Header Ads Widget

WANAWAKE VIONGOZI WATAKIWA KUWABEBA WENZAO KUWANUSURU NA UDHALILISHAJI

Mkurugenzi wa TAMWA-Z’bar, Dkt. Mzuri Issa Ally akifungua mafunzo ya siku nane kwa baadhi ya waandishi wa Habari Zanzibar yenye lengo la kuwaeleza wanahabari umuhimu wa kuwaunga mkono wanawake kushika nafasi za uongozi.

Na Muhammed Khamis,TAMWA-Z’bar
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema ili wanawake wengi Zanzibar waweze kufikia malengo yao yakiwemo ya kuwa viongozi wanawake wenye nafasi hawana budi kuwavuta wengine.

Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku nane kwa waandishi wa habari visiwani hapa yaliotolewa na TAMWA-Zanzibar, ZAFELA pamoja na PEGAO chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway Tanzania katika ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe mjini hapa.

Amesema ni wakati sasa umefika kwa wanawake wanaoshika nafasi mbali mbali za kisiasa na kijamii kuhakikisha wanaweka mkakati maalumu wa kuwavuta wanawake wenzao kwa kuwa walio wengi bado wanahitaji msaada.

Sambamba na hayo amewataka wanawake kutokata tamaa na changamoto za udhalilishaji zinazowakabili kwa kuwa ili uwe kiongozi kwa mwanamke yapo mengi ambayo utayapitia.

‘’Mimi binafsi nimepitia changamoto ambazo ziwezi hata kuzisema hapa lakini leo hii nimeonekana uwezo wangu hatimae nimechaguliwa kuwa Waziri,’’ aliongezea.

Aidha Waziri huyo wa habari aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanayatumia vyema ikiwemo kuibua na kuandika changamoto za wanawake zitakazosaidia kuwajenga.

Awali Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa alisema mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yataleta mabadiliko na kuwa chachu kwa washiriki.

Alisema kwa kuwa waandishi wa habari ni watu muhimu kwenye jamii na wenye uwezo mkubwa wa kusikilizwa wameona ipo haja kuwapatia mafunzo katika mkakati maalumu ambao lengo ni kuwaibua wanawake wengi zaidi kwenye nafasi za maamuzi.

Hata hivyo alisema ipo haja kwa jamii kuzingatia haki na wajibu wa kila mwanamke na kufahamu kuwa nafasi za uongozi hawapaswi kuwa wanaume pekee.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud alisema kupitia mradi huo ambao utatekelezwa katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba na utawanufainisha wanawake 600.

Alisema kuwa wanawake hao kupitia mradi huo wa miaka minne ana imani kuwa wengi wao watakwenda kushika nafasi tofauti za uongozi kwa ngazi mbali mbali.

Sambamba na hilo alisema pia mradi huo utawajengea uwezo waandishi wa habari 60 kutoka Unguja na Pemba ambao watafanya kazi kupitia mradi kwa kipindi chote cha utekelezaji.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita (katikati) akifungua mafunzo ya siku nane kwa baadhi ya waandishi wa Habari Zanzibar yaliolenga kuwajengea uwezo katika kutambua haki za msingi za Wanawake ikiwemo kushiriki katika nafasi za uongozi.
Mkufunzi wa maswala ya haki za Wanawake, Dkt. Ananilea Nkya akitoa mafunzo kwa baadhi ya waandishi wa Habari Zanzibar yaliolenga kuwajengea uwezo kutambua haki za msingi za wanawake ikiwemo ushirikishwaji katika nafasi za uongozi,mradi huu wa miaka minne unatekelezwa na TAMWA-Z’bar,ZAFELA pamoja na PEGAO chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania.
Baadhi ya washiriki ambao ni waandishi wa habari wakifuatilia mafunzo hayo.

Post a Comment

0 Comments