Header Ads Widget

MSICHANA INITIATIVE YAWAKUTANISHA VIONGOZI WA DINI NA MILA SHINYANGA VITA DHIDI YA NDOA ZA UTOTONI, RC TELACK ASEMA UZEMBE WA WAZAZI NI TATIZO

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (wa tatu kutoka kulia waliokaa), Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (kulia kwa mkuu wa mkoa), Mkuu wa Wilaya ya Kishapu (wa kwanza kulia waliokaa), Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Hadon Addou (wa kwanza kushoto waliokaa) na Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Rebecca Gyumi (wa pili kushoto waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa kimila waliohudhuria kikao cha kujadili umuhimu wa viongozi wa dini na mila katika kutokomeza ndoa za utotoni (Na Mpiga picha wetu).

Na Damian Masyenene, Shinyanga 
KATIKA kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na kukomesha matukio ya ndoa za utotoni kwa wasichana wadogo katika mkoa wa Shinyanga, Taasisi ya Msichana Initiative kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa, wadau mbalimbali ikiwemo Agape Aids, Sisema, Kiwohede na UN Women, leo Desemba 3, 2020 wamekutana na viongozi wa dini na kimila kutoka wilaya za Kishapu na Shinyanga kujadili nafasi yao kwenye kumaliza tatizo la ndoa za utotoni. 

Kikao hicho kilifanyika katika hoteli ya Vigimark Mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba na Mwakilishi Mkaazi Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), Hodan Addou. 

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amesema kuwa kila mzazi ana wajibu wa kumlea mtoto wake kwa kuwatunza watoto wa kike, kuwafuatilia na kufahamu mienendo yao, huku akisisitiza kuwa wazazi wasipokuwa makini vitendo vya ngono vitaendelea ndani ya nyumba zao baina ya watoto. 

“Nawaasa wazazi wenzangu tuanze kulinda watoto wetu tangu wakiwa katika umri mdogo, vile vile ni wajibu wa mtoto wa kike kujitunza vile ipasavyo ikiwemo kukwepa vishawishi. Akina baba na watoto wa kiume wakibadilika mtoto wa kike atasoma, wakitambua kwamba mabinti hao ni watoto wao na dada zao basi watoto wa kike watasoma kwahiyo tubadilike ili kujenga taifa imara. 

”Kikao hiki ni fursa pekee kusema yale yote mnayoyafahamu ili kwa pamoja tupate namna bora ya kuhakikisha watoto wetu wa kike wanalelewa na kusimamiwa vizuri wapate nafasi ya kutimiza ndoto zao, kwahiyo muwe huru kila mmoja kutoa mchango wake ili tufanye tathmini ya mila na desturi kandamizi na kuweka mipango sahihi,” amesisitiza. 

Aidha, RC Telack ameeleza kuwa katika jitihada za kuwasaidia watoto wa kike wanaofanya vizuri kimasomo wilayani Kishapu ambao walikuwa waathirika wa ndoa za utotoni, mkoa uliamua kutenga madarasa kwa ajili ya kuwasaidia kimasomo, ambapo jitihada hizo zimeleta matunda chanya, huku akiwaomba wadau ikiwemo shirika la UN Women kusaidia ili kuipanua shule hiyo iweze kuchukua wasichana wengi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa huo. 

Akizungumzia umuhimu wa kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative, Rebecca Gyumi amesisitiza kuwa viongozi wa kidini na kimila ni watu wanaoheshimiwa na kusikilizwa, hivyo kuzungumza nao na kuweka mikakati watakuwa na kitu cha kufanya ambacho viongozi wenzao wa mikoa mingine watapata sehemu ya kujifunza. 

Pia Gyumi amesema kuwa changamoto kubwa ambazo wamekuwa wakikumbana nazo katika kumkomboa mtoto wa kike kutoka kwenye janga la ndoa na mimba za utotoni ni kesi kumalizwa nyumbani (kifamilia) na mwitikio mdogo katika kutekeleza sheria, huku akiwahimiza wadau wote kufanya kazi kwa pamoja kumaliza tatizo hilo. 

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, amesema kuwa kuna hatua zimefanyika katika halmashauri za wilaya hiyo kuokoa watoto ambao walikuwa wanahangamia, ambapo aliahidi wilaya hiyo kuhakikisha wanavikomesha kabisa vitendo hivyo,huku Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba ameeleza kuwa watoto wa kike wakilelewa vizuri wakajitambua watailinda jamii na kwamba wilaya hiyo imepiga hatua katika kukomesha mimba na ndoa za utotoni. 

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Usawa wa kijinsia (UN Women), Hodan Addou amebai nisha kuwa takribani wasichana Milioni 12 duniani huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, huku asilimia 40 wakiwa Africa, ambapo kwa Tanzania asilimia 31 ya wasichana huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na asilimia 5 kabla ya kufikisha umri wa miaka 15, huku akiipongeza Msichana Initiative kwa mchango wao mkubwa wa kupigania haki za wasichana wadogo nchini. 

Addou amesisitiza kuwa ukimya wa viongozi wenye mamlaka umekuwa sababu kubwa ya kuchochea tatizo hilo, hivyo akawaomba viongozi waliohudhuria kikao hicho kuzungumza na kufikia mapendekezo ambayo yatasaidia kuwalinda watoto, huku akibainisha madhara ya ndoa za utotoni kuwa huathiri afya za watoto wa kike, vifo wakati wa kujifungua, kupata magonjwa ikiwemo Virusi Vya Ukimwi (VVU), kunyimwa haki yao ya elimu na kukosa nafasi ya kujiinua kiuchumi. 

Naye Mwakilishi wa Bodi ya Msichana Initiative na Mkurugenzi wa Shirika la WoteSawa, Angela Benedicto akishauri sheria zilizopo kutekelezwa kwa ukali zaidi bila kuoneana huruma kwa watekelezaji wa vitendo hivyo na kwamba elimu iendelee kutolewa kwa makundi hayo kila sehemu. 

Mmoja wa viongozi wa dini waliohudhuria kikao hicho, Sheikh Balilusa Khamis akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, amewaomba wadau wote kushiriki kwa pamoja, kukemea kwa nguvu zote kuufukuza mzimu unaoangamiza ndoto za vizazi vyetu, huku mwakilishi wa viongozi wa kimila, Faustine Sengerema akisisitiza kuwa ili vita hiyo ifanikiwe ni lazima kushirkiana na viongozi kuanzia ngazi ya chini, wasanii na serikali iwashirikishe wadau wote katika vikao vya namna hiyo. 

Naye Msichana ambaye alikuwa muathirika wa vitendo vya ukatili, Elizabeth Nangi ambaye kwa sasa anasoma katika shule ya Agape Knowledge Open School inayosaidia mabinti waathirika wa ukatili, amesema jamii kuchukulia vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vya kawaida na kumalizana kifamilia imekuwa changamoto, ambapo amewaomba viongozi kulivalia njuga.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza kwenye kikao hicho
 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza katika kikao hicho
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akizungumza na washiriki wa kikao hicho
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative, Rebecca Gyumi
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Usawa wa kijinsia (UN Women), Hodan Addou
Mkurugenzi wa shirika la Agape Aids, John Myola
Mjumbe wa Kamati ya amani mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis
Picha ya Pamoja na baadhi ya viongozi wa dini kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga waliohudhuria kikao hicho
Picha ya Pamoja na wajumbe wa kamati ya amani ya mkoa wa Shinyanga waliohudhuria kikao hicho
Picha ya Pamoja na baadhi ya watumishi wa Serikali waliohudhuria kikao hicho
Picha ya pamoja na viongozi wa dini kutoka manispaa ya Shinyanga waliohudhuria kikao hicho

Picha na Mpiga picha wetu






















Post a Comment

0 Comments