Header Ads Widget

WASAJILI WASAIDIZI WA NGOs WAASWA KUZINGATIA MAADILI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na washiriki wakati akifungua Mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora yaliyofanyika jijini Dodoma.

Na Mwandishi wetu, Dodoma
Wasajili wasaidizi wa Mashirikia Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) wametakiwa kuzingatia weledi na misingi ya uzalendo katika utendaji kazi wao huku wakitanguliza maslahi ya taifa mbele.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu, Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa Wasajili wasaidizi kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora pamoja na Wizara zinazosimamia mashirika hayo.

Dkt. Jingu amesema wasajili wa NGOs lazima wazingatie weledi na kufuata taratibu, sheria, kanuni na miongozo katika utendaji kazi wao.

Amesema Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hivyo wasajili wana jukumu la kuhakikisha wanasimamia vizuri kwa kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika kutekeleza shughuli zao nchini na kutanguliza maslahi ya Taifa.

“NGO ni Sekta muhimu katika kila sekta, zinatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, ndiyo maana tupo hapa ni jukumu letu kama Maafisa wa Serikali na waratibu katika maeneo yetu kujipanga kusimamia kwa weledi, kuzingatia maslahi ya Taifa, Kanuni na Sheria zilizopo” amesema Dkt. Jingu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka washiriki kukumbuka kuwa wasajili wasaidizi ni watumishi wa Umma, wanawajibika kwa Serikali na Wananchi hivyo, wahakikishe wanafuata misingi na taratibu za utumishi wa umma.

Ameongeza kuwa watumishi wa umma wanatakiwa kuzingatia maadili kwa kufuata kanuni na sheria mbalimbali zilizowekwa ikiwemo Sheria ya NGOs.

"Ni wajibu na lazima kujituma na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili tuweze kutimiza majukumu yetu" Amesema

Mmoja wa Wasajili wasaidizi waliohudhuria mafunzo hayo, Dominic Joseph amesema walitarajia kujifunza vitu vingi kwani wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali wakiwa wanaratibu NGOs maeneo yao na kuwashukuru makatibu wakuu wa afya na utumishi ambao wamewapitisha kwenye Kanuni na Sheria za kuzingatia kusaidia Watanzania.

“Wametusaidia kutupa shule ya namna ya kutambua umuhimu wa utumishi wetu katika kuhakikisha tunasimamia maslahi ya Taifa na kutanguliza uzalendo tukiwa tunaratibu NGOs, tunashukuru sana kwani wengi hatukuwahi kupata mafunzo kama haya”.

Wizara ya Afya - Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kutoa mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika ngazi za Mikoa na Halmashauri kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza Majukumu yao kutokana na Sheria namba 3 ya mwaka 2019 pamoja na mwongozo wa uratibu wa NGOs wa mwaka 2020.
 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na washiriki wa mafunzo kwa Wasajili Wasaidiizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora yaliyofanyika jijini Dodoma.
 
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya wasajili wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa katika mafunzo hayo

Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga akitoa neno katika mafunzo ya Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyofanyika jijini Dodoma Mwanasheria kutoka Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dennis Bashaka akiwasilisha mada kuhusu dhana ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Mafunzo ya Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wa Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Post a Comment

0 Comments