Header Ads Widget

KWANDIKWA AZINDUA KAMPENI USHETU KUWAOMBEA KURA MADIWANI NA RAIS MAGUFULI

Vijana wa kikundi cha Amsha Amsha cha Jimbo la Kahama Mjini wakisherehesha katika uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Ushetu.

Na Salvatory Ntandu, Ushetu
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ushetu wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Elias John Kwandikwa ambaye tayari amekwishatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa amepita bila kupingwa amewaomba wananchi wa jimbo hilo kumpigia kura, Rais Dk John Pombe Magufuli na wagombea udiwani wa chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Ombi hilo amelitoa jana katika kkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za ubunge wa jimbo hilo uliofanyika katika uwanja wa Magufuli kata ya Bulungwa halmashauri ya Ushetu, uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hizo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa.

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli imetatua kero mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wananchi wa jimbo hilo kama vile miundombinu ya barabra,afya,elimu, umeme na maji ambazo awali zilikuwa zinasababisha washindwe kufanya shughuli za maendeleo.

“Rais Magufuli katika jimbo hili ametutendea haki kwa mfano katika sekta ya afya ametoa zaidi ya shilingi bilioni mbili katika ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Ushetu,Ujenzi na ukarabati wa vituo vyetu mbalimbali vya afya,gari la wagonjwa katika kituo cha afya Ushetu ambavyo vyote vinalenga kuboresha afya za wanachi wetu,” alisema Kwandikwa.

Alifafanua kuwa katika sekta ya elimu katika jimbo hilo zaidi ya Sh Bilioni 2 zimetolewa katika elimu ya msingi na sekondari kupitia mfumo wa elimu bure unaotekelezwa na serikali, pia ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na mabweni katika shule za sekondari mbalimbali katika jimbo hilo.

“Tumejenga Mabweni ya wasichana katika shule za sekondari mbalimbali katika jimbo letu kama vile Ulowa, Sabasabini na Dakama ambayo yatawasaidia wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu, kupanga katika nyumba za watu ambazo husababisha wengi wao kurubuniwa na wanaume ili kuwasaidia kutimza malengo yao,” alisema Kwandikwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa (CCM) mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, wakati akimnadi Eliasi John Kwandikwa amewaomba wananchi wa Jimbo hilo kuwachagua wagombea wote wa chama hicho kuanzia ngazi ya Raisi, Wabunge na Madiwani katika uchaguzi mkuu ili waendelee kuwaletea wananchi maendeleoa na kukuza uchumi wa Taifa.

“Katika Ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2010-2015 tuliahidi na tumetekeleza miradi mbalimbali mikubwa ya kitaifa ya maendeleo kama vile ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa Reli ya kisasa ya (SGR) ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme Rufiji, usambazi wa nishati ya umeme vijijini kupitia mradi wa REA na uanzishwaji wa viwanda vikubwa na vya kati,” alisema Mlolwa.

Amewataka wananchi kuendelea kuiamini na kuipigia kura CCM ili kundelea kuwatumikia kwa miaka mingine mitano ambapo kupitia ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 imezingatia vipaumbele vya wananchi katika maeneo yote ya mijini na vijijini katika kukuza uchumi na ustawi wao.

Katika mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni katika jimbo hilo umehudhuriwa na wagombea ubunge wa Jimbo la Msalala (CCM) Idd Kasimu Idd, Jimbo la Kahama Mjini Jumanne Kishimba na Wagombea wa ubunge wa Mkoa wa Shinyanga na baadhi ya madiwani wa majimbo hayo matatu, pamoja na kamati za siasa za chama hizo za Wilaya na Mkoa.
 Vijana wa Amsha Amsha wa Chama Cha mapinduzi (CCM) Kahama Mjini wakiusindikiza Msafara wa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ushetu Elias John Kwandikwa kuingia katika Uwanja wa Magufuli Bulungwa kwaajili ya uzinduzi wa Kampeni.
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara wa Uzinduzi wa Ubunge wa Jimbo la Ushetu kuwaomba kura za kuwachagua wagombea wa chama hicho kwa ngazi za Urais,Ubunge na Udiwani.
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akimtambulisha Mgombea Ubunge jimbo la Msalala Iddi Kasimu Iddi katika Uzinduzi wa kampeni Jimbo la Ushetu.
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akimtambulisha Mgombea Ubunge Jimbo la Kahama Mjini Jumanne Kibera Kishimba katika Uzinduzi wa kampeni Jimbo la Ushetu.
 Mgombea Ubunge wa (CCM) mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika Uzinduzi wa kampeni Jimbo la Ushetu jana kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa.
 Mgombea Ubunge wa (CCM) mkoa wa Shinyanga Dk Christina Mzava akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika Uzinduzi wa kampeni Jimbo la Ushetu jana kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa.
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, akimtambulisha mgombea Ubunge wa (CCM) mkoa wa Shinyanga Santiel Kirumba katika Uzinduzi wa kampeni Jimbo la Ushetu.
Baadhi ya Wagombea Ubunge wa CCM wa Majimbo ya Msalala,Ushetu na Kahama Mjini Wakicheza nyimbo za asili katika Ufunguzi wa sherehe za Uzinduzi wa Kampeni jimbo la Ushetu.