Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Edson Makallo akifungua mafunzo ya Ukusanyaji, Uchakataji, Utumaji na Utunzaji wa Takwimu  za Kesi za Jinai na Kumbukumbu za Makosa ya Rushwa kwa Makatibu Sheria yanayofanyika mkoani Singida kuanzia tarehe 3 Februari,2021 hadi tarehe 08 Febry,2021. Kushoto kwa Bw. Makallo ni  Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uratibu wa Upelelezi Bi. Neema Mwanda.Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Edson Makallo akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya Ukusanyaji, Uchakataji,Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai na Kumbukumbu za Makosa ya Rushwa kwa Makatibu Sheria yanayofanyika Mkoani Singida kuanzia leo tarehe 3 Februari 2021 hadi 08 Februari,2021. Kushoto ni Mkurugenzi wa Raslimali Watu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Sheusi Mburi pamoja na viongozi wengine kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Edson Makallo  amewasihi watumishi wa Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka kuzingatia Maadili katika maeneo yao ya kazi pamoja na kufanya kazi
kwa bidii.
Naibu Mkurugenzi Makallo ameyasema hayo mapema leo wakati
akifungua mafunzo ya ukusanyaji, uchakataji, utumiaji na utunzaji wa takwimu za
kesi za Jinai na kumbukumbu  za makosa ya
Rushwa kwa Makatibu Sheria wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yanayofanyika Mkoani
Singida kuanzia tarehe 03 Februari 2021.hadi tarehe 08  Februari,2021
Bw. Makallo amesema kada ya utumishi wa Makatibu wa  Sheria inakumbana na changamoto mbalimbali za
kiutendaji na kimaadili  hivyo mafunzo hayo
wanayopatiwa yatumike kuwasaidia na kuboresha utendaji wao wa kazi.
Amesema katika miaka ya karibuni dunia imeshuhudia kuwepo
kwa mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu
kiuchumi,kijamii, kisiasa, kiteknolojia na kiutamaduni ambapo athari za mabadiliko  hayo ni pamoja na kubadilika kwa mbinu za kupanga
na kutekeleza uhalifu na hivyo kuwataka Makatibu wa Sheria wakiwa ni miongoni
mwa watoa huduma katika taasisi ya Haki Jinai kukumbuka kuwa wana jukumu kubwa
la kuhakikisha wanashiriki katika kupambana na kuzuia uhalifu huo kwa njia ya
kutekeleza vema majukumu yao.
Aidha, amesema kuwa  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imejipanga vyema
katika kushughulikia matendo ya mmomonyoko wa maadili kwa watumishi wa Umma
ambapo hatua madhubuti zimekuwa zikichukuliwa kwa watumishi wanaobainika
kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Amesema watumishi wa Umma wakizingatia miiko iliyopo katika
utendaji wao wa kila siku huleta matokeo chanya kwa huduma wanazotoa kwa jamii
na hivyo jamiu hujenga imani kwa serikali na kuleta hali ya Usalama.
Bw. Makallo alitoa rai kwa Makatibu Sheria waliohudhuria
mafunzo hayo  kuwa kila aliyepata mafunzo
arudipo katika sehemu yake ya kazi 
kuweka ujuzi aliopata kwa vitendo na kushirikisha ujuzi walioupata kwa
wengine  ambao hawajapata nafasi ya
kuhudhuria mafunzo ili kupanua ushiriki wa mafunzo wa Makatibu Sheria wengi
zaidi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutunza siri zinazohusu
taarifa za majalada yanayowafikia  huku
wakielewa kwamba suala la utunzaji wa siri ni la lazima kwa watumishi wote wa
Umma.
Mafunzo hayo ya siku sita kwa Makatibu Sheria  yameandaliwa kwa ushirikiano wa Divisheni ya
Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi 
na  Divisheni ya Makosa ya
Udanganyifu, Utakatishaji Fedha na Rushwa  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zitatolewa zikiwepo mada juu ya Maadili ya Makatibu Sheria, Kutunza na kushughulikia majalada ya rushwa, ukusanyaji, uchakataji na utumaji wa takwimu za kesi, utunzaji na mfumo wa regista ya ofisi,mfumo wa kielektroniki wa upokeaji na utunzaji wa majalada, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za serikali pamoja na.masuala mengine yanayohusu maadili.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya  Usimamizi wa Kesi za Jinai   Bw. Tumaini Kweka akizungumza  katika mafunzo ya ukusanyaji, uchakataji na
utumiaji wa takwimu na kumbukumbu za makosa ya rushwa kwa Makatibu Sheria
yanayofanyika Mkoa wa Singida kuanzia leo tarehe 3 Februari, 2021 na kumalizika
tarehe 08 Februari,2021.
Katibu Sheria Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Gilley Manara akitoa taarifa ya majukumu ya kiofisi katika mafunzo ya ukusanyaji, uchakataji na utumiaji wa takwimu na kumbukumbu za makosa ya rushwa yanayofanyika Mkoani Singida kuanzia tarehe 3 Februari, 2021 na kumalizika tarehe 8 Februari, 2021.
