Header Ads Widget

WATATU WADAKWA WIZI WA SIMU 5 MECHI YA MWADUI VS SIMBA, RPC AOMBA WALIOIBIWA KUJITOKEZA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Damian Masyenene, Shinyanga
VIJANA watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga kwa tuhuma za kuiba simu tano wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kati ya Mwadui FC dhidi ya Simba SC uliochezwa jana (Jumapili) uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Aprili 19, 2021 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, wizi huo ulifanyika jana saa 10 jioni wakati mchezo huo ukiendelea.

Kamanda Magiligimba amewataja wanaoshikiliwa kwa makosa ya wizi kuwa ni Amos Shija (38) na Gerald Abdallah (18) wakazi wa Majengo mjini Shinyanga na Rashid Hamis (25) mkazi wa Tabora .

Ameongeza kwa kuzitaja simu zilizoibwa kuwa ni Iphone 5 aina ya s7+ rangi nyeusi, Infinix hot 08, Sony Xperia, Itel ndogo na Tecno rangi ya Silver.

"Wakati askari wakiwa katika majukumu ya kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa wakati wa mechi ya ligi kuu kati ya Mwadui FC na Simba SC ikiendelea, waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa wameiba simu tano. Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika," amesema.

Hata hivyo, Kamanda Magiligimba amewaomba wananchi walioibiwa simu zao siku ya Aprili 18, 2021 ndani ya uwanja wa kambarage kufika kituo kikubwa cha polisi Shinyanga ili kubaini simu zao.


Post a Comment

0 Comments