Header Ads Widget

NAIBU WAZIRI AMPA SIKU 44 MKANDARASI CHUO CHA UALIMU SHINYANGA, APATA MASHAKA UJENZI VETA KISHAPU

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipang (katikati) akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa Kampuni ya Afrique Engineering & Co. Ltd inayosimamia ujenzi na ukarabati wa majengo katika chuo cha ualimu Shinyanga, Thadeus Koyanga (kushoto) ambaye anadaiwa kuchelewesha mradi huo, ambapo amepewa siku 44 kuukamilisha na kuukabidhi kwa serikali. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko.

Na Damian Masyenene, Shinyanga
KUENDELEA kuchelewa kukamilika kwa mradi wa ukarabati na ujenzi wa majengo mapya katika Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHY COM), kumemkera Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga ambaye amelazimika kumpa mkandarasi anayesimamia mradi huo, kampuni ya Afrique Engineering and Co. Ltd kukamilisha ujenzi huo ifikapo Machi 31, mwaka huu ili madarasa hayo yaanze kutumika kuanzia Aprili 9, mwaka huu wanafunzi watakaporejea chuoni hapo.

Mradi huo wenye thamani ya Sh Bilioni 5.2 unaohusisha ujenzi wa bweni la wavulana, majengo mawili ya madarasa, ukumbi na ukarabati wa bwalo la chakula ulianza Agosti 2016 na ulitarajiwa kukamilika Aprili 5, mwaka 2018 lakini umekuwa ukilegalega na kuchelewa kukamilika, ambapo hadi sasa mkandarasi amekwishalipwa asilimia 76 ya mkataba wake.

Akitoa maagizo jana Februari 15, 2020 baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga amesema kushindwa kutimiza maagizo hayo kwa Mkandarasi ni kujitia matatizoni, ambapo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko kupita kila wiki kukagua maendeleo ya ujenzi huo na kujiridhisha.

Naibu Waziri huyo aliwataka pia washauri wa mradi huo, kampuni ya Bureau for Industrial Construction kukaa eneo la mradi huo hadi hapo utakapokamilika Machi 31, mwaka huu, kwani imebainika kuwa washauri hao wamekuwa hawaonekani eneo la mradi na kusababisha ujenzi kulegalega na kubainika mapungufu kadhaa ya kiufundi.

“Mkandrasi amekaa eneo la mradi miaka mitano, mwenzake waliyeanza nae alishamaliza zamani, kwahiyo sasa maagizo yangu ni kwamba kufika Machi 31 mwaka huu kazi zote katika eneo hili ziwe zimekamilika, hadi sasa ukiangalia kazi nyingi za nje hazijasogea kabisa, kwahiyo kuanzia Aprili mosi tuanze majaribio (testing) ili Aprili 9 wanafunzi wanapokuja yawe tayari kutumika.

“Kushindwa kufanya hivyo ni kujitia matatizoni, tumekubaliana hivyo hakuna visingizio vingine. Pia washauri wa mradi fanyieni kazi mapungufu yote,” amesisitiza.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amemshauri Naibu Waziri huyo kufikiria kutumia mafundi wazawa kwani wakandarasi wamekuwa wakichelewesha miradi mingi inayohitajika kwa haraka, huku akimtaka mkandarasi kuongeza nguvu kazi ya mafundi ili eneo lake la kazi lichangamke na kazi ziende kama inavyotarajiwa.

“Kwa sasa kila eneo lake hakuna lililokamilika kwa asilimia 100, sisi tutaendelea kumsimamia kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa sababu kwa sasa imegeuka hadi kero kwa wanafunzi, unakuta mwanafunzi kaingia hapa mwaka wa kwanza anaona majengo hadi anahitimu chuo hajayatumia,” amesema.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Shinyanga, John Nandi amesema kuwa chuo hicho kinachotoa astashahda ya ualimu wa msingi, sekondari na masomo ya biashara kinao wanafunzi 580, huku kikiwa na upungufu wa walimu wa masomo ya kiingereza na hisabati, ambapo aliiomba serikali kufikiria kukarabati nyumba za walimu kwani nazo zimechakaa sana pamoja na majengo mengine ya chuo ambayo hayako kwenye mradi.

Naibu Waziri huyo aliitimisha ziara yake mkoani Shinyanga kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi (VETA) cha wilaya ya Kishapu kinachojengwa katika Kata ya Igaga kinachogharimu Sh Bilioni 1.6 kikijumuisha majengo 17, ambapo hadi sasa majengo nane yamefikia hatua ya upauaji, sita hatua ya boma, moja liko kwenye renta na mawili hatua ya kufunga mkanda wa juu.

Akiwa katika eneo hilo ambalo alianza ukaguzi majira ya saa 11 jioni hadi saa 2 usiku, Naibu Waziri Omari Kipanga ameonyesha mashaka juu ya maendeleo ya ujenzi huo na kuhofia uwepo wa dalili za rushwa kwani matumizi ya fedha ni makubwa kulinganisha na kazi iliyofanyika, ambapo ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kuupitia mradi huo, huku akionya kuwa yeyote ambaye amecheza na fedha za mradi huo basi atawajibika.

Kipanga amewataka VETA wanaosimamia mradi huo kuhakikisha unakamilika Machi 30, mwaka huu kama ilivyo kwenye mkataba na kurekebisha kasoro zilizobainika kwenye mradi huo ikiwemo usimamizi dhaifu wa kazi na kuwataka kufanya kazi usiku na mchana ili kumaliza ndani ya muda.

“Hapa mmetumia zaidi (matumizi ni makubwa) kwahiyo usimamizi wa fedha siyo mzuri, kwahiyo niwahakikishie kuwa yeyote ambaye amecheza nah ii fedha haitamuacha salama, mtu wa Takukuru aupitie ajiridhishe.

“Asilimia 60 ya fedha yetu ilikuwa iwe imeshapaua na kuezeka, lakini matumizi ni makubwa kuliko kazi iliyofanyika, ujenzi umefikia asilimia 35 na kiasi cha Sh Bilioni 1.2 zimeshatumika sawa na asilimia 75 ya fedha zote….fundi mmoja anakabidhiwa majengo matano anashindwa kufanya kazi kwa ufanisi na kwa mwendo huu sioni hata dalili za kumaliza kazi Machi 31, mwaka huu,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo tangu mwanzo ulionekana kuwa gharama hazitatosha na ndiyo maana vibarua wa mwanzo walikimbia na hata wanaojenga kwa sasa siyo wa eneo hilo kwani inaonekana wanajenga kwa bei ya chini, ambapo kuna wakati ujenzi ulichelewa kuanza kutokana na vifaa kukosekana na nguvu kazi kuwa ndogo.

Ambapo, amewataka wasimamizi wa mradi huo na mafundi kuwajibika ili mradi ukamilike kwa wakati na wakabidhiwe ukiwa na ubora unaotakiwa, huku akiahidi kuwaletea ulinzi ili wafanye kazi usiku na mchana, na endapo mtu yeyote ataleta masihara katika hilo basi ataswekwa ndani.

“Kama alivyoagiza Naibu Waziri kwamba majengo haya yakamilike ndani ya muda, nasi tunapenda iwe hivyo kweli kama wana Kishapu tukabidhiwe kitu kilicho bora. Kama kuna mtu mzuri anayeweza kusimamia hii kazi hapa ‘Site’ aletwe kazi iende kadri ya makadirio,” amesema.

Awali Mkuu wa Chuo cha VETA mkoa wa Shinyanga ambao wanasimamia mradi huo, Magu Mabelele alisema kuwa eneo la chuo hicho ni ekari 48 ambalo lipo Km 1 kutoka barabara ya Muunze -Kishapu-Shinyanga, ambapo ujenzi wake ulianza Januari 24, mwaka jana na wanatarajia kukamilisha mradi ifikapo Machi 31, mwaka huu na kwa sasa ujenzi umefikia wastani wa asilimia 52, huku wakitarajia kufikia mwisho wa mwezi huu kupaua na kuezeka majengo nane.

Amesema hadi sasa wameshapokea Sh Bilioni 1,199,656,904 na jumla ya Sh 1,190,253,513 zimeshatumika hadi kufikia Februari 14, mwaka huu, huku wakitarajia kudahili wanafunzi 240 katika fani sita ambao watakuwa wa bweni na kutwa, huku wanafunzi wa bweni wakitarajiwa kuwa 144 wakiwemo wasichana 64 na wavulana 80.

Katika hatua nyingine, akipokea taarifa ya elimu mkoa wa Shinyanga iliyowasilishwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Beda Chamatata, Naibu Waziri Omari Kipanga amewataka viongozi wa mkoa huo kuwafuatilia wanafunzi zaidi ya 7,000 ambao walipangiwa shule kidato cha kwanza mwaka huu lakini hadi sasa hawajaripoti, ambapo ameomba wafuatiliwe ijulikane wako wapi na kwa nini hawajaripoti.

Naibu Waziri huyo alikagua pia maendeleo ya ujenzi wa bweni, vyoo vya nje, karakana na jengo la utawala katika chuo cha maendeleo ya wananchi Buhangija mjini Shinyanga, ambapo mradi huo umetengewa jumla ya Sh Milioni 664 na ujenzi ulianza Novemba mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu ukiwa tayari umeshatumia jumla ya Sh Milioni 208.2, ambapo kukamilika kwake kutaongeza udahili wa wanafunzi na kufikia 208 kutoka 106 waliopo sasa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga (aliyeshika karatasi) akikagua maendeleo ya ujenzi mradi wa ukarabati majengo katika chuo cha ualimu Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akimueleza mambo mbalimbali juu ya mradi wa ukarabati wa majengo chuo cha ualimu Shinyanga, Niabu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga (wa pili kushoto)
Mkandarasi anayesimamia ujenzi huo, Thadeus Koyanga (wa tatu kushoto) akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwa Naibu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga (aliyevaa kofia nyeupe) juu ya maendeleo ya mradi huo. Kushoto ni Mshauri wa mradi huo, Emmanuel Moshi
Naibu Waziri, Omari Kipanga pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko wakiendelea na ukaguzi chuoni hapo
Ukaguzi ukiendelea
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akimueleza mambo mbalimbali, Naibu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga ikiwemo kutoonekana kwa washauri wa mradi katika eneo la kazi na kasoro kadhaa za kiufundi katika mradi huo
Muonekano wa jengo la bweni linalojengwa katika chuo cha maendeleo ya wananchi Buhangija wilayani Shinyanga
Muonekano wa jengo la utawala la Chuo cha ufundi stadi (VETA) wilaya ya Kishapu linalojengwa katika kijiji cha Igaga A
Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa VETA wilaya ya Kishapu, Godias Kayego (aliyenyoosha kidole) akitoa ufafanuzi mbalimbali kwa Naibu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga alipokuwa akifanya ukaguzi kwenye mradi huo
Naibu Waziri, Omari Kipanga na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba wakipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa mradi huo kutoka kwa msimamizi wa mradi, Godias Kayego
jengo mojawapo linalojengwa katika mradi wa VETA wilaya ya Kishapu
Majengo ya karakana na bweni la wavulana
jengo la choo na bweni la wasichana
Naibu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga akitoa maelekezo kwa viongozi wa wilaya ya Kishapu
Naibu Waziri akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi ili kuhakikisha unakamilika ndani ya muda uliopangwa

Naibu Waziri akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa mafundi wanaotekeleza mradi huo




Post a Comment

0 Comments