Header Ads Widget

USAFIRI WA ‘HIACE’ MANISPAA YA SHINYANGA KUANZA APRILI, MKURUGENZI AAHIDI KUKAMILISHA UJENZI MABOMA YA ZAHANATI

Meya Mstahiki wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila akisisitiza mambo mbalimbali leo wakati akihairisha kikao cha baraza la madiwani wa manispaa ya Shinyanga kilichofanyika kwenye ukumbi wa manispaa hiyo.

Na Damian Masyenene, Shinyanga
IMEBAINISHWA kuwa usafiri wa abiria kwa kutumia daladala za Hiace na bajaji katika manispaa ya Shinyanga mkoa wa Shinyanga utaanza rasmi Aprili, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi wakati akijibu maswali ya hapo kwa hapo ya madiwani kwenye baraza la kawaida la madiwani wa manispaa hiyo na kueleza kuwa ndani ya mwezi huu watafanya kikao na wamiliki wa bajaji na magari ili kufikia makubaliano ya pamoja.

Akijibu swali la Diwani wa Kata ya Mwawaza, Juma Nkwambi aliyetaka kufahamu ni lini huduma ya usafiri wa daladala (Hiace) iliyoazimiwa na baraza la madiwani lililopita (2015/2020) itaanza kufanya kazi, Mkurugenzi Mwangulumbi amesema kuwa kabla ya baraza la madiwani la Aprili, mwaka huu usafiri huo utaanza rasmi.

“Baraza liliazimia usafiri wa hiace na bajaji uanze haraka iwezekanavyo, zoezi limeanza kuratibiwa na mwezi huu (Februari) tutawaita wamiliki wa hiace na bajaji na kukutana nao kuazimia usafiri uanze.

“Na tunaahidi kabla ya baraza la Aprili basi usafiri huo utaanza rasmi kwa maana ndani ya mwezi Machi na Aprili,” amesisitiza.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila amekazia na kueleza kuwa baada ya huduma ya daladala kuanza kazi, baiskeli zinazobeba abiria hazitoruhusiwa kuingia katikati ya mji badala yake wataruhusiwa kuendelea na huduma hiyo maeneo ya pembeni ya mji.

Nkulila amewaomba madiwani wa halmashauri hiyo kutogawanyika kwani wote wanaijenga Shinyanga na wala hakuna kata yenye upendeleo, huku akiamini kwamba yote yaliyowasilishwa yatatekelezwa na ni wajibu wa kila mmoja hivyo wanatakiwa kushirikiana na kushikamana.

Manispaa ya Shinyanga imekosa usafiri wa ndani wa uhakika wa daladala na bajaji, huku usafiri wa daladala za baiskeli ukishika kasi na kuwa mkombozi pekee kwa mizunguko (route) ya mjini.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huo amesema kuwa maboma ya zahanati mbalimbali na kituo cha afya Butengwa yaliyosimama kwa muda mrefu yataendelezwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha ili yaanze kutoa huduma kwa wananchi.

Akijibu swali la Diwani wa Kata ya Kitangiri, Mariam Nyangaka aliyehoji kuhusu hatma ya maboma nane ya zahanati na kituo cha afya Butengwa ambavyo viko hatua ya renta na vimesimama kwa muda mrefu, Mkurugenzi Mwangulumbi ameeleza kuwa maboma hayo anayatambua na utekelezaji wake umo kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021, ambapo kituo cha afya Butengwa kitaendelezwa na kuingizwa tena kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 na ana imani kwamba kitakamilika.

“Maboma mengine pia yamo kwenye bajeti na yasipo kamilika yataingizwa kwenye bajeti mpya kama ilivyoagizwa na baraza la madiwani,” amesema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masekelo, Peter Koliba amehoji ni lini zahanati ya kata hiyo itaanza kujengwa kwani imesimama kwa muda wa miaka mitano ikiwa hatua ya renta ambayo ingeweza kuhudumia wananchi zaidi ya 15,000, huku Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu akihoji mipango ya halmashauri kujenga kituo cha afya katika kata hiyo ambayo haina zahanati ikiwa na wakazi zaidi ya 47,000.

Akijibu hoja za madiwani hao wawili, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geoffrey Mwangulumbi, amesema kuwa katika zahanati ya Masekelo tayari wameweka mikakati ya kuikamilisha na kuahidi kuwa ujenzi wake utakamilika kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, huku akieleza kuwa ujenzi wa kituo cha afya kata ya Ngokolo hauko kwenye mipango badala yake wataendelea na mipango ya ujenzi wa zahanati katika mtaa wa Kalonga.

Naye Diwani wa Kata ya Ndala, Zamda Shaban amehoji ni lini wakazi wake watapata hati za viwanja vyao ambavyo wamepimiwa muda mrefu na tayari wameshafanya uendelezaji, ambapo Mkurugenzi Mwangulumbi ameeleza kuwa zoezi limekwishakamilika na kumtaka awaelekeze wananchi wafike idara ya ardhi kupata hati zao, huku akihimiza wananchi wahamasishwe kuomba hati miliki za ardhi kwani tayari ofisi ya kamishna wa ardhi ipo mkoani Shinyanga.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, kikao hicho kilianza kupokea taarifa za utendaji katika kata 17 ambazo zinatoa mustakabali wa manispaa hiyo, ambapo hoja mbalimbali ziliibuka ikiwemo kukithiri kwa uchafu katika masoko na dampo, wagonjwa kufurika katika hospitali ya wilaya ya Kambarage, wakopeshaji wasiofuata utaratibu, upungufu wa watumishi, ubovu wa barabara, shule mpya ya sekondari Mwangulumbi kukosa mkuu wa shule na msaidizi wake pamoja na utendaji usioridhisha wa kitengo cha dharura Tanesco.

Akijibu hoja kuhusu kulega kwa kitengo cha dharura Tanesco, Kaimu Meneja wa shirika hilo mkoa wa Shinyanga,  Mhandisi Antony Tarimo amekiri kuwa kutokana na ukubwa wa eneo wanalolihudumia, kitengo kimekuwa kikizidiwa na kushindwa kutoa huduma kwa wakati, ambapo tayari wameanza kuchukua hatua kwa kuanzisha kituo katika eneo la Solwa na Isaka na kuviwezesha kujitosheleza kuweza kuhudumia maeneo ya pembezoni mwa mji.

Pia ameeleza kuwa miundombinu mingi ya umeme katika mji huo ni chakavu na ya muda mrefu, ambapo ili kumaliza changamoto zilizotokana na itilafu za miundombinu kutokana na mvua kubwa  iliyonyesha juzi, leo Februari 16 ofisi ya Tanesco mkoa wa Shinyanga wamesitisha shughuli zote na kujielekeza kutatua changamoto za dharura zilizojitokeza.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila amewataka Tanesco kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kufanya maboresho kuliko kusubiria madhara ya mvua ndipo waingie kwenye gharama kubwa za kufanya maboresho.

Nkulila ameutaka uongozi wa manispaa hiyo chini ya Mkurugenzi Geoffrey Mwangulumbi kumaliza kero ya kukithiri uchafu kwenye masoko na vituo vya kukusanyia (Ghuba) na kuhakikisha inaisha ili kuleta ufanisi.

TAZAMA PICHA HAPA
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila akitoa maelekezo juu ya hoja mbalimbali wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa manispaa ya Shinyanga kilichofanyika leo mjini Shinyanga
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila akizungumza na madiwani pamoja na watendaji wa halmashauri hiyo na wale wa taasisi za serikali waliohudhuria kikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo leo kwenye ukumbi wa manispaa
Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa Shinyanga, Geoffrey Mwangulumbi akifuatilia hoja na maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na madiwani wa manispaa hiyo leo kwenye kikao cha baraza la madiwani hao
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga, Boniphace Nchambi akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali zilizoibuka katika kikao hicho
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila akizungumza katika kikao hicho
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Mjini, Moshi Kanji akiwasilisha taarifa ya utekelezaji katika kata hiyo kwa niaba ya Diwani, Gulamhafidh Mukadam
Madiwani wakifuatilia taarifa mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kikaoni hapo
Diwani wa Kata ya Masekelo, Peter Koliba akipitia kwa umakini taarifa utekelezaji katika kata 17 za manispaa ya Shinyanga iliyowasilishwa kwenye kikao cha baraza la madiwani leo
madiwani wakiendelea kupitia taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo
Madiwani wakipitia na kusoma taarifa mbalimbali zilizowasilishwa kwenye kikao hicho

Kikao cha baraza hilo kikiendelea
Madiwani wakiendelea kupitia taarifa zilizowasilishwa

madiwani kiendelea kupitia na kuhakiki taarifa za ripoti hiyo
Madiwani wakiendelea kuipitia taarifa hiyo
Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu (kulia) akifuatilia majibu yaliyokuwa yakitolewa na Mkurugenzi wa Manispaa juu ya ujenzi wa zahanati na kituo cha afya katika kata hiyo
Diwani wa Viti Maalum kata ya mjini, Moshi Kanji akiwasilisha taarifa ya kata hiyo
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Mjini, Shela Mshandete akifuatilia kwa umakini hoja mbalimbali katika kikao hicho
Baadhi ya watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali wakiwa sehemu ya kikao hicho
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Manispaa ya Shinyanga, Lucy Sewe (kulia) akipitia taarifa hiyo ya utekelezaji
Viongozi wa chama (CCM) na katibu wa Mbunge wakiwa sehemu ya kikao hicho
Watendaji mbalimbali wa serikali wakiwa ni sehemu ya kikao hicho

Baadhi ya watumishi wa manispaa ya Shinyanga nao wakifuatilia kikao hicho




Post a Comment

0 Comments