Header Ads Widget

WANACHAMA 70 CCM WACHUANA MAJIMBO YA MSALALA, KAHAMA MJINI NA USHETU

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kahama Emmanuel Mbamange (kushoto) akimkabidhi fomu ya kugombea Ubunge Jimbo la Kahama Mjini, Shidula Mabambasi

Salvatory Ntandu - Kahama

Baada ya Chama cha mapinduzi (CCM) kuanza zoezi la kutoa fumu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho kuanzia leo Julai 14, 2020, Jumla ya wagombea 70 wakiwemo wanawake 7 wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na chama hicho katika nafasi za Ubunge majimbo ya Kahama mjini,Ushetu na Msalala.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo baada ya kukamilisha siku ya kwanza ya utoaji wa fomu za ubunge na Udiwani, Katibu wa CCM wilaya ya Kahama, Emmanuel Mbamange amesema mwaka huu wagombea wengi wamejitokeza kuwania nafasi za ubunge tofauti na  uchaguzi wa mwaka 2015.

Alisema kuwa katika Jimbo la kahama Mjini leo wamejitokeza wagombea 37 ambapo kati yao wanawake ni sita na vijana ndio wameongoza katika zoezi hilo ambalo linatarajia kufungwa Julai 17, 2020 saa 10 jioni.

“Katika Jimbo la Msalala mpaka sasa kunawagombea 25 ambapo mwanamke ni mmoja  huku Jimbo la Ushetu likiwa na wagombea nane pekee,natarajia mapaka tarehe ya mwisho wagombea wengi watajitokeza kuomba nafasi mbalimbali za Ubungea na udiwani ili waweze kuwatumikia wananchi katika maeneo yao,”amesema Mbamange.

Amebainisha kuwa CCM mpya inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imejidhatiti kuboresha demokrasia ndani ya chama hicho, hali ambayo imesababisha watu wengi kukipenda chama hicho na mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya Tano ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili wananchi wanyonge.

“Kukua kwa demokrasia ndani ya CCM imewavutia watuwengi kujiunga na chama ndio maana unaona watu wengi wanaomba nafasi mbalimbali za uongozi kutokana na misingi mizuri inayosimamiwa na mwenyekiti wetu wa Taifa Dk Magufuli,”amesema Mbamange.

Sambamba na hilo amesema kuwa jumla ya wagombea 50 wamejitokeza kugombea nafasi za udiwani wa viti maalum huku katika kila kata zote katika majimbo matatu fomu za udiwani zikiendelea kutolewa ambapo mwitikio nao umekuwa ni mkubwa ikilinganishwa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katibu wa CCCM wilaya ya Kahama Emmanuel Mbamange (Kushoto) akimkabidhi fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Msalala, Anitha Obadia Shamawele.

Katibu wa CCCM wilaya ya Kahama Emmanuel Mbamange