Header Ads Widget

TWIGA MINERALS YALIPA USHURU WA SH BILIONI 2.387 KAHAMA NA MSALALA, DC ASHAURI ZIMALIZE CHANGAMOTO ZA ELIMU NA AFYA

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (katikati), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Yahya Bundala na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Anderson Msumba (kushoto) wakipokea hundi ya Sh Bilioni 1.6 kutoka kwa Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu ambayo ni malipo ya ushuru wa huduma kwa miezi sita (Julai hadi Desemba, 2020).

Na Damian Masyenene, Kahama 
KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Twiga Minerals, ambayo ni kampuni iliyoundwa kwa ushirikiano baina ya kampuni ya madini ya Barrick na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kupitia migodi yake ya Dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, imekabidhi hundi zenye jumla ya thamani ya Sh 2,387,745,061.23 kwa manispaa ya Kahama na halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga ikiwa ni malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, mwaka jana. 

Mgodi wa Buzwagi umelipa kiasi cha Sh 1,642,815,335.45 kwa Manispaa ya Kahama, huku mgodi wa Bulyanhulu ukilipa Sh 744,929,725.78 kwa halmashauri ya Msalala, ambapo Migodi ya Twiga Minerals hulipa ushuru wa huduma kila baada ya miezi sita kwa halmashauri ambazo migodi hiyo inaendesha shughuli zake kulingana na mapato ya kila mwaka. 

Makabidhiano hayo yamefanyika leo mjini Kahama katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya manispaa ya Kahama ikihudhuriwa na wakurugenzi wa halmashauri hizo mbili pamoja na watendaji mbalimbali wa serikali. 

Akipokea hundi hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha ametoa maelekezo kwa halmashauri zilizolipwa ushuru huo kuwekeza fedha hizo kwenye sekta ya elimu na afya kwa kuhakikisha miundombinu inayohitajika ikiwemo vyumba vya madarasa na vituo vya afya vinamalizika na kuondoa kasumba ya kusubiri wahamasishwe na viongozi wa kitaifa katika kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta hizo. 

“Maelekezo kwa halmashauri hizi ni kwamba fedha hizi zitumike kukidhi mahitaji ya wananchi na tuache kuzihusisha na mambo madogo yasiyo ya msingi. Ningependa fedha hizi zipelekwe kwenye elimu kwa kumalizia upauaji wa maboma ya madarasa na kununua madawati ili maandalizi ya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza kwa mwaka 2022 yaanze sasa hivi na tuwe na utaratibu wa madarasa kusubiri wanafunzi siyo kusubiri kukumbushwa na viongozi. 

“Nia yetu ni kuhakikisha ikifika Desemba watu waende likizo, wasisubirie kuzuiliwa ili wakamilishe vyumba vya madarasa. Pia kwenye afya tunavyo vituo na zahanati ambazo zimekaa muda mrefu na kuchakaa ama kutomalizika tuhakikishe vinakamilika,” ameelekeza. 

Akikabidhi hundi hiyo, Meneja Mkuu wa Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, Benedict Busunzu amesema kuwa wanaona fahari kubwa kuona matunda ya matumizi sahihi ya fedha hizo katika uboreshaji wa miundombinu mbalimbali inayoimarisha uchumi na huduma muhimu kwa ajili ya wananchi, huku akiahidi kampuni hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kujenga jamii endelevu ili kuendana na mpango wa maendeleo wa miaka mitano na dira ya taifa 2025. 

“Kipimo cha mafanikio kwetu ni matokeo chanya na endelevu yanayotokana na mchango wa fedha hizi, hivyo tunafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya maendeleo ya Kahama, Msalala na hata mkoa wa Shinyanga kwa ujumla, kwani tumeshuhudia mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupandishwa hadhi halmashauri ya mji wa Kahama na kuwa manispaa. Tunawapongeza sana viongozi kwa ushirikiano na juhudi tunazoziona za kusimamia vizuri matumizi ya fedha za ushuru wa huduma ambazo tunalipa kila kila baada ya miezi sita. 

“Juhudi hizo zinatuhamasisha kufanya kazi zaidi ili tuzalishe zaidi na tulipe ushuru mkubwa na kuendelea kuchangia zaidi maendeleo chanya katika mkoa wetu wa Shinyanga na manispaa ya Kahama na halmashauri ya Msalala,” amesisitiza. 

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama, Yahya Bundala ameshukuru migodi hiyo kwa kutoa fedha hizo, huku akisisitiza kuwa madiwani wataunga mkono mapendekezo ya mkuu wa wilaya ya kutaka fedha zilizopokelewa kuweka nguvu katika kutatua changamoto kwenye sekta ya elimu na afya. 
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akisisitiza jambo kwa watendaji wa halmashauri za manispaa Kahama na Msalala baada ya kupokea fedha hizo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Anderson Msumba (kushoto) na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Yahya Bundala wakiwa wameshikilia hundi yenye thamani ya Sh Bilioni 1.6 iliyotolewa na Mgodi ya Buzwagi kama sehemu ya malipo ya ushuru wa huduma
Mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala, Simon Berege (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha wakiwa wameshikilia hundi yenye thamani ya Sh Milioni 744.9 iliyotolewa na mgodi wa Bulyanhulu kwa halmashauri hiyo kama malipo ya ushuru wa huduma
Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hizo
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama, Yahya Bundala akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo

Viongozi hao kwa pamoja wakiwa wameshikilia hundi hizo baada ya hafla ya makabidhiano katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya manispaa ya Kahama


TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807