Header Ads Widget

SEKRETARIET YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA YAWATAHADHARISHA MADIWANI JIMBO LA SOLWA, MAKUSANYO YA NDANI YAFIKIA SH MIL. 954.4

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza na madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo wakati wa zoezi la kula kiapo cha uadilifu

Na Moshi Ndugulile -Shinyanga 
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wametakiwa kutanguliza mbele masilahi ya wananchi badala ya kulenga kujinufaisha wao binafsi, huku wakiaswa kufanya kazi kwa uadilifu ili utendaji wao uweze kuakisi kiapo walichokula. 

Kauli hiyo imetolewa Jana na Afisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Uongozi wa Umma Kanda ya Magharibi, Onesmo Msalangi baada ya kuwaapisha madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma. 

“Ndiyo maana tunawaasa nyinyi waheshimiwa,viongozi msiende kuwa mchwa katika Halmashauri zenu na badala yake tunawaomba mkaitumikie halmashauri yenu,mkawatumikie wananchi ambao ndiyo waliowatuma,wekeni pembeni maslahi binafsi” amesema Msalangi.
Onesmo Msalangi
Awali akizungumza katika kikao hicho ambacho ni cha kwanza tangu madiwani hao kuchaguliwa, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela amesema jukumu kubwa lilipo mbele ya madiwani hao ni kwenda kuwasikiliza wananchi ili kujua kero wanazokabiliana nazo kisha kutafuta ufumbuzi kwa kushirikiana na Halmashauri hiyo. 

Amewataka kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani ya CCM ikiwa ni pamoja na kuweka msukumo kwenye upatikanaji wa Maendeleo na huduma bora kwa wananchi. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amesisitiza madiwani hao kwenda kusimamia utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kusimamia vyanzo vya mapato vilivyopo katika kata zao ili kuchangia pato la Halmashauri hiyo. 

“Bila mapato hatuwezi kufanya kazi za halmashauri,vitega uchumi vilivyopo kwenye kata zetu vipatikane kwani fedha hizo ndizo zinazorudi kwenye vikundi vya ujasiliamali wanawake,vijana na wenye ulemavu, wote sasa tumerudi kufanya kazi ya kutekeleza ilani ya chama (CCM), yote tumekwishaelekezana kwenye vikao vya chama.

"Lakini pia nisisitize kupitia kikao hiki kila mmoja katika kata yake ahakikishe kazi zilizoainishwa kwenye ilani zinatekelezwa, zipo changamoto mbalimbali kwenye kata zenu hasa suala la madarasa kwa ajili ya watoto wetu wa kidato cha kwanza lakini pia wale wa shule za Msingi, tukasimamie, tuhamasishe, kwa kushirikiana na viongozi wetu wa Chama, Serikali, Maafisa Watendaji kata, maafisa tarafa, wenyeviti wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji” amesema DC Mboneko. 

Wakati huo huo Wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamemchagua Mheshimiwa Ngassa Mboje kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa kipindi cha Miaka mitano ijayo kuanzia sasa 

Mheshimiwa Mboje ambaye ni Diwani wa kata ya Mwalukwa amechaguliwa jana kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo kilicho fanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika kata ya Iselamagazi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
Ngassa Mboje
Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa muda wa kikao hicho katibu tawala wa Wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi amemtaja Mheshimiwa mboje kuwa ndiye mshindi wa nafasi hiyo baada ya kupigiwa kura 36 za ndiyo za madiwani wote waliohudhuria baraza hilo, na kwamba hakuna kura ya hapana wala iliyoharibika. 

Madiwani hao pia wamemchagua Mheshimiwa Izack Sengerema diwani wa kata ya Iselamagazi kuwa makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo 

Uchaguzi huo umefanyika baada ya majina ya Mwenyekiti na Makamu wake kuthibitishwa na Chama cha Mapinduzi CCM. 

Kabla ya uchaguzi huo kufanyika madiwani wote wa Baraza hilo walikula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma. 

Wakizungumza baada ya kuchaguliwa viongozi hao wameahidi kufanya kazi kwa uadilifu ili kuleta Maendeleo kwa Wananchi hao 

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngasa Mboje ameahidi utumishi uliotukuka kwa Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na madiwani wote pamoja na menejimenti. 

Amesema atahakikisha anasimamia vyema utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuweka msukumo katika ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa haki na usawa katika kata zote ili kuleta maendeleo kwa Wananchi bila upendeleo. 

Ngassa pia amewaomba wataalamu katika halmashauri hiyo wakiwemo maafisa kilimo,ughani na mifugo kuandaa mpango mkakati utakaolenga kuwasaidia Wakulima na wafugaji kutoka kilimo na ufugaji uliopitwa na wakati ili waweze kunufaika 

Amewataka kuja na mbinu za kitaalamu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu sahihi kuhusu kilimo cha kisasa na ufugaji bora,ushauri na maelekezo ili weze kunufaika. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi Hoja Mahiba, amesema Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh 954,448,747.48 sawa na asilimia 37 ya makisio ya mapato ya ndani ya Sh 2,552,536,677.04 kwa Mwaka wa fedha 2020/2020 

Mahiba amesema taarifa hiyo inajumuisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta mbalimbali zilizofanyika katika kipindi cha Julai hadi Novemba Mwaka huu 2020,kwa kuzingatia kanuni,taratibu,sheria na miongozo mbalimbali ya sekretariety ikiwemo ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi (CCM) 

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga lina Jumla ya Madiwani 37 wote kutoka Chama cha Mapinduzi CCM, waliochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Nchini kote Oktoba 28,Mwaka huu ambapo jana waliokula kiapo cha ahadi ya uadilifu ni 36,huku mmoja kati yao ikielezwa hakuhudhuria kwa taarifa. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba

Post a Comment

0 Comments