Header Ads Widget

BAADA YA KUMUUA BABA MKWE, MAHAKAMA YAMHUKUMU KUTOKUNYWA POMBE MIEZI 12


Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, imemuachia huru Boniphace Kachila, mkazi wa Kijiji cha Kiyungwe wilayani Kasulu mkoani humo kwa sharti la kutokutenda kosa na kutokunywa pombe ndani ya miezi 12, baada ya Mahakama hiyo kumtia hatiani kwa kosa la kumuua baba mkwe wake bila kukusudia.

Kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2021, kati ya Jamhuri na mshtakiwa Boniphace Kachila, kosa linaloelezwa kutendeka Juni 13 ,2019, baada ya mshtakiwa wakiwa na marehemu wakitoka kwenye klabu cha pombe wamelewa walianza kugombana ambapo inadaiwa kuwa marehemu Ndolele Donansiano, alipigwa ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili na kufa muda mfupi baada ya ugomvi huo, na uchunguzi wa daktari ulionesha alipasuka fuvu na kusababisha damu kuvuja.

Maelezo ya kesi hiyo yametolewa na Wakili wa serikali Clement Masua, na kusema kuwa mara baada ya tukio hilo mshtakiwa Boniface, aliandika maelezo ya kuuwa bila kukusudia na maelezo ya ungamo huku akiitaka Mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwake ili iwe fundisho kwani marehemu alikatiliwa haki yake ya msingi ya kuishi na alikuwa na familia inayomtegemea.

Wakili wa upande wa utetezi Sadiki Aliki, aliiomba Mahakama impunguzie adhabu mtea wake ikiwezekana kuwe na mbadala wa kutokukaa gerezani kama hatua ya kupunguza msongamano, huku akieleza kwamba mazingira ya mauaji hayo yalikuwa ya bahati mbaya kama ajali kwani mshtakiwa alikuwa mtu wa karibu na marehemu na anategemewa na wake wawili, watoto saba na mama yake mzazi mwenye umri wa miaka 80 na pia ameshapata funzo kwani amekaa mahabusu mwaka mmoja na miezi nane.

Akitoa hukumu hiyo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Jaji Athumani Matuma, amesema kwa kuzingatia pande zote mbili na mazingira ya kosa ni wazi mshtakiwa anahitaji huruma ya Mahakama kwani amekuwa muungwana tangu hatua za awali kukubali kosa na hakuna mahali popote kwenye mwenendo wa shauri hilo panaonesha kuna upelelezi ulifanyika ili kumbaini aliyeanzisha ugomvi, kwani wakati wanagombana hakuna aliye kuwepo hivyo mshtakiwa angeweza kudanganya.

Hivyo Jaji Matuma amesema kuwa Mahakama hiyo inamuachia huru mshtakiwa kwa sharti la kutokufanya kosa lolote katika kipindi cha miezi 12 ikiwemo sharti la kutokunywa pombe kwa kipindi hicho cha uangalizi na endapo sharti lolote litakiukwa atarudishwa mahakamani hapo kuhukumiwa kwenda jela.
TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807