoye akieleza mchango wa vyombo vya habari
Mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Julius Lugobi akichangia mjadala kwenye maadhimisho hayo
    Mwakilishi wa Meneja wa Tanroads Shinyanga, Herieth Montesa akieleza namna wanavyoshirikisha vyombo vya habari katika utekelezaji wa shughuli zao
Mhandisi wa maji kutoka RUWASA, David Alloys nae akichangia hoja kwenye maadhimisho hayo
Diwani wa Kata ya Kahama Mjini, Hamidu Kapama akitoa ushauri kwa waandishi wa habari
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Kahama (KUWASA), John Mkama akieleza namna vyombo vya habari ni muhimu katika shughuli zao
Wadau mbalimbali wakifuatilia maadhimisho hayo
Mjumbe wa kamati tendaji ya SPC, Suzy Butondo akichangia hoja katika mjadala kwenye maadhimisho hayo
DC Macha akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi, viongozi wa dini na siasa waliohudhuria maadhimisho hayo
DC Macha akiwa katika picha ya pamoja na waandishi kwenye maadhimisho hayo



Post a Comment

0 Comments