Header Ads Widget

RC GEITA AZINDUA MAONESHO YA MADINI SHINYANGA, AWATAKA WAWEKEZAJI KUACHA MAZOEA YA KUJENGA CHOO NA DARASA


Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel (kulia) akipata ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa Afisa Madini mkoa wa Shinyanga, Joseph Kumburu (kushoto) katika banda la Tume ya Madini wakati wa maonesho ya biashara na teknolojia ya madini kwenye uwanja wa Butulwa Old Shinyanga mjini Shinyanga.

Na Damian Masyenene –Shinyanga
MKOA wa Shinyanga umezindua rasmi maonesho yake ya kwanza ya biashara na teknolojia ya madini pamoja na kuzindua mwongozo wa uwekezaji ulioainisha fursa zote za uwekezaji katika mkoa huo.

Uzinduzi wa maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu ya ‘Biashara ni chachu ya maendeleo ya Shinyanga’ umefanyika leo Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa maonesho wa Butulwa Kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga, huku mgeni rasmi wa maonesho hayo ambayo kilele chake kitakuwa Desemba 1, mwaka huu alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel.

Akizungumza wakati wa kukagua mabanda na kuzindua maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ameupongeza mkoa huo kwa kufanya maonesho hayo kwa mara ya kwanza, huku akibainisha kwamba ni maonesho ya kipekee na ya kihistoria katika mkoa huo wa madini kwani yana manufaa kwa wananchi wote kwakuwa yamekusudia kuleta mapinduzi kiuchumi na yatakuwa shule kwa wachimbaji wadogo.

Mhandisi Gabriel amezitaja fursa zitakazopatikana kuwa ni wafanyabiashara kujua masoko yaliyopo ya madini na kuwarahisishia uuzaji, kujua mahitaji halisi ya wateja, fursa ya kuwekeza, nafasi ya kujifunza teknolojia mpya katika uzalishaji na kuongeza thamani katika mnyororo wa sekta ya madini.

“Tunataka tuone mkufu wa Almasi unatoka Shinyanga na hili linawezekana, tuanzishe utaratibu wa utengenezaji bidhaa za Mwisho zitokanazo na madini yetu na hii ni fursa kwa masonara kutengeneza bidhaa zitakazokutana na walaji, tunataka Shinyanga ibadilike kwa mwendo wa kasi.

“Kampuni kubwa zitumie fursa hiyo kuwekeza katika eneo hili la maonesho kwa kujenga kumbi, miundombinu, sehemu za burudani kwa watoto na watu wazima, maeneo ya wajasiriamali......huu siyo tena wakati wa kampuni kubwa za madini kujenga choo na darasa kwenye jamii, tutoke huko tupige hatua tujenge vitu vitakavyoacha alama,” amesisitiza.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amesema kupitia maonesho hayo, wajasiriamali na wachimbaji wadogo wamepata fursa na eneo la kuonesha bidhaa zao na kuchambua fursa ya soko, huku ikiwa ni fursa kwa wazalishaji kuonesha bidhaa zao na wafanyabiashara wa ndani na nje wakiongeza masoko.

RC Telack amebainisha kwamba wanatarajia eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 65 kuwa endelevu kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji kwani sasa maonesho hayo yatafanyika kila mwaka mwezi Julai na litatumika kwa shughuli zingine ikiwemo maonesho ya Kilimo (Nane Nane) na mengine ya kitaifa na kimkoa.

“Tunatamani kuona mageuzi makubwa ya kiuchumi katika mkoa wetu kwa mfano tangu Julai mwaka huu tumeuza Almasi yenye thamani ya Sh Bilioni 42.5, ninaomba wafanyabiashara wote wa madini waache kuukimbia mkoa wao bali wawekeze nyumbani, wengine wanasema hawawezi kuwekeza hapa kwasababu hakuna biashara, Lakini biashara inaletwa na watu kwahiyo wawekeze viwanja vipo na mji utakua kwasababu ya uwekezaji,” amesisitiza.

Awali akitoa taarifa ya maonesho hayo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi amesema kuwa maonesho hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2017 na kubaini kuwa mji huo umeiva na unahitaji maonesho yatakayowakutanisha wafanyabiashara na kuonesha fursa mbalimbali.

Amesema Manispaa hiyo inavyo viwanda vikubwa na vya kati 29 na vidogo 127 na kwamba wapo wazalishaji wa vifungashio Lakini wafanyabiashara wamekuwa wakiagiza nje kutokana na kutokuwa na uelewa, hivyo wakaona haja ya kuwa na maonesho ya biashara ili kuwaleta pamoja na wazalishaji kutoa suluhu chanya ya changamoto ya mzunguko wa fedha.

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi (CCM), akaweka wazi kuwa lazima wafanya kazi kubwa ili mkoa wa Shinyanga uwe na kitu ama jambo la kujivunia, kuutambulisha na kuufanya uheshime na kupitia mwongozo wa uwekezaji utasaidia kukaribisha wawekezaji, huku akimuahidi RC Gabriel kwamba maonesho hayo yatakua makubwa na kuzidi yale ya Mkoani Geita.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji wadogo wa Madini Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Gregory Kigusi akieleza kuwa ni jambo zuri kwa wachimbaji na wadau wote wa madini kukutanishwa pamoja ili kubadilishana ujuzi na teknolojia, pia kukutana na taasisi nyingine ikiwemo za fedha kuona namna ya kupata mikopo.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabaishara wenye Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga, Kulwa Meshack akieleza kuwa watautumia mwongozo wa uwekezaji wa mkoa huo uliozinduliwa na kuhakikisha wanautangaza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje. 

Uwanja huo wa maonesho utatambulika kwa jina la uwanja wa Zainab Telack baada ya mapendekezo yaliyowasilishwa na waandaaji wa maonesho hayo kupitia kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi kukubaliwa na mgeni rasmi, Mhandisi Robert Gabriel.
Mhandisi Robert Gabriel akiwasili uwanjani hapo na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (katikati) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (Kulia).
Mhandisi Robert Gabriel akisalimiana na Mstahiki Meya mteule wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila na kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Mgeni rasmi wa maonesho hayo, Mhandisi Robert Gabriel akisalimiana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba baada ya kuwasili uwanjani hapo



Mhandisi Robert Gabriel akisalimiana na Mlimbwende (Miss) wa Utalii mkoa wa Shinyanga



Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel (katikati aliyevaa miwani) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa maonesho ya kwanza ya biashara na teknolojia ya madini katika mkoa wa Shinyanga leo kwenye uwanja wa Butulwa kata ya Old Shinyanga. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi na anayefuata ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko

Afisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Joseph Kumburu (kulia) akitoa maelezo kwa viongozi juu ya kazi za Tume ya Madini wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya biashara na teknolojia ya madini mkoa wa Shinyanga
Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji madini wadogo mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Gregory Kigusi (aliyeshika kipaza sauti) akitoa maelezo kuhusu utendaji kazi wa chama hicho mbele ya viongozi mbalimbali waliofika kwenye banda hilo.
Mhandisi Robert Gabriel akikagua banda la Mgodi wa Williamson Diamond
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akitoa maelezo ya kazi zinazofanywa na kitengo cha Dawati la Jinsia, mbele ya mgeni rasmi wa maonesho hayo, Mhandisi Robert Gabriel
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi (CCM) akiwapongeza wafanyakazi wa Chama cha Wachimbaji wadogo mkoa wa Shinyanga (SHIREMA)
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi wakizungumza na baadhi ya wafanyakazi walipotembelea mabanda mbalimbali kwenye maonesho hayo
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa akipata maelezo kutoka kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenye maonesho hayo
Mjasiriamali Abubakar Kondo anayemiliki vifaa vya kupima upatikanaji wa madini kwa teknolojia ya kisasa, akitoa maelezo kwa Mhandisi Robert Gabriel namna vifaa hivyo vinavyofanya kazi
Mhandisi Robert Gabriel akipata maelezo namna mgodi wa Mwadui unavyootesha miti kwa ajili ya kuigawa kwa wananchi wapande kwa ajili ya utunzaji mazingira
Viongozi wakiendelea na ukaguzi wa vibanda katika maonesho hayo
Mhandisi Robert Gabriel akizungumza na wananchi baada ya kufanya ukaguzi wa vibanda katika maonesho hayo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza katika maonesho hayo ambapo alisisitiza wawekezaji wa mkoani humo kutouelekeza mkoa wao na kukimbilia mikoa mingine huku wakiuacha ukitaabika
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi akitoa taarifa ya maonesho hayo ambayo kwa sehemu kubwa yameasisiwa na halmashauri ya manispaa hiyo
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia maonesho hayo ya kwanza ya biashara na teknolojia ya madini mkoa wa Shinyanga kwenye uwanja wa Butulwa kata ya Old Shinyanga
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar Gulam akitoa neno la chama kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga, Meshack Kulwa akitoa neno kwa niaba ya wafanyabiashara
Awali, RC Telack akiwasili uwanjani hapo
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (katikati) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko pamoja na Katibu Tawala wa mkoa huo, Albert Msovela (kushoto) wakifanya ukaguzi wa mabanda kabla ya kuwasili mgeni rasmi uwanjani hapo
RC Telack akisalimiana na Mbunge, Patrobas Katambi walipokutana kwenye maonesho hayo
Kwaya ya AIC Shinyanga ikitumbuiza kwenye maonesho hayo
DC Mboneko na Afisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Joseph Kumburu wakiburudika pamoja na wanakwaya wa AIC Shinyanga katika maonesho hayo
Mbunge Katambi, Elias Kwandikwa na Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela wakiburudika pamoja na kwaya ya AIC Shinyanga
Baadhi ya bidhaa za madini zilizoletwa kwenye maonesho hayo

Mitambo ya kuosha mchanga inayomilikiwa na Wachimbaji wadogo ilikuwa ni sehemu ya kivutio kwenye maonesho hayo 
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA) ilikuwa ni sehemu ya wadau walijitokeza kwenye maonesho hayo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba (aliyevaa kofia) naye alijitokeza kushuhudia ufunguzi wa maonesho hayo, anayemfuata kulia ni Mkurugenzi wa SHUWASA, Flaviana Kifizi.
Wadau mbalimbali waliojitokeza kwenye maonesho hayo

Wananchi wakiendelea kufuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yakijili uwanjani hapo


Wananchi wakifuatilia maonesho hayo
Wananchi wakiendelea kushuhudia shughuli mbalimbali katika maonesho hayo


Wananchi waliojitokeza kwenye uwanja wa Butulwa Old Shinyanga wakishuhudia mambo mbalimbali kwenye maonesho hayo.
Picha na Marco Maduhu

Post a Comment

0 Comments