Header Ads Widget

MFUMO DUME NDANI YA FAMILIA WAWATESA WANAWAKE TINDE

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba.
Afisa elimu Kata ya Tinde Vumilia Mauna
 **
Na Stella Herman Shinyanga Press Club Blog

Uelewa mdogo juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia umesababisha  baadhi ya wanawake kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kunyanganywa mali na kutelekezwa na watoto katika Kata ya Tinde  halmashauri ya Shinyanga na kushindwa kuripoti matukio hayo .

Hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na Klabu ya waandishi wa habari Kata ya Tinde kupitia mradi wake wa nafasi ya vyombo vya habari katika kumaliza ukatili kwa wanawake  na watoto unaofadhiliwa na mfuko wa wanawake Tanzania (WFT)ili kubaini changamoto zilizopo na kuchukuwa hatua ya kumaliza tatizo hilo.

Afisa maendeleo ya jamii Kata ya Tinde Eva Mlowe amesema wanawake wengi wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili ndani ya familia zao,lakini wamekuwa waoga na kushindwa kutoa taarifa kutokana na mfumo dume kwa kuogopa kuvunja ndoa zao ama kutengwa kwenye ukoo.

“Ukatili mkubwa unaofanyika hapa Kata ya Tinde ni wanawake kunyanyaswa na waume zao,utakuta mwanaume mwingine anaowa mwanamke halafu anampeleka kwenda kuishi naye ndani ya nyumba anayoishi na mke wake wa ndoa na  wakati mwingine anauza mali za familia yakiwemo mazao bila kumshirikisha mke wake na hela anakwenda kunywea pombe”,alisema.

Ukatili mwingine ni vipigo na baadhi ya wanaume kuuza mazao waliyolima na wake zao na kwenda kuyahifadhi lakini baada ya muda kupita wamekuwa wakiwadanganya kuwa wameibiwa,kitendo ambacho kimekuwa kikichochea vitendo vya ukatili ndani ya familia.

Katika mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto,baadhi ya wakazi wa Kata hiyo akiwemo Hashimu Mkalambati amesema hatua inayopaswa kuchukuliwa  kukomesha matukio hayo ni jamii kuendelea kupatiwa elimu pamoja na madawati ya jinsia yashuke hadi nganzi ya Kata kusogeza huduma karibu.

Pili Abdallah mkazi wa Tinde mama wa watoto wawili amesema alifanyiwa ukatili na mume wake baada ya kufukuzwa na kunyanganywa mali zote walizotafuta pamoja kisha mwanaume akaowa mwanamke mwingine na kumtelekeza na watoto lakini hakujua kama huo ni ukatili aliofanyiwa kutokana na kutokuwa na uelewa.

Katika utafiti uliofanywa na timu ya waandishi wa habari Kata ya Tinde umebaini kuna ukatili mkubwa wanaofanyiwa wanawake lakini kutokana na kukosa uelewa wa matukio wanayofanyiwa wamekuwa wakiona na kawaida kufanyiwa vitendo hivyo ambapo elimu bado inahitaji kuendelea kutolewa ili kuwawezesha kupata uelewa zaidi.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Shinyanga Hoja Mahiba amesema kutokana na kushamili matukio ya ukatili wa kijinsia,wameamuwa kutumia jeshi la jadi (Sungusungu)kuwadhibiti watu wanaofanya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

Amesema pia viongozi wa ngazi za vijiji wamewataka kuweka sheria ndogo ambazo zitatumika kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kama wanavyofanya katika matukio mengine.

Afisa elimu msingi Kata ya Tinde Vumilia Mauna amesema kwa sasa ukatili mashuleni umepungua kutokana na elimu iliyotolewa ikiwa ni pamoja na walimu kuepuka kutoa adhabu kali  ambazo zinaweza kuwa chanzo cha ukatili kwa watoto.

Amesema kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wazazi kuwasomesha watoto wa kike tofauti na miaka ya nyuma ambapo watoto wengi walikuwa wakibaki nyumbani wanachunga mifugo na wasichana kwenda kuolewa.
Afisa maendeleo ya jamii Kata ya Tinde Eva Mlowe
Wanafunzi wa shule ya msingi Tinde B ambayo iko kwenye mpango mkakati wa serikali wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA)
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba
Wanafunzi wa shule ya msingi Tinde B halmashauri ya Shinyanga
Hashimu Mkalambati mkazi wa Kata ya Tinde

Post a Comment

0 Comments