Header Ads Widget

SHINYANGA YAPIGA ’STOP’ MALIPO YA MKONONI KWA WAKULIMA WA PAMBA, RC SENGATI AWATAHADHARISHA VIONGOZI AMCOS

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati akizungumza na wadau mbalimbali wa zao la Pamba mkoani humo leo kwenye kikao cha wadau wa zao hilo ambacho kimehitimishwa kwa kuafikia maazimio mbalimbali yanayolenga kuleta ufanisi kwenye ununuzi wa Pamba

Na Damian Masyenene, SHINYANGA
WADAU wa Pamba mkoa wa Shinyanga wamefikia maazimio manne muhimu ambayo yataanza kutekelezwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 yatakayosaidia kuinua uzalishaji na ufanisi katika zao hilo na kuleta manufaa kwa wakulima, moja ya maazimio hayo ni malipo yote ya wakulima wa zao hilo yafanyike kwa njia ya benki ama simu za mkononi na siyo kwa fedha taslimu mkononi (Cash) kama inavyofanyika sasa hali ambayo inachochea dhuluma na mwanya wa wizi kwenye malipo ya wakulima.

Maazimio mengine ni kwa vyama vikuu vya ushirika SHIRECU kuanzisha na kusimamia mfumo wa usajili wa wakulima na utunzaji wa kumbukumbu, Vyama vya msingi vya wakulima (AMCOS) kuweka akiba ya fedha asilimia 60 ya ushuru wanaopokea kwa ajili ya shughuli za maendeleo na asilimia 40 matumizi ya kawaida, Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) kufikia Mei 29, mwaka huu (Keshokutwa) kupeleka mizani kwenye maeneo yote inayoyasimamia kwani kwa sasa wamesambaza mizani 90 pekee katika wilaya za Kishapu na Shinyanga.

Hayo yamefikiwa leo Mei 27, 2021 katika kikao cha wadau wa zao la Pamba mkoani humo kilichojadili mwenendo wa ununuzi wa zao hilo, ambapo wadau hao wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati wameazimia hayo kwa pamoja kwa nia ya kuleta mchango chanya kwenye zao la Pamba.

Akikazia maazimio hayo, Dk. Sengati amesema kuwa yeyote atakayegundulika anakwamisha mipango hiyo hususan viongozi wa AMCOS atawajibishwa kwa kufutwa kazi na kutafutwa watu wenye weledi wanaoweza kusimamia majukumu hayo ambao wataweza kufanya kazi kwa ubunifu, uzalendo na kutoa suluhisho kwenye matatizo yanayozikumba AMCOS ili waweze kuacha alama ya kukumbukwa.

“Sitegemei kuona huko chini baadhi ya watu wanaanza kutengeneza mazingira ya kupata fedha taslimu, hili tukiligundua basi tutachukua hatua na tutawawajibisha. Vyama vikuu vya ushirika viendelee kuimarisha mifumo yao ya kuwasajili na kuwatambua wakulima wao, niwahidi na niendelee kuwahikikishia kuwa nitawapa ushirikiano, kusimamia haki, kuzingatia uzalendo.

“Hatutaki Amcos za kuomba na kulia kila siku. Tunahitaji tuone wanaweka akiba wanajiendesha kuliko sasa wanapata, wanatumia na kumaliza, hata fedha ya kupakia na kushindilia nayo hawana. Tunataka wabadilike na zilete matumaini kwa wakulima wa Pamba,” ameeleza.
Akichangia hoja hiyo ya malipo, Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi, Said Pamui amesema maeneo mengi wameshaondokana na mfumo wa malipo kwa wakulima kwa njia ya pesa taslimu na kushangazwa kwanini inashindikana kuingiza mfumo wa manunuzi rasmi ya pamba kutoka kwa wakulima wakati kwenye mazao mengine imewezekana.

“Huu unatumika kama mwanya wa kuwadhulumu wakulima na ndiyo maana unakuta bei ya pamba inatangazwa kupanda lakini wakulima wanalipwa kwa fedha ya zamani alafu ile faida inaenda kwa watu wa kati.

“Nakuomba Mkuu wa mkoa ufanye maamuzi, kwenye mkoa wetu tupitishe hili kwamba malipo yapite kwenye akaunti za benki…akaunti zipo, kusema kwamba wakulima hawana akaunti ni hoja mfu kwa sababu hadi jana jumla ya akaunti 31,000 zilikuwa zimeshafunguliwa kwenye ukanda wetu,” amesisitiza Pamui.

Vilevile, Pamui ameeleza kuwa taasisi za fedha hazijumuishwi kwenye muongozo kama wadau wa pamba, na hapo ndipo changamoto zinapoanzia kwani ili manunuzi yaende salama ni lazima taasisi za fedha zishirikishwe kwa sababu ndiyo wadau wakubwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha amesema kuwa mfumo huo wa malipo umepunguza malalamiko wilayani kwake, huku akikiri kuwa changamoto ni kwamba wakulima wanatumia akaunti hizo kupitishia fedha hizo lakini hawaziendelezi hivyo zinakuwa mfu.

“Watu wa mitandao ya simu wawe makini kuepusha utapeli kwa wakulima wetu,kuwe na usiri wa malipo ya wakulima na taarifa za wakulima zisiwafikie matapeli ili kutowaumiza wakulima wetu. Amcos zetu zimekuwa na matumizi yasiyo na akiba. Wao kila msimu ukiisha nao wameishiwa, hawana akiba yoyote, kwanini wasiwe na akaunti na wakawa na kianzio kwenye kila msimu mpya unapoanza,” ameshauri.

Awali akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa ununuzi wa pamba msimu ulioisha mwaka 2020, Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniphace amesema kuwa mkoa huo unavyo vyama 462 vya ushirika n ani 197 tu vinavyohusika nap amba, huku akibainisha kuwa Zaidi ya Kilo Milioni 14 za Pamba zilinunuliwa msimu uliopita, huku kukiwa na deni la malipo ya ushuru ya Sh Milioni 22.8 inayodai Shirecu (Sh. Milioni 6) na AMCOS (Sh. Milioni 16.8) kutoka kampuni ya KOM.

“Utaratibu wa malipo uliotumika sehemu kubwa ilikuwa malipo ya fedha taslimu hasa wilaya ya Kishapu na shinyanga, lakini Kahama malipo yalifanyika kupitia akaunti na makampuni ya simu. Changamoto malipo ya fedha taslimu ni kwamba wakulima wanapunjwa fedha zao, yametumika kama ulaghai kwa baadhi ya watumishi wa makampuni na wahasibu wa amcos, yamepelekea ugumu kwenye ufuatiliaji wa fedha za amcos, yameleta ugumu katika kufanya shughuli za ukaguzi (utunzaji kumbukumbu ni mgumu) na yameleta migogoro kwa wakulima kubaini malipo halali baina yao,” ameeleza.

Kaimu Mrajisi huyo ameeleza kuwa jumla ya Mizani 198 imekusanywa, mizani 20 ni mibovu imeshindwa kutengenezeka na hali ya mizani hiyo ni mbovu imetumika kwa muda mrefu sana, mingine ikiwa na zaidi ya miak 10 kwahiyo hata ubora wake umepungua hivyo kuna haja ya kuwapatia wakulima wetu mizani mipya.

Akitoa Muongozo wa ununuzi wa Pamba kwa msimu wa mwaka 2021/2022, Kaimu Meneja wa Bodi ya Pamba (TCB) Kanda ya Mwanza, Mhandisi Kisinza Ndimu ameeleza kuwa muongozo unaelekeza kuwa malipo ya fedha taslimu yatafanyika pale ambapo hakuna miundombinu ya kulipa kupitia benki ama simu, hivyo njia hizo ni uchaguzi wa mwisho kabisa.

Wakichangia mawazo kwenye kikao hicho na kueleza changamoto, mafanikio na mapendekezo, wadau mbalimbali akiwemo Katibu wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake na wenye Viwanda Mkoa wa Shinyanga, Maselina Saulo amedai kuwa malipo ya fedha taslimu mkononi yalisababisha baadhi ya ndoa kuvunjika kutokana na baadhi ya wanaume wakishapokea malipo hayo hawarudi nyumbani hadi pale fedha zitakapomuishia mkononi.

Meneja wa Tigo Mkoa wa Shinyanga, Sadock Phares amebainisha kuwa baadhi ya maeneo wamekuwa wakikwama kuwasajilia line za simu wakulima kutokana na kukosa namba za NIDA, hivyo akapendekeza kuwa maeneo yenye vyama na wakaulima wa pamba yapewe namba za NIDA ili waweze kusajili namba na kuwa simu kwa ajili ya malipo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba ameshauri AMCOS zijengewe uwezo mkubwa kwasababu baadhi ya viongozi hugeuka kuwa mawakala wa wafanyabiashara kwa kukusanya mazao na kulipa wakulima.

Naye Mkaguzi kutoka Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika, Justine Maro amesema kuwa kwenye kaguzi zao wamebaini kwamba kuna mvutano baina ya viongozi na wawakilishi wa wakulima namna gani bora ya kuwalipa wakulima, ikifika hii hatua kila mmoja anapendekeza njia yake bila kumfikiria mkulima.

“Sisi kama wakaguzi tunapendekeza njia ya benki kwa sababu ni salama na ya uhakika nani rahisi kupata kumbukumbu za malipo. Makatibu wa vyama vya ushirika kila inapopendekezwa njia ya malipo na wakatakiwa kwenda kutoa elimu kwa wakulima wao wanaenda kutoa elimu kinyume na maazimio ya wadau. Wanapenda njia ya fedha taslimu ili wanufaike na chenji ndogo ndogo,” amesema.

“Utunzaji na uandishi wa kumbukumbu katika vyama vya pamba ni mdogo, zinapohitajika ni vigumu sana kuzipata. Napendekeza wakurugenzi watoe fungu la kuvipa mafunzo ya uandishi bora wa kumbukumbu vyama vya ushirika kwa sababu halmashauri zinapata mapato kutoka kwenye vyama hivi, hii pia itasaidia kuondoa hati mbaya na chafu kwenye ukaguzi,” amesisitiza.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Kahama (KACU) ambacho kimepongezwa kwa kufanya vizuri, Emmanuel Charahani amesema kuwa kitu kinachotesa vyama hivyo ni takwimu za wakulima, ambapo amependekeza viondoke kwenye mifumo ya kizamani na kwenda kwenye mfumo wa kisasa wa usajili ili kurahisisha utendaji kazi.

“Ukienda kwenye baadhi ya amcos hata hawajui orodha ya wakulima wao, takwimu hazijakaa sawa. Tutenge fungu la kuandaa taarifa za wakulima, tununue mfumo wa usajili wa wakulima na kumbukumbu zote. Hili litatusaidia kuondoa migongano na kuvutana,” amekazia.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba amesema kuwa changamoto nyingi zinazoelezwa ikiwemo ubovu wa mizani na uhaba wa shajala (vitabu vya kutunza kumbukumbu), vyama vya ushirika vinaweza kuzitatua na kujiendesha kwa weledi lakini hawafanyi hivyo kwa makusudi kwa sababu wananufaika na mianya hiyo.

“Likija suala la kulipa kwa akaunti za benki na mitandao ya simu vikao vinawaka moto, najiuliza kwanini isiwezekane? – Ni wazi kuwa wakulima wanaibiwa, kuna watu wanafaidika hapo kati. Nami nasema kwamba katika wilaya yangu hakuna malipo ya taslimu,”amesisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati akifungua kikao hicho
Dk. Sengati akizungumza na Wadau wa Pamba mkoani humo leo
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akichangia hoja na kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kuhusu ununuzi wa zao la Pamba wilayani kwake
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akieleza namna ambavyo wilaya yake imepiga hatua katika mfumo wa malipo kwa wakulima wa pamba kwa njia za kielektroniki na ugawaji wa mizani
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Emmanuel Charahani akizungumzia namna ambavyo takwimu zimekuwa changamoto kubwa kwa vyama vya ushirika
Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Nchini (WMA), Hilolimus Mahundi akitolea ufafanuzi wa suala la uchakavu wa mizani kwa vyama vya ushirika
Wadau wa Pamba wakichangia mawazo kwenye mjadala wa kuboresha utendaji kazi wa vyama vya msingi vya wakulima (AMCOS)
Wadau wakifuatilia kikao hicho
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson (mbele kulia) akifuatilia kwa karibu hoja mbalimbali kwenye kikao hicho
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha wakifuatilia kwa umakini kikao hicho
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba (katikati) na wadau wengine wakifuatilia kikao cha wadau wa pamba mkoani Shinyanga
Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi, Said Pamui (kulia mstari wa mbele) akifuatilia mawasilisho kwenye kikao hicho
Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea

Picha na Marco Maduhu


Post a Comment

0 Comments