Header Ads Widget

WIZARA, SIDO ZAKUBALIANA KUWEKEZA KITUO CHA UBUNIFU MABUGHAI TANGA

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu

Mwandishi Wetu -Lushoto
 Wizara ya Afya, Idara kuu ya Maendeleo ya jamii  na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Shirika la viwanda vidogo SIDO zimekubaliana kuwekeza katika kituo cha ubunifu kilichopo katika chuo cha  Maendeleo ya Jamii Mabughai mkoani Tanga na kuhakikisha rasilimali na vifaa muhimu vinapatikana ili kituo hicho kiwe na tija.

Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho alipotembelea chuoni hapo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu amesema kazi hiyo itaanza mwaka huu na tayari Serikali imeshatenga  sh.milioni 500 ikiwa ni pamoja na kuandaa mazingira bora ya chuo.

“Serikali imewekeza vya kutosha kuhakikisha kuna mazingira mazuri ya kujifunza, fedha hiyo ipo sh. Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu, ukarabati wa darasa moja na bweni la wavulana, hivyo nawasisitiza mtumie nafasi hiyo vizuri ili uwekezaji huo usipotee bure” amesema.

Aidha, Dkt. Jingu amewahakikishia wanachuo hao kuwa Serikali inalenga kuwawezesha wahitimu kujiajiri kupitia maarifa wanayopata kwa kuanzisha mtandao na waajiri watakaokuwa tayari kuwachukua na kufanya kazi kwa vitendo pamoja na kutengeneza zaidi fursa ya kujifunza.

Amesema pia, Wizara ipo katika hatua za mwisho kuanzisha kampuni itakayomilikiwa na chuo ili kuwapa nafasi ya kujiandaa wanapotoka chuoni hapo.

“Tunataka kuanzisha kampuni ya chuo ambayo itakuwa inamilikiwa na chuo kama ilivyo SUMA JKT  ili kuwapa fursa zaidi”

Akiwa chuoni hapo Dkt. Jingu ametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo kituo cha ubunifu cha kidijitali kinacholenga kuwasaidia wanafunzi hao kubuni na kuendeleza maarifa wanayopata chuoni hapo.