Header Ads Widget

MATUKIO 91 YA UBAKAJI YARIPOTIWA KISHAPU, 9 WAFUNGWA, DC TALABA AONYA

Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Kishapu wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali wakati wa maandamano ya kupinga ukatili yaliyoandaliwa na Dawati la jinsia la jeshi la polisi wilayani humo.

Na Malaki Philipo, Kishapu
Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, wamefanya maandamano ya amani kwa kupita katika mitaa mbalimbali ndani ya Halmashauri ya wilaya hiyo wakiwa na mabango yenye jumbe tofauti za kuhamasisha kupinga ukatili wilayani humo.

Maandamano hayo yalifanyika jana Desemba 4, 2020, ambapo Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wamekutana na kufanya maandamano kuanzia eneo la Mto Tungu hadi shule ya Sekondari Kishapu,  ikiwa ni nyenzo mojawapo katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Miongoni mwa wadau walioshiriki maandamano hayo ni Shirika lisilo la Kiserikali la Redeso, NMB, Red Cross, TCRS na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ambao kwa pamoja wamehimiza jamii kuacha ukatili kutokana na kusababisha madhara makubwa kiafya, kiuchumi, kimwili na hata kisaikolojia na kusema kwamba vitendo, hivyo vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo hivyo basi jamii haina budi kuachana navyo.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Kishapu, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Rose Mbwambo amesema maandamano hayo yanaakisi umakini wa dawati hilo katika kutoa elimu ya haki na uwajibikaji ili kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwamba dawati hilo limekuwa likifanyakazi kwa weledi, ambapo kwa mwaka huu jumla ya wanaume tisa wamefungwa kifungo cha miaka 30 kila mmoja.

“Ukitazama Takwimu za Januari hadi Novemba, 2020 tumepata taarifa 91 za ubakaji, kati ya hizo taarifa watu 43 wamefikishwa mahakamani na tayari wanaume tisa wamefungwa miaka 30 kila Mmoja, changamoto iliyopo ni ufichwaji wa mashahidi na kufanya mapatano ya kfiamilia kumaliza kesi za namna hiyo lakini dawati linaendelea kuchukua hatua za kisheriia kwa wanaobainika na makosa hayo” Amesema Rose.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba ambaye aliyapokea maandamano hayo amesema msimamo wa Serikali ni kuhakikisha hali ya usawa, utulivu na amani katika kuvikabili vitendo vyote vinavyokiuka haki na utu wa mtu, na kuitaka jamii kuacha imani za kishirikina, imani zinazowaweka watoto kwenye hatari ya kubakwa na kundi la wazee katika hatari ya mauaji.

“Wilaya ya Kishapu si kwamba imeharibiwa na mila na desturi lakini uelewa wa baadhi ya wazazi kutambua mchango wa mtoto hasa wa kike kwenye maendeleo lakini imani za kishirikina zimekuwa mwiba unaowatia hofu ya kubakwa kwa watoto ama kulawitiwa lakini pia wazee kuingiwa ha hofu ya kuuawa,” amesema Talaba

“Lakini Serikali Kwa Kushirikiana Na Wadau Mbalimbali Wa maendeleo tutaendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili na kuhakikisha tunachukua hatua kali za kisheria kwa wale wanaoendelea na vitendo hivyo kwa sababu zao, hatutawafumbia macho,” ameongeza Talaba.

Maandamano ya Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu yametamatishwa na ugawaji wa taulo za kike, madaftari, kalamu pamoja na michezo mbalimbali ukiwemo mpira wa Pete kati ya askari Polisi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kishapu.

TAZAMA PICHA CHINI

Maandamano ya dawati la jinsia wilaya ya kishapu kupinga ukatili wa kijinsia
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu, Rose Mbwambo wakati akieleza mikakati ya dawati hilo, baada ya maandamano katika shule ya Sekondari Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba (kushoto) akimpatia mwanafunzi daftari na taulo za kike wakati wa maadhimisho hayo
Mama akipokea taulo za kike na vifaa mbalimbali kwa niaba ya mwanae
Zoezi la kugawa taulo la kike kwa wanafunzi likiendelea

DC Talaba na wageni mbalimbali wakifuatilia shughuli mbalimbali zilizokuwa zinaendelea wakati wa maadhimisho hayo
Bango lililobeba ujumbe wa jeshi la polisi Kitengo cha Dawatik la jinsia wilaya ya Kishapu
Timu za mpira wa pete za Jeshi la Polisi na Sekondari ya Kishapu zikiwa tayari kwa ajili ya mchezo wakati wa maadhimisho hayo
Wachezaji wa timu hizo wakichuana uwanjani wakati wa mchezo huo
TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807