Header Ads Widget

BABU ATUPWA JELA MIAKA 30 KWA KUMNAJISI BINTI WA MIAKA 10


MKAZI wa kijiji cha Ulumi A katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa Medadi Chitenzi (60) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukiri kumnajisi msichana mwenye umri wa miaka kumi.

Awali alipofikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Kalambo kwa mara ya kwanza Chitezi alikana kutenda uhalifu huo lakini shauri lake lilipofikia hatua ya kusikilizwa na upande wa Mashataka kuita mashahidi wake ,mshtakiwa huyo alikubali.

Kabla ya kumuadhibu Hakimu Nixson Temu alieleza mahakama kuwa licha ya mshtakiwa kukiri kosa lake bado ameenda kinyume na Kifungu cha Sheria 130(1)(2) na (e) sambamba na Kifungu 131(1) ,Kanuni ya Adhabu ,Sura ya 16 iliyofanyiwa mapitio 2019.

Aliendelea kueleza kuwa licha ya mshtakiwa kukiri kosa lake bado ushahidi uliotolewa mahakama hapo na upande wa mashtaka ulioongozwa na Rajab Ndunda haujaacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda uhalifu huo .

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Agosti 12 mwaka huu katika kijiji cha Ulumi A wilayani Kalambo.

Akijitetea Chitezi aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza pia alikuwa amelewa usiku huo wa tukio.