Header Ads Widget

KAMPUNI YA MSILIKARE 'YAPORA' NYUMBA 2 ZA MJASIRIAMALI ZA SH. MILIONI 55 KISA MKOPO WA SH MILIONI 5, TAKUKURU YAZIREJESHA

Afisa Mchunguzi Mkuu wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Emily Mandia (kulia) akimkabidhi hati za nyumba mbili, Mjasiriamali Josephine Kiyuga alizokuwa ameporwa na mmiliki wa kampuni ya kutoa mikopo ya Msilikare baada ya kukopeshwa Sh Milioni 5.5. (Picha na Kadama Malunde)

Na Damian Masyenene, Shinyanga
NYUMBA mbili zenye thamani ya Sh Milioni 55 za mjasiriamali aitwaye Josephine Edward Kiyuga mkazi wa Viwanja vya Mwadui Manispaa ya Shinyanga, zimeokolewa na kurejeshwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa baada ya kuporwa isivyo halali na Mmiliki wa kampuni ya kutoa mikopo ya Msilikare, Robert Manyanyiho.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Francis Luena akitoa taarifa ya utendaji kazi ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2020-2021 (Oktoba-Desemba) mbele ya waandishi wa habari mjini Shinyanga, Mjasiriamali huyo ambaye anafuga kuku alikopa kiasi cha Sh Milioni 1.5 mnamo Septemba 19, mwaka jana kwa mmiliki wa kampuni ya Msilikare inayojishughulisha na kutoa mikopo katika Manispaa ya Shinyanga na kukubaliana kurejesha kiasi cha Sh Milioni 2.1 kwa muda wa mwezi mmoja.

Luena amesema, mnamo Septemba 25, mwaka jana mjasiriamali huyo alikopa tena kwa mmiliki huyo Sh Milioni 4 na kutakiwa kurejesha Sh Milioni 5.6 kwa muda wa mwezi mmoja lakini mmiliki wa kampuni hiyo alimuandikisha Mkopeshwaji mkataba wa mauziano ya nyumba na siyo mkataba wa ukopeshaji wa fedha. Hivyo basi, Jumla ya fedha alizokopeshwa ni Sh Milioni 5.5 ambazo alitakiwa kurejesha jumla ya Sh Milioni 7.7.

Hata hivyo, Mkopaji alifanikiwa kurejesha Sh Milioni 8 kama faida ya riba ya kuchelewesha kulipa deni, lakini mkopeshaji alikataa kurejesha hati za nyumba na kudai kuwa muda wa kurejesha deni ulishapita hivyo kama mkopaji anahitaji nyumba hizo inabidi azinunue tena kutoka kwake kwa gharama ya Sh Milioni 19 ili zitimie fedha hizo yaani Sh Milioni 19 mkopaji alitakiwa kuongeza Sh Milioni 11.

"Baada ya Takukuru mkoa wa Shinyanga kupata malalamiko hayo na uchunguzi kufanyika ilibaini kuwa mkopeshaji alikuwa na nia ya kujipatia nyumba hizo kwa njia isiyo sahihi. Hivyo basi, Takukuru mkoa wa Shinyanga iliweza kuziokoa nyumba hizo na zitakabidhiwa leo (Jumatano) kwa mwananchi huyo," alisema.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa hati za nyumba zake, Josephine Kiyuga ameeleza kuwa alipata matatizo katika biashara yake kwa kukosa chakula cha kuku hivyo akakutana na dalali ambaye alimuunganisha kwa Msilikare ili kupata mkopo, ambapo hatua zilifanyika na mmiliki wa kampuni hiyo akaenda kuziona nyumba na kukubali kumpa mkopo.

"Lakini alinigeuka, alifikia hatua ya kutaka kuuza nyumba zangu bila mimi kuwepo akiziita ni za kwake, akanipigia simu nikaondoe wapangaji. Nilifanya jitihada mbalimbali za kuongea nae na nikamlipa fedha lakini hakutaka kunipa nyumba zangu na nilikuwa nimekata tamaa baada ya jitihada mbalimbali kushindikana, ikabidi niende Takukuru ambao walinipa matumaini na hatimaye leo nimepata haki yangu, hili limenipa funzo kuwa makini na hii mikopo umiza," ameeleza.

Katika hatua nyingine, Takukuru imerejesha na kumkabidhi Mwalimu Mstaafu Sh Milioni 2.45 ikiwa ni sehemu ya Sh Milioni 45 zinazoendelea kurejeshwa zilizochukuliwa isivyo halali na wakopeshaji watatu tofauti ambao aliwalipa Sh Milioni 52, ambapo tayari Mwalimu huyo alikwishakabidhiwa Sh Milioni 26.6 katika kipindi cha Julai na Oktoba, mwaka jana.

Vile vile, Taasisi hiyo imefanikiwa kuzirejesha Jumla ya Sh Milioni 7.6 na kuwakabidhi wananchi mbalimbali waliokuwa wakidaiana wakiwemo wafanyabiashara, mafundi ujenzi na vibarua ambazo walidhulumiwa na mabosi wao.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Francis Luena, katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2020-2021 (Oktoba - Desemba), imeendelea kufuatilia miradi ya maendeleo inayopewa fedha za serikali na ufadhili wa wadau wa maendeleo, ambapo imefuatilia miradi miwili yenye thamani ya Sh Bilioni 2.7, huku ikipokea taarifa 54 ambazo baadhi uchunguzi umekamilika na nyingine bado unaendelea.

"Katika kipindi hicho Jumla ya wananchi 10,002 wameelimishwa kupitia elimu kwa umma, pia tumeweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi siku moja kila mwezi kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao," amesema.

Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Francis Luena akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Shinyanga wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi ya taasisi hiyo kwa kipindi cha robo ya pili (Oktoba -Desemba) ya mwaka wa fedha 2020-2021
Mjasiriamali, Josephine Kiyuga (kushoto) akifurahia na kuonyesha hati za nyumba zake mbili zilizorejeshwa na kukabidhiwa kwake leo na Takukuru baada ya kuporwa na mmiliki wa kampuni ya kutoa mikopo ya MsilikareAfisa Mchunguzi Mkuu wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Emily Mandia (kulia) akiwakabidhi fedha baadhi ya wananchi waliokuwa wamedhulumiwa na watu mbalimbali
Picha zote na Kadama Malunde

Mjasiriamali Josephine Kiyuga kionyesha nyumba zake mbili zilizokuwa zimechukuliwa isivyo haali (Picha na Marco Maduhu)
TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807