Header Ads Widget

BWALYA, ONYANGO WAONGEZA IDADI YA WALIOSAJILIWA SIMBA SC

Mchezaji mpya wa Simba, Larry Bwalya (kulia) akitambulishwa na timu hiyo leo Agosti 15, 2020. kushoto ni Kocha Msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola.

Na Damian Masyenene, Shinyanga Press Club Blog
KATIKA kuhakikisha inajiandaa vyema kwa msimu mpya kwa ajili ya kutetea mataji yake matatu iliyoyoyatwaa msimu huu nchini pamoja na maandalizi ya michuano ya kimataifa, Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wameendelea kuyaanika hadharani majina ya nyota waliowasajili kwenye dirisha hili la usajili lililofunguliwa Agosti 1, 2020.

Katika harakati hizo, leo Agosti 15, 2020 saa 11 jioni klabu hiyo imemtambulisha kiungo wa kimataifa wa Zambia, Larry Bwalya.

Kupitia ukurasa wao wa Instagram leo wakati wanamtambulisha Bwalya, Simba waliandika "Larry Bwalya wenyewe wanamuita locomotive. Box to box midfielder, super maestro, magician left footer, aliyetuletea Chama ndio aliyemleta Bwalya. Ethiopia Airlines iliyomleta ndio wenzetu wameenda kumfata, kiufupi wamebugi. Karibu Mwamba wa Kitwe," 
Larry Bwalya (kulia) akisaini mkataba wa kujiunga na Simba SC mbele ya Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola

Jana Agosti 14, 2020, Wekundu hao wa Msimbazi walitangaza kumsajili na kumtambulisha beki raia wa Kenya, Joash Onyango ambaye anatokea klabu ya Gor Mahia ya nchini humo.

Usajili huo wa Onyango ambaye ni beki wa kati unalenga kuisuka upya idara ya ulinzi ya Wekundu hao hususan mabeki wa kati, ambapo Simba walinukuliwa kwenye ukurasa wao wa Instagram wameandika kwamba "Tumeweka malengo makubwa msimu huu ya kufika mbali kwenye ligi ya Mabingwa Afrika na mashindano ya nyumbani hivyo lazima pia klabu isajili mabeki na wachezaji wenye uzoefu mkubwa katika mechi kubwa kubwa. Beki wa kimataifa wa Kenya, Joash Onyango ametua Msimbazi. Onyango aliyekuwa anapakaa rangi nywele na ndevu zake, sasa amekuja kivingine tayari kuchezea Mabingwa wa Taifa hili,".
Joash Onyango (kushoto) akisaini mkataba wa kuitumikia Simba.

Mbali na Onyango, Simba pia walimtambulisha mshambuliaji mpya waliyemsajili kutoka KMC ya Dar es Salaam, Charles Ilanfya ambaye amekusudiwa kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji na kuleta ushindani kwa nyota waliopo John Bocco na Meddie Kagere.
Mshambuliaji mpya wa Simba, Charles Ilanfya (kulia)

Pia mchezaji mwingine aliyetambulishwa ni David Kameta, beki wa kulia aliyemsajili kutoka Lipuli FC ya Iringa. 
Mlinzi wa kulia wa klabu ya Simba, David Kameta (kushoto) akisaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo.

Hata hivyo, wiki hii imekuwa na pilika nyingi kwa Wekundu wa Msimbazi, ambapo mbali na utambulisho huo wa wachezaji, Simba SC ilitambulisha nembo (logo) yao mpya na jezi zitakazotumika kwa msimu ujao.
Muonekano wa kisasa wa nembo mpya ya klabu ya Simba

Picha kwa hisani ya Simba SC Tanzania