Header Ads Widget

TAKUKURU YANUSA UFISADI KANISANI, SH. BILIONI 11 ZA WAJANE NA YATIMA ZAPIGWA, MSD MATATANI


Na Shinyanga Press Club Blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imetoa taarifa ya shughuli zake kiuchunguzi, uelimishaji umma, udhibiti na uokoaji na urejeshwaji wa mali za umma na zile za watanzania wayonge katika kipindi cha miezi mitatu (Oktoba hadi Desemba mwaka 2020).

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana  na Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mara, Alex Kuhanda, katika kipengele cha uchunguzi wa uendeshaji mashtaka, taasisi hiyo ilipokea jumla ya malalamiko 233 na kuyafanyia kazi. Kati ya malalamiko hay0 jumla ya malalamiko 76 yalihusu tuhuma za rushwa katika uchaguzi mkuu. 

Katika chunguzi zingine zilizofanyika, Takukuru  iliweza kunusa harufu ya rushwa katika Kanisa la Mennonite Tanzania Wilayani Serengeti, ambapo baadhi ya watumishi na waumini wanatuhumiwa kutumia nafasi zao kuuza gari aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Kanisa hilo kwa Tsh Milioni 10 na kuleta sintofahamu miongoni mwa waumini. 

 "Gari hilo litaendelea kuwa mikononi mwa TAKUKURU hadi uchuguzi utakapokuwa umekamilika na uamuzi kufikiwa," alisema.

Katika hatua nyingine, Takukuru imeyafanyia kazi maelekezo ya Rais Dk. John Magufuli aliyoyatoa kwa watendaji wa Serikali alipokuwa mkoani Mara wakati wa kampeni za udiwani, ubunge na Urais 2020 kuwasaidia wajane na yatima katika kuwarejeshea faraja na mali zao zilizoporwa na kuangukia mikono ya wasimamizi umiza wa mirathi. 

Katika kulitekeleza hilo, Kuhanda alisema kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita imeweza kuchunguza na kubaini uwepo wa wasimamizi umiza wa mirathi ambapo jumla ya kiasi cha Tsh bilioni 11, nyumba tano na magari mawili mali za marehemu kutoka familia tofauti zilianguikia mikononi mwa wasimamizi wa mirathi umiza na kuwaacha wajane na yatima wakihagaika, huku uchunguzi wa matukio hayo ukiwa katika hatua za mwisho.

"Kwa robo ya kipindi chote cha kuanzia Januari 2021 hadi mwisho wa mwaka wa fedha Juni 2021, pamoja na mambo mengine, TAKUKURU Mkoa wa Mara inajipanga kukamilisha chunguzi zote ziazohusiana na mirathi (kiasi cha Tsh 200 bil tuhuma ambazo tumeshazipokea)," alibainisha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TAKUKURU Mkoa wa Mara imenusa ufisadi wa kutisha wenye kuhatarisha maisha ya watanzania unaofanywa na Duka la Madawa ya Serikalini (MSD) Kanda ya Ziwa, kwa kusambaza madawa ya binadamu yanayokaribia au yaliyokwisha muda wake na hivyo kupoteza sifa ya kuendelea kutumiwa na binadamu. 

"Mchezo huu si kwamba unaathiri watumiaji wa madawa hayo bali pia kuhujumu uchumi kwani yananunuliwa kwa gharama kubwa kwa kutumia fedha za walipa kodi.

"Katika uchunguzi huu tulifanikiwa kupita katika baadhi ya Hospital, vituo vya Afya na zahanati, na tulibaini uwepo wa madawa ya binadamu yaliyokwisha muda wake box 40 zenye thamani ya Tsh 155.1 M. Kibaya zaidi madawa hayo yalikuwa yakiendelea kugawiwa huku wagawaji wakijua kuwa madawa hayo yalikuwa yameisha muda. 

"Uchunguzi wa nani alihusika kuingiza nchini madawa yaliyokaribia kuisha muda wake au nani aliyazuia madawa hayo kugawiwa kwa wahitaji yakiwa bado hayajaisha muda wake bado unaendelea," alieleza Kuhanda.

Vilevile, katika kuwarejeshea wananchi wayonge fedha walizoporwa na wakopeshaji umiza, taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu imefanikiwa kuokoa fedha kiasi cha Tsh Milioni 63.6, ambapo Sh Milioni 17.4M ni fedha zilizorejeshwa Serikalini baada ya baadhi waliobainika kukwepa kodi kubanwa na Takukuru na hatimaye kulipa kodi walizokuwa wakidaiwa. 

"Aidha kiasi cha Tsh Milioni 1.5 kilipokelewa na Wakala wa Misitu Tanzania Mkoa wa Mara kufuatia lori la mkaa tulilolikamata likikwepa kulipa ushuru. fedha zilizobaki kiasi cha Tsh Milioni 44.7 ni fedha zilizookolewa kutoka mikononi mwa wakopeshaji umiza na tulizirejesha kwa waliokuwa wameporwa ambao wengi ni walimu wastaafu. Pia trekta lenye thamani ya Tsh Milioni 39 Mali ya Serikali tulikabidhi Serikalini Desemba 2020," alisema.
 

TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807