Header Ads Widget

KATAMBI AWAPA MAELEKEZO AL HILAL MINERALS NA KIWANDA CHA JEOLONG HOLDING MALIPO YA WAFANYAKAZI

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na Afisa Utawala wa kiwanda cha kuchakata mafuta ya kupikia cha Jielong Holding kilichopo Mkoani Shinyanga.

Na Suzy Luhende, Shinyanga
Wamiliki wa makampuni na waajiri wametakiwa kuzingatia sheria za kazi katika maeneo yao ya kazi ili waweze kuboresha mazingira ya utendaji kazi utakaoleta tija na ufanisi.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi alipokuwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Shinyanga alipotembelea Mgodi wa Almasi wa Al – Hilal Mineral Ltd uliopo wilayani Kishapu na Kiwanda cha Jielong Holding kilichopo Shinyanga Mjini kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi.

Naibu Waziri Katambi amesema kuwa ni wajibu wa waajiri kuhakikisha wanatekeleza sheria za kazi katika maeneo ya kazi akitolea mfano wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004 ambayo imekuwa ikisaidia kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyakazi na waajiri kuwa na mahusiano mazuri baina yao.

“Kwenye maeneo mengi ya kazi ambayo wamekuwa hawafuati na kutekeleza sheria za kazi migogoro hutokea mara kwa mara kati ya waajiri na wafanyakazi kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa sheria za kazi katika maeneo yao,” ameeleza Katambi

“Itambulike kuwa Wajibu wa Mfanyakazi ndio haki ya mwajiri na wajibu wa mwajiri ndio haki ya mfanyakazi,” amesema

Alifafanua kuwa katika kupunguza migogoro mahali pa kazi, serikali imekuwa ikifanya kaguzi na kusimamia uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi na jinsi tume ya usuluhishi na uamuzi imeendelea kutimiza wajibu wake wa kusuluhisha migogoro.

Amesema kuwa, ushirikiano mzuri wafanyakazi na waajiri ni jambo muhimu kwa kuwa kupitia vyama vya wafanyakazi wataweza kuwasilisha malalamiko, kero au changamoto zitakazo kuwa zinawakabili katika vyombo husika na kutatuliwa.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi ikiwemo sekta binafsi na sekta ya umma. Katika kutekeleza hayo haki imekuwa ikitolewa kwa usawa kwa waajiri na wafanyakazi kwenye maeneo yao ya kazi.

“Serikali haitasita kuwachukulia hatua waajiri ambao hawatekeleza sheria za kazi kwenye maeneo yao ya kazi kwa kuamua kujichukulia maamuzi ambayo yamekuwa yakiwakandamiza wafanyakazi,” amesema Katambi

Aidha, Naibu Waziri Katambi amewataka waajiri wote kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi mishahara kwa wakati ili kupunguza malalamiko ya ucheleweshwaji wa mishahara, Pamoja na hayo ametoa maagizo kwa maafisa kazi kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za katika maeneo mbalimbali ya kazi iwe sekta ya umma au binanfsi.

Pia amewasihi waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati na watambue kuwa huo ni wajibu wao na ni takwa la kisheria kufanya hivyo.

Sambamba na hayo Naibu Waziri Katambi ametoa maagizo kwa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ikiwemo Idara ya Kazi, Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Fidia kwa Wfanyakazi (WCF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kutoa elimu kwa umma hususan waajiri na wafanyakazi waliopo kwenye maeneo kazi ili watambue sheria za kazi, miongozo na taratibu itakayowawezesha kupata haki na ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Ameyasema hayo baada ya wafanyakazi kulalamika kuwa wanafanyishwa kazi kinyume na sheria wananyanyaswa hawalipwi mishahara kwa wakati, hawalipwi stahiki zao inavyotakiwa pindi wanapokuwa wanasafilisha mizigo kwenda mikoani.

Kwa Upande Wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko ameeleza kuwa ziara hiyo ya kikazi itasaidia kuhamasisha waajiri wengi hususan wa sekta binafsi kufuata sheria za kazi na kutekeleza wajibu wao ambao utachangia kupunguza malalamiko ya wafanyakazi.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda cha Jeolong, Ji Zhong Jun alisema maagizo yote yaliyotolewa na waziri watayazingatia na watakaa na kufanya utaratibu wa kuwapa stahili zao wote wanaodai, na utaratibu wa kuwalipa mishahara yao ambao hawajalipwa.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya El - Hilal Minerals, Hilal Hamad akiongea kwa njia ya simu ya mkononi na Naibu Waziri Katambi alisema kampuni yake ilishasitisha uzalishaji tangu mwaka 2019 lakini kwa sasa ana wafanyakazi 40 ambao aliahidi kuwalipa wafanyakazi 21 ambao hawajalipwa mshahara ndani ya siku 30 ili waachishwe kazi kisheria.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wenye kofia nyeusi) akikagua mikataba ya Madereva ambao waliwasilisha malalamiko yao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi Mkoani Shinyanga.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (mwenye jaketi jeusi) akijadiliana jambo na Viongozi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na Wafanyakazi wa Kiwanda cha Jielong Holding wakati wa ziara yake ya kikazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Kishapu na Wafanyakazi wa Mgodi wa almasi wa Al – Hilal Mineral Ltd alipowasili katika mgodi huo kwa ajili ya kutatua kero za wafanyakazi dhidi ya mwajiri wao na kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi Mkoani Shinyanga.
Mfanyakazi wa Mgodi wa almasi wa Al – Hilal Mineral Ltd, Bi. Joyce Kuya (kulia) akimweleza jambo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa ziara ya kikazialiyoifanya Mkoani Shinyanga.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela (aliyesimama) akitoa taarifa fupi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani huo kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili mkoani Shinyanga kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wenye kofia nyeusi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Mgodi wa almasi wa Al – Hilal Mineral Ltd alipowasili katika mgodi huo kwa ajili ya kutatua kero za wafanyakazi dhidi ya mwajiri wao na kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi Mkoani Shinyanga.


Post a Comment

0 Comments