Header Ads Widget

BARAZA LA MAASKOFU LAWAHIMIZA WAGOMBEA NA WAFUASI WAO KUHESHIMU POLISI NA NEC


Padri Charles Kitima


KATIBU Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima amewahimiza wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na wafuasi wao, kuheshimu na kutoingilia wala kujaribu kuvuruga majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi.

Aidha, ameitaka NEC na Polisi kuendelea kuzingatia uadilifu na weledi kwa kuhakikisha wanatenda haki zaidi kwa vyama vyote vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa rais, wabunge na madiwani.

Alisema hayo Dar es Salaam juzi alipozungumza na wanahabari katika Siku ya Amani Duniani inayoadhimishwa Septemba 21 kila mwaka na kusisitiza kuwa, vyama vya siasa na wafuasi wao wakizingatia miiko na maadili ya uchaguzi, huku NEC na vyombo vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Polisi wakitenda haki, amani iliyopo nchini itazidi kuimarika.

Tunaposisitiza amani, tunamaanisha kabla ya uchaguzi yaani sasa kampeni zinapoendelea, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi na ndiyo maana tunawapongeza polisi kwa kuonesha na kusimamia utulivu maana hatujaona matumizi ya nguvu kupitia kiasi katika kipindi hiki cha kampeni na pia, hatujaona mihemuko.

Alisema walezi wa amani na wasimamizi hao wa sheria wameonesha mfano kwa kutenda haki pande zote kwa kuhakikisha kuna ulinzi na usalama wa kutosha katika maeneo mbalimbali ya mchakato wa uchaguzi.

Polisi safari hii wameonesha waziwazi kuwa hawana upande wowote wanaoegemea ndiyo maana unaona kila sehemu hakuna msuguano; tunaona kampeni za utulivu zinaendelea. Hili ndilo tunalolitaka Watanzania liendelee hadi wakati wa kupiga kura, kutangaza matokeo na kuwaapisha waliochaguliwa

Akisisitiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuzingatia uadilifu, Dk Kitima alisema

Tume ni kama refa wa Yanga na Simba, lazima iendelee kutenda haki kwa timu zote na iheshimiwe na wadau wote

Alisema miongoni mwa mambo yanayopaswa kufanyika ili kudumisha amani inayosisitizwa na Kanisa Katoliki na dini nyingine, ni pamoja na kupendana na kuheshimiana, kila mmoja kuheshimu haki ya mwingine, kutimiza wajibu wake na kuzingatia kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo.


Kwa mujibu wa Kitima, inapotokea kiongozi wa dini akakengeuka na kufanya au kusema mambo yasiyopaswa hasa akiwa mgombea, ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria kama mgombea na siyo kama kiongozi wa dini maana pale yeye ni mgombea kama wagombea wengine.

Post a Comment

0 Comments