Header Ads Widget

WACHIMBAJI WADOGO MAGANZO WAMLILIA HAYATI JPM, WAIKUMBUKA AHADI YA KUPATIWA ENEO

Wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Maganzo wilaya ya Kishapu wakiendelea na shughuli za uchimbaji huku wakiomboleza kifo cha aliyekuwa Hayati Dk. John Magfuli.

Na Shinyanga Press Club Blog
WACHIMBAJI Wadogo wa madini katika Kijiji cha Maganzo wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga wameungana na Watanzania wengine kuomboleza kifo cha Hayati Rais Dk. John Magufuli, huku wakikumbuka namna alivyowajali na aahidi ya kuwapatia eneo la kuchimba madini lililopo Kijiji cha Mwang’olo Kata ya Mwaduiluhumbo.

Wachimbaji hao wametoa hisia zao za majonzi na masikitiko, jana walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Maganzo, ambapo walisema kuwa hayati Magufuli aliwatetea na kuwapatia maeneo ya kuchimba lakini ameondoka kabla ya kukamilisha ahadi yake ya kuwapatia eneo lingine.

Mmoja wa wachimbaji hao, Ester Luhende mkazi wa Maganzo alisema awali walikuwa wanauza madini kiholela na kushindwa kunufaika nayo, lakini hayati Magufuli alisimamia na ofisi za kuuza madini kufunguliwa ambapo kwa sasa wananufaika na madini wanayouza.

Masanja Joseph mchimbaji mdogo wa madini alisema walikuwa wananyanyaswa na wawekezaji lakini baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani,alisimamia vizuri na kuwawezesha kufanya kazi zao kwa uhuru bila kufukuzwa pamoja kuuza madini sehemu salama.

“Hapa nilipo sijui hatima ya kazi yangu hii maana tumepata pigo kubwa sana ambalo hatutalisahau mtetezi wetu ameondoka,tunamuomba Rais aliyechukuwa kijiti asituache aendelee kututetea wanyonge na kuendeleza alipoishia Magufuli,” alisema Joseph.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Maganzo, Charles Manyenye alisema serikali ya awamu ya tano imefanya kazi kubwa ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa na kuboresha sekta yamadini kwa kuzuia utoroshwaji wa madini kwenda nje ya nchi pamoja na uuzaji holela.

Alisema hayati Magufuli ameondoka wakati bado taifa lilikuwa linamuhitaji na kuwaacha katika majonzi makubwa,ambapo wachimbaji wadogo ahadi ya kuwapatia eneo jingine la uchimbaji mtetezi wao kaenda kabla hajakamilisha malengo yake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majimaji eneo wanapochimba madini, Seba Ndekelo alisema Dk. Magufuli ameonyesha njia kwa viongozi wengine ambayo iwapo wataifuata itasaidia kufikia ndoto zake alizozitamani kuona watanzania wananufaika na rasilimali zao.

Hayati Rais Dk. John Magufuli alifariki Machi 17, Mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena, Jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na tatizo la moyo, ambapo anatarajiwa kuzikwa leo Machi 26, 2021 katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwa hayati Magufuli wilayani Chato.

PICHA

Wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Maganzo wilaya ya Kishapu wakiendelea na shughuli za uchimbaji.
Shughuli za uchimbaji madini zikiendelea katika kijiji cha Maganzo wilaya ya Kishapu.
Wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Maganzo wilaya ya Kishapu wakiendelea na shughuli za uchimbaji
Mmoja wa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Maganzo akiendelea na shughuli zake za utafutaji madini
Mwenyekiti wa Kijiji cha Maganzo, Charles Manyenye
Mwenyekiti wa kitongoji cha Majimaji eneo wanapochimba wachimbaji wadogo, Seba Ndekelo
Mmoja wa wachimbaji hao, Ester Luhende
Mchimbaji mdogo wa madini, Masanja Joseph akimzungumzia JPM alivyowasaidia kuacha kufukuzwa na kuchimba kwa uhuru
Mchimbaji mdogo wa madini,  Emmanuel Maige akieleza jinsi JPM alivyowasaidia

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini katika Kijiji cha Maganzo wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga wakiendelea na shughuli zao kama walivyokutwa na Mwandishi wetu jana, huku wakimzungumzia na kumkumbuka Hayati Dk. Magufuli namna alivyowasaidia.


Post a Comment

0 Comments