Header Ads Widget

MAWAKALA WA CHADEMA WALIOFARIKI RUKWA WAFIKIA 6


MAWAKALA wa Chadema waliopoteza maisha katika ajali ya gari wamefikia sita. Majeruhi wawili wanaendelea kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.

Ajali hiyo ilitokea Jumatano na ilihusisha gari aina ya Noah lililokuwa likisafirisha mawakala tisa wa Chadema, kwenda kula kiapo cha uchaguzi mkuu katika Kijiji cha Sandulula Jimbo la Kwela.

 Gari hilo liliacha njia na kupinduka mara kadhaa katika Kijiji cha Malonje Manispaa ya Sumbawanga.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Rukwa,Dk John Lawi alieleza kuwa awali walipokea miili ya marehemu watatu na majeruhi watano walilazwa kwenye chumba maalumu (ICU) kwa matibabu.

“Lakini baadae watatu walipoteza maisha wakiwa wanapatiwa matibabu, kwa sasa wamebakia majeruhi wawili, mwanamke na mwanaume wakiendelea na matibabu” alisema Dk Lawi.

Alisema marehemu watatu wametambuliwa majina yao na watatu wengine bado hawajatambuliwa. Alitaja waliotambuliwa ni James Karim (29) mkazi wa Kizwite Manispaa ya Sumbawanga, Lemi Nyamuva (45) mkazi wa Bangwe na Lucy Magazine (40) mkazi wa Edeni Manispaa ya Sumbawanga.

Alisema wote watatu walifariki dunia wakitibiwa hospitalini hapo. Marehemu ambao hawajatambuliwa mpaka sasa ni watatu. Hao walipoteza maisha katika eneo ilipotokea ajali hiyo.

Dk Lawi aliwataja majeruhi kuwa ni Emanuel Mwakaunga (50), mkazi wa Mlowo mkoani Songwe ambaye amelazwa wodi namba tatu. Mwingine ni Galus Pesambili (32) mkazi wa Bangwe Manispaa ya Sumbawanga.

“Ajira Nwandola (30) ambaye ni mkazi wa mji mdogo wa Tunduma mkoani Songwe alitibiwa na kuruhusiwa”
alieleza. 

Alisema miili hiyo ya marehemu sita imehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali hapo, ikisubiri kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya maziko yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masonje alisema ajali hiyo ilitokea Jumatano saa mbili asubuhi katika barabara ya Sumbawanga -Mkima katika Kijiji cha Malonje.

CHANZO: Habari Leo 

Post a Comment

0 Comments