Header Ads Widget

HALMASHAURI YA USHETU YAONGEZA MAPATO KWA ASILIMIA 62 BAADA YA KUSITISHA MIKATABA YA WAZABUNI

Mkurugenzi wa Halmasuari ya Ushetu, Michael Matomora akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Halmashauri hiyo kwa Baraza jipya la Madiwani ambalo limezinduliwa rasmi kwaajili ya kuanza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

Na Salvatory Ntandu -Ushetu
Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeongeza Mapato kwa asilimia 62 katika vyanzo vya Mapato ya ndani ambavyo hapo awali vilikuwa vinasuasua baada ya kusitisha mikataba na mawakala wa ukusanyaji wa mapato na kuamua kuwatumia watumishi ambapo hadi sasa wamekusanya zaidi ya Sh Milioni 300 kwa kipindi cha miezi minne.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Michael Matomora wakati akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Halmashauri hiyo kwa baraza jipya la madiwani ambalo limezinduliwa rasmi kwaajili ya kuanza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

Alisema kuwa Kamati ya Maendeleo ya Halmashauri hiyo ililazimika kusitisha mikataba na Mawakala wa Ukusanyaji wa Mapato ya ndani katika Minada na Mageti kwa kipindi cha miezi mine na kuwatumia Watumishi wake ampao mpaka sasa wamefanikiwa kuongeza mapato kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na hapo awali.

“Katika Mnada wa uyogo Mawakala awali walikuwanakusanya Sh Milioni 15.2 baada ya kusimamia Halmashauri kwa sasa tunakusanya Sh Milioni 27,Mnada wa Chona awali zilikuwa zinakusanywa shilingi milioni 10.6 kwa sasa ni Sh Milioni 11.6,Mnada wa Bugomba awali Sh Milioni 3.9 hadi Sh Miloni 9.1,”alisema Matomora.

Alifafanua kuwa katika Mageti mapato yameongezeka kwa kiwango kikubwa ambapo katika Geti la Kisuke awali walikuwa wanakusanya shilingi milioni 7.4 hadi kufikia milioni 44, geti la Iboja awali laki 1 na elfu 15 hadi milioni 11.9 geti igunda awali milioni 6.5. hadi milioni 39.5, geti la Mzenga shilingi million 36 ,geti la Igalula milioni 64.2 Geti la mpunde awali milioni 6.5 hadi milioni 24.7 Geti la Mwabomba milioni12.5.

Doa Limbu ni Diwani wa Kata ya Nyakende na Pili Sonje Kata ya Ushetu wakati wakitoa maoni yao baada ya Taarifa hiyo kuwasilishwa wameipongeza Kamati ya wataalamu wa Halmashauri hiyo kwa kazi kubwa ya kudhibiti ukwepaji wa mapato katika vyanzo hivyo ambavyo hapa awali vilikuwa havikusani vizuri sambamba na kushauri kubuniwa kwa vyanzo vipya vya mapato.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika Kikao hicho cha Madiwani aliwaomba madiwani hao kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakika Ushetu inasonga mbele katika sekta ya Maendeleo sambamba na kwenda kutatua kero za wananchi waliowachagua katika uchaguzi uliopita.

Madiwani hao pia wamemchagua Gagi Lala Gagi Diwani kata ya Igwamanoni kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo huku Emanuel Makasi Diwani wa kata ya Sabasabini kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Timothy Ndanya akimkabidhi Cheti cha Ushindi Diwani wa kata ya Igunda Tabu Katoto kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Michael Matomora.


TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807