Header Ads Widget

MWILI WA PROFESA WARUDISHWA MOCHWARI BAADA YA KUFANYIWA IBADA YA MAZISHI... MKE, FAMILIA WATOFAUTIANA


WAOMBOLEZAJI wamepatwa na mshangao kutokana na mwili wa Profesa Japhet Gilyoma kurudishwa mochwari baada ya kumalizika kwa ibada ya kumuaga katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Victoria Nyanza. 

Wakati ilitarajiwa baada ya kuaga juzi jijini Mwanza, waombolezaji wangekwenda moja kwa moja kwenye shughuli ya maziko, mambo yalikuwa tofauti kutokana na kuibuka mgogoro baina ya mke wa marehemu, Alice Kambona na ndugu juu ya eneo la kwenda kumzika.

Profesa Gilyoma alikuwa mwajiriwa wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) katika kitengo cha pua, masikio na koo (ENT).

Mashuhuda waliliambia gazeti hili kwamba, baada ya kukamilika kwa ibada iliyoendeshwa na Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Kefa Bulugu, mke wa marehemu alichukua kipaza sauti na kutangaza kuwa mwili wa mumewe marehemu mmewe unatakiwa uzikwe katika makaburi ya kanisa Anglikana yaliyoko Kapripoint. 

Mjane huyo ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu kimoja jijini Mwanza, alisema mumewe alimwachia wosia unaoonesha mahali alikotaka azikwe. 

“Ni kweli mimi nimeendesha ibada hiyo hapa kanisani, lakini mambo mengine kuhusiana na mwili huo kaiulize familia,” alisema Mchungaji Bulugu aliliambia HabariLeo. 

Mwandishi wa gazeti hili lilimtafuta mke huyo wa marehemu, Alice kwa ajili ya kupata undani wa taarifa hizo lakini hakuwa tayari kuzungumzia zaidi ya kumwambia kwamba aache kufuatilia suala hilo, vinginevyo atamshitaki.

Kwa upande wake, Msemaji wa familia ya marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Ester Gilyoma, alisema ndugu yao alikuwa na haki ya kupata matibabu lakini kwa zaidi ya wiki mbili, simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.

Alisema baada ya familia kuamua kwenda kumtafuta nyumbani kwake NyegeziLuchelele, walimkuta Profesa Gilyoma akiwa amedhoofika kiafya na mke hakuruhusu wampeleke hospitali. 

Alisema baadaye hali yake ilipokuwa mbaya, alimpeleka hospitali ambako Machi 8 mwaka huu asubuhi alikumbwa na mauti kabla ya kupatiwa matibabu. 

Ester alisema kikao cha familia kilikaa na uongozi wa Hospitali ya Bugando Machi 9 mwaka huu na kuamua kuwa marehemu atazikwa Kisesa.

Kwa mujibu wa Ester, uongozi wa BMC ulikuwa tayari umejenga kaburi na kugharimia gharama zote kwa ajili ya maziko. Kikao cha familia kilifanyika kikaamua kwanza mwili wa marehemu ufanyiwe uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.

“Na hili suala tunatarajia kulipeleka kwenye vyombo vya kisheria vituthibitishie kuwa mkewe anadai aliachiwa wosia na marehemu unaoonesha amzike kwenye makaburi ya Kapripointi ambayo siyo ardhi yetu ni ya watu wote,” alifafanua

“Tunaomba ndugu jamaa na marafiki wa marehemu mpendwa wetu Profesa Gilyoma wawe watulivu, taarifa rasmi ya mazishi itatolewa baada ya taratibu za kisheria kukamilika,” alisema. 

Kwa mujibu wa Ester, wamefungua kesi polisi juu tukio hilo la kugombea mwili. 

Jana hadi saa 1 usiku, familia iliendelea na kikao. Kwa upande wa uongozi wa hospitali ya Rufaa ya Bugando, ambayo ni mwajiri, ulipotafutwa haukupatikana.

Post a Comment

0 Comments