Header Ads Widget

WAJASIRIAMALI PEMBA WATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU KUPANUA SOKO LA BIDHAA ZAO

Baadhi ya wajasiriamali wanawake kisiwani Pemba wakiendelea na mafunzo katika mkutano wa kamati ya biashara kwa ajili ya kubadilishana mawazo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar.

Na Gaspary Charles- TAMWA
WAJASIRIAMALI kisiwani Pemba wametakiwa kuongeza ubunifu wa kazi zao kwaajili ya kujitangaza na kuongeza wigo wa uuzaji wa bidhaa wanazozalisha ili kuendelea kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika mkutano wa kamati ya biashara kwaajili ya kubadilishana mawazo kwa wajasiriamali ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, mwezeshaji wa mkutano huo, Hamad Hassan Chande amesema ili bidhaa ya mjasiriamali
iweze kupendwa ni lazima iongezewe ubunifu.
Mwezeshaji wa mkutano huo, Hamad Hassan Chande akizungumza na washiriki (hawapo pichani). 

Chande amewahimiza wajasiriamali hao kuacha kuogopa kukabiliana na changamoto za kibiashara na badala yake watumie changamoto hizo kama silaha ya kubuni njia mpya ya uendelezaji wa shughuli zao.

Alisema, “ujasiri na uthubutu kwa mjasiriamali katika kuchukua maamuzi magumu ya kukabiliana na changamoto katika utekelezaji wa shughuli zake ndiyo sifa kuu na muhimu kwa mjasiriamali hivyo tusiogope kukabiuliana na changamoto kwani siku zote mjasiriamali anahitaji changamoto zaidi ili kukuza ubunifu wake,”.

Katika hatua nyingine mwezeshaji huyo aliwataka wajasiriamali hao kuweka nguvu zaidi katika matumizi ya mitandao ili kuongeza wigo wa soko kupitia mitandao hiyo.

“Tuchangamkie fursa iliyopo kwenye mitandao ya kijamii kwani mitandao ndio sehemu kuu kwa sasa ambayo mtu unaweza kuuza bidhaa zake kwa haraka na kuwafikia wateja wengi zaidi kwa wakati mmoja” alisema.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Fatma Moh’d Juma, alishukuru TAMWA Zanzibar kwa kuwezesha kutolewa kwa mafunzo hayo na kuahidi kuanza kutumia mitandao ya kijamii kutangaza bishara yake ili engo lake la
kujiinua kiuchumi lieweze kufanikiwa kwa urahisi.

“Niwashukuru sana TAMWA Zanzibar kwa nafasi hii ya leo nimejifunza mengi sana kupitia mafunzo haya na sasa nimetoka na wazo la kuanza kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii ili kazi zangu ziwafikie wengi zaidi
duniani,” alisema.

Kwa upande wake, Salama Omar Salum, alisema mafunzo hayo yamewawezesha kupata mbinu mpya za kujasiriamali na kuachana na dhana ya kufanya kazo zao kwa mazoea jambo linalopelekea kushindwa kukidhi mahitaji kamili ya
soko.

Alisema, “Kupitia mkutano huu tumejifunza umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora hitajika na kuacha kutengeneza bidhaa zetu kwa mazoea kwani kufanya hivyo kumekuwa kukitupunguzia imani ya wateja dhidi ya
biashara zetu,”

Mapema afisa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi TAMWA ofisi ya Pemba, Asha Mussa Omar alisema chama kupitia mradi huo kinaendelea na juhudi za kuhakikisha wanawake Zanzibar wanajikwamua kiuchumi kupitia
shughuli mbalimbali za ujasiriamali.