Header Ads Widget

MAALIM SEIF AMPONDA MEMBE, ASIKITISHWA KUTOONEKANA MAJUKWAANI



MGOMBEA urais wa chama cha ACT Wazalendo visiwani Zanzibar ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ameeleza kusikitishwa kwake na tamko la jana la mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Bernard Membe, kuwa yeye ni mgombea halali wa urais, hivyo ataipeperusha bendera ya chama na ana uhakika atashinda.

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne, Oktoba 20, 2020, jijini Dar es Salaam, amesema ACT-Wazalendo kupitia mkutano mkuu wa taifa walisema wanataka mabadiliko nchini ambapo mkutano huo ulibariki kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ili kuiondoa CCM madarakani.

“Membe alipokuja tulimwambia uamuzi wa mkutano mkuu ni tushirikiane na vyama vingine. Tukamuuliza tukiamua kushirikiana utakubali? Akasema ‘Naam.’ Tulipoona kampeni zetu zimesuasua, tukaamua, na Membe akiwepo, tumuunge mkono Tundu Lissu.

“Mgombea wetu (Bernard Membe) haonekani. Ni afadhali mzee wa ubwabwa (Hashim Rungwe) anaonekana. Kamati ya uongozi kwa kauli moja pamoja na Membe tulikubaliana tumuunge mkono Tundu Lissu. Siyo kwamba hatumpendi Membe.

“Alilosema Zitto Kabwe si lake! Nililosema mimi Maalim Seif si langu! Bali ni maamuzi ya chama. Ni msimamo wa ACT Wazalendo anayekaribia kumshinda Magufuli ni Tundu Lissu na huyo ndiye tunamsapoti. Mimi nam-challenge, afanye hizo kampeni zake tuone hizo kampeni ziko wapi. Nia yake ni kutaka kuwachanganya Watanzania.

”Zimebaki siku saba kwa wananchi kufanya maamuzi ya kuwachagua viongozi wanaowataka wao. Tunaelekea katika uchaguzi mkuu wakati wagombea wetu kadhaa wameenguliwa katika kinyang’anyiro hicho lakini tukafanye maamuzi.

“Nyakati zote mimi nilikuwa nawazuia watu wasiingie barabarani! Sasa mwaka huu simzuii mtu. Yeyote atakayeamua kufanya lolote afanye hiyo tarehe 27 na 28. Wazanzibar wamepanga kulinda demokrasia kwa gharama yoyote! Wamevuta subira kwa muda mrefu. Sasa imetosha!” amesema Maalim.

Post a Comment

0 Comments