Header Ads Widget

KATIBU MTENDAJI TUME YA MADINI AKUTANA NA WADAU KUSIKILIZA NA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO


Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya leo tarehe 10 Septemba, 2020 amekutana na wadau wa madini jijini Dodoma kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali.

Wadau waliohudhuria kikao chake ni pamoja ja wawakilishi kutoka Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki na Wizara ya Madini.

Akizungumza kupita mahojiano maalum Profesa Manya amesema kuwa, kikao hicho kitaipa Tume ya Madini picha ya changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini kwenye usimamizi na ukusanyaji wa kodi mbalimbali ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Uchumi wa Nchi.

"Kama Tume ya Madini tumejipanga katika kuhakikisha Sekta ya Madini inaongeza mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi," amesema Profesa Manya.

Akielezea mikakati ya kuwawezesha wachimbaji wadogo amesema kuwa Serikali inahamasisha wachimbaji wadogo kuunda vikundi ili kupatiwa leseni za madini na kuomba mikopo kwenye benki mbalimbali nchini.

Aidha, Profesa Manya amewataka wachimbaji wa madini nchini kuendesha shughuli zao kwa kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.