Header Ads Widget

CHAMA ASEMA SIMBA KUNA RAHA, AAHIDI KUSAINI MKATABA MPYA

Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama amewatoa wasiwasi mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kwa kuwaahidi kuwa atasaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea siku chache zijazo.

Mkataba wa sasa wa Chama na Simba utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu na kumekuwa na wasiwasi kuwa kiungo huyo raia wa Zambia ataachana na klabu hiyo lakini ameamua kuzima tetesi hizo na kusema kuwa ataendelea kubakia Simba.

Chama amefichua hayo jana kupitia majibu aliyokuwa akiyatoa katika ukurasa wake wa Instagram ambapo aliwapa nafasi mashabiki wa  soka kumuuliza maswali ambayo alikuwa akiyajibu.

"Fresh kaka vipi? Bado bro nategemea ndani ya muda mfupi mambo yatakuwa mazuri," Chama alimjibu shabiki mmoja aliyetaka kufahamu kwamba ameshasaini mkataba mpya au bado.

Chama pia alimjibu shabiki mwingine kuwa yuko tayari kusaini mkataba mpya wa Simba 

Lakini jibu la Chama kwa shabiki wa Yanga aliyemuomba ajiunge na timu hiyo ndio huenda likawapa matumaini makubwa Simba ya kuendelea kufaidi huduma ya kiungo huyo mshambuliaji.

"Asante sana lakini hapa Simba pana raha zaidi. Tamu eeh," alijibu Chama.

Chama amekuwa mchezaji tegemeo wa Simba na pia kipenzi; cha mashabiki wa timu hiyo na wa soka nchini kutokana na kiwango cha juu na mchango mkubwa anaoutoa kwa timu yake tangu alipojiunga nayo mwaka 2018.

Katika msimu wa 2018/2019, Chama alitoa mchango mkubwa kuiwezesha Simba kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiifungia jumla ya mabao matano katika mashindano hayo huku pia akiisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huo.

Msimu uliopita aliiongoza kutwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu, taji la Kombe la Shirikisho la Azam huku pia akiweza kuibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ambayo alipiga pasi 12 zilizozaa mabao

Katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu, Chama ameifungia Simba mabao mawili na kupika mabao matatu.

Post a Comment

0 Comments