Header Ads Widget

SHINYANGA SUPER QUEENS YAONJA KIPIGO MECHI ZA MAANDALIZI, KOCHA AAHIDI MAZURI DARAJA LA KWANZA


Kocha Msaidizi wa Shinyanga Super Queens, Suleman Shaban Hamad akizungumza na wachezaji wake baada ya kupoteza mchezo wa kirafiki dhidi ya ES Unyanyembe ya Tabora kwa mabao 5-3.

Na Damian Masyenene–Shinyanga Press Club Blog
TIMU ya Soka ya Wasichana, Shinyanga Super Queens ya mkoani Shinyanga imeendelea na maandalizi kwa ajili ya kujiweka fiti kwa michuano ya Ligi Daraja la kwanza upande wa Wanawake ambayo itatoa timu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL) msimu ujao.

Katika michezo hiyo ya maandalizi, Jana Agosti 1, 2020, timu hiyo iliwakaribisha ES Unyanyembe ya Tabora katika mchezo uliopigwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga ukihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Shinyanga, Benister Lugora na Kaimu Katibu Mkuu wa soka mkoa wa Tabora, Richard Kiyenze.

Shinyanga Super Queens ambayo imekamilisha usajili wake hivi karibuni, ilijikuta ikiduwazwa baada ya kukung'utwa mabao 5-3 katika uwanja wake wa nyumbani, ambapo mchezo huo wa kirafiki ni wa pili kwa timu hiyo baada ya ule waliocheza mwezi Julai, 2020 mkoani Geita dhidi ya Katoro Queens na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku benchi la ufundi likiitumia michezo hiyo kuangalia mapungufu ya kikosi chao. 

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Shinyanga Super Queens, Mzanzibari Suleman Shaban Hamad, alisema kikosi chake bado hakijatimia kwani bado wanaendelea kukisuka na baadhi ya wachezaji hawajajiunga na timu hiyo, hata hivyo mchezo huo dhidi ya timu yenye uzoefu umewasaidia kuyatazama makosa ambayo wameyaona na watayafanyia kazi hususan eneo la golikipa na mabeki. 

“Ni mchezo wa kwanza wa kirafiki nyumbani, bado wachezaji hawajakaa pamoja kwa muda mrefu kutengeneza muunganiko, ndipo tumeanza kuisuka timu na wachezaji wengi hawana uzoefu, lakini naamini tutaimarika na kuwa bora zaidi,” alisema. 

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa ES Unyanyembe, Abiud Hamis, alisema ushindi walioupata umetokana na wachezaji wake kuyafuata vyema maelekezo ya walimu wao, huku akilia na ubutu wa safu ya ushambuliaji. 

“Tunawaheshimu wapinzani wetu wamecheza vizuri, lakini tumepata nafasi nyingi na hatujazitumia vizuri hili linanionyesha bado kuna tatizo kwenye umaliziaji….tunahitaji michezo mingine ya kirafiki kuboresha mapungufu, tunaomba sapoti ya wadau,” alisema. 

Nahodha wa Shinyanga Super Queens, Tatu Abbas alisema licha ya kupoteza mchezo wa jana lakini wamepata uzoefu kwa kukabiliana na timu yenye wachezaji bora na kwamba walimu wao watakaa chini kuyasahihisha mapungufu yaliyoonekana, huku Ofisa Habari wa kikosi hicho, Robert Onesmo akiendelea kuwasihi wadau na wapenda soka katika mkoa wa Shinyanga kuiunga mkono timu yao ambayo ni mwakilishi pekee wa mkoa huo katika soka la wanawake.

TAZAMA PICHA CHINI
  Beki wa Shinyanga Super Queens, Aisha Mohamed akiondoa mpira kwenye hatari wakati wa mchezo wa kirafiki uliozikutanisha Shinyanga Super Queens dhidi ya ES Unyanyembe kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga
   Mshambuliaji wa ES Unyanyembe, Ashura Shaban (fulana nyeusi) akiwatoka wachezaji wa timu ya Shinyanga Super Queens wakati wa mchezo wa kirafiki uliozikutanisha timu hizo Jana.
 Mlinda Mlango wa Shinyanga Super Queens, Hellen Samson akidaka mpira wakati wa mchezo wa kirafiki ulioikutanisha timu yake na ES Unyanyembe ya Tabora kwenye uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga, jana.
  Kocha Msaidizi wa Shinyanga Super Queens, Seleman Hamad Shaban, akitoa maelekezo kwa vijana wake
 Wachezaji wa timu za Shinyanga Super Queens na ES Unyanyembe wakiwania mpira wa kona wakati wa kirafiki uliozikutanisha jana kwenye uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga
 Mchezaji wa ES Unyanyembe, Zulfa Maulid (kushoto) akidhibitiwa na mchezaji wa Shinyanga Super Queens, Patricia Kipanda wakati wa mchezo wa kirafiki uliozikutanisha timu hizo jana kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.

Kocha wa ES Unyanyembe, Abiud Khamis akitoa maelekezo kwa wachezaji wake

Mchezaji wa kikosi cha Shinyanga Super Queens, Novia Selestine akimdhibiti mchezaji wa ES Unyanyembe jana kwenye mchezo wa kirafiki uliozikutanisha timu hizo kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga, Benister Lugora (katikati) akizungumza na viongozi wa timu ya Shinyanga Super Queens baada ya kumalizika mchezo wa kirafiki dhidi ya ES Unyanyembe ya Tabora 
Kocha Msaidizi wa Shinyanga Super Queens, Seleman Shaban Hamad akitoa tathmini ya mchezo kwa waandishi wa habari
Nahodha wa Shinyanga Super Queens, Tatu Abbas akizungumza baada ya kukamilika kwa mchezo wa kirafiki waliopoteza kwa mabao 5-3.
 Ofisa Habari wa Shinyanga Super Queens, Robert Onesmo (Kulia) akizungumza na mwandishi wa habari
 Wachezaji wa Shinyanga Super Queens wakipasha misuli baada ya kumalizika kwa mchezo huo
 Sehemu ya benchi la Ufundi la ES Unyanyembe
 Sehemu ya benchi la ufundi la Shinyanga Super Queens
 Kocha wa timu ya ES Unyanyembe, Abiud Khamis akitoa tathmini ya mchezo huo kwa wachezaji wake
 Kocha Seleman Shaban Hamad wa Shinyanga Super Queens akiwapa tathmini ya mchezo wachezaji wake baada ya kumalizika mchezo huo
Wachezaji wa Unyanyembe wakimshukuru Mungu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Shinyanga Super Queens
Picha zote na Damian Masyenene