Header Ads Widget

‘KUPIMA WATOTO DNA KUNA MADHARA MAKUBWA’

Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk Joyce Nyoni

WANASAIKOLOJIA na wataalamu wa masuala ya ustawi wa Jamii wanashauri jamii kuwa masuala ya kupima kina saba (DNA) ili kujua uhalali wa mtoto au watoto lisiwe jambo la kukimbilia kwa sababu lina madhara makubwa kuliko faida na iwapo italazimu kufanya, wahusika wawe tayari kupokea na kubeba matokeo ya vipimo.

Akizungumza na HabariLEO, Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk Joyce Nyoni alisema katika familia masuala ya kufanya DNA kwa watoto yanapaswa kutazamwa kwa jicho pana zaidi kwa sababu madhara yake ni makubwa kuliko faida.

“Watoto ni kiunganishi cha familia,watoto au mtoto baba anajenga bondi na watoto, amewapa jina lake na mengine mengi ya kuimarisha uhusiano baina yao, sasa ghafla unafanya DNA unajua mtoto sio wako, baadhi ya wanaume wanaweza kuhimili na kuendelea kuishi naoi la wengine hawawezi kuvumilia, hapo ndio mwanzo wa kuparaganyika,”alisema Dk Nyoni.

Alieleza kuwa jambo hilo la kupima na kubaini mtoto au watoto sio wa baba husika linavunja uhusiano baina ya familia na watoto wakishajua huyo sio  baba yao huwanyima rah ana kuanza msongo wa mawazo huku baba aliyebaini akiondoka na maumivu makali.

“Ushauri wangu ni kwamba suala la kupima DNA libaki kwenye masuala ya uhalifu na mambo ya mirathi ila kama baba anataka tu kuwapima watoto kutaka kujua uhalali wao, sishauri hilo, kwa sababu madhara ni makubwa, tubaki na utaratibu wetu za zamani kitanda hakizai haramu,”alisema Dk Nyoni.

Alitoa mfano na kusema zipo familia ambazo mke na mume wameoana na wamekaa kwenye ndoa miaka mingi bila kupata watoto na ikatokea mwanamke akachepuka na kupata ujauzito bila mumewe kujua akalea mimba hadi mtoto akazaliwa na wengine wakaendelea kuzaliwa kwa njia hiyo huku mwanaume akiwalea na ikabainika kuwa mwanaume hakuwa na uwezo wa kuzalisha, lakini yote hayo yakabaki siri ya familia.

“Ndio maana nasema hili jambo liangaliwe kwa jicho pana iwe uamuzi wa mwisho kabisa kuchukuliwa, hivi mtoto umeshampa jina lako na umetengeneza bondi na watoto, ghafla unapima unakuta watoto sio wako, utawanyangánya jina lako? Hapo watoto ni wakubwa wanajua unafikiri wanaishi kwa amani hapo au wataondoka, mkeo naye ataendelea kuwa na wewe au mausiano ndio yanavunjika,”alisema Dk Nyoni.

Alisema njia bora ni kubaki kwneye ile Imani na kanuni ya zamani kuwa kitanda hakizai haramu ili kuondoa mkanganyiko huo vinginevyo iwapo baba ameakua kupima akubaliane na matokeo ya vipimo bila kuleta madhara kwa familia.

Alisema suala la kupima DNA libaki kwenye masuala ya mirathi na makosa ya kiuhalifu na jamii isipende kukimbilia jambo hilo kwa sababu pamoja na kuujua ukweli, halina afya katika familia.

Mwanasaikolojia, John Shayo alisema wanaume wanakwenda kupima DNA kwa sababu ya ubinafsi na wivu vitu na kwamba mambo hayo husababisha migogoro kwenye jamii.

Shayo alisema, ubinafsi unasababisha mwanaume aamue kupima DNA ili kujiridhisha kama mtoto au watoto ni wa kwake na kwamba wivu unachangia kwa sababu mwanaume anakuwa hajiamini kama mtoto aliyenaye ni wa kwake.

Alisema msukumo kutoka kwa ndugu au marafiki pia huchangie mwanaume atake kupima DNA ya mtoto au watoto kwa kuambiwa kuwa huenda ‘anaibiwa’ na akipima na kukuta kweli si watoto wake mambo mabaya huibuka kwenye familia.


Post a Comment

0 Comments