Header Ads Widget

SIMBA YAKABIDHIWA RASMI KOMBE LA VPL, MANARA ATAMBA KUELEKEA JUMAPILI

Wchezaji wa timu ya Simba na baadhi ya viongozi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabdhiwa kombe la ubingwa wa ligi kuu.
Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Simba SC ya Jijini Dar es Salaam leo Julai 8, 2020 imekabidhiwa rasmi kombe la ubingwa wa michuano hiyo katika Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Simba imekabidhiwa kombe hilo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala aliyemuwakilisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya wenyeji wao, Namungo FC kwa suluhu ya 0-0.

Wekundu wa Msimbazi Simba walitwaa ubingwa huo msimu huu wakiwa tayari wana alama 81 baada ya kushuka dimbani mara 34 huku wakiwa na michezo minne mkononi.

Hafla ya kukabidhiwa kombe hilo pamoja na zawadi zingine kwa mabingwa hao mara tatu wa VPL ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hassan Abbas ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali pamoja na Rias wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mguto. 

Hata hivyo Simba wamekabidhiwa ubingwa huo bila ushindi kwenye mchezo wa leo ikiwa ni mara ya pili, ambapo msimu uliopita pia walikabidhiwa ubingwa kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye dimba la Jamhuri, Morogoro uklimalizika kwa sare ya 0-0.

Pia ni mara ya pili mfululizo kwa mabingwa hao kukabidhiwa ubingwa huo wa ligi nje ya Dar es Salaam, baada ya hii leo kukabidhiwa zawadi hizo mkoani Lindi na msimu uliopita kukabidhiwa mkoani Morogoro. 
 Nahodha wa Simba SC, John Bocco akinyanyua kombe baada ya kukabidhiwa hii leo.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Afisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara alisema lengo la timu yao ni kubeba ubingwa huo mara 10 mfululizo, hivyo kupatikana kwa ubingwa huo msimu huu kunafanya yabaki makombe  saba tu kukamilisha lengo lao.
Manara amesema jeuri hiyo inatokana na uwezo mkubwa wa kikosi chao unaotokana na usajili mzuri.

Afisa Habari huyo amebainisha kuwa timu yao itaingia jijini Dar es Salaam kesho asubuhi saa 3 kisha kuelekea Mtaa wa Msimbazi yalipo makao makuu ya Klabu kumkabidhi kombe hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Zungu ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ilala.

Naye Kocha Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola amesema kuwa “Imekuwa ni furajha kwetu kupata ubingwa mapema tuwapongeze wana Simba wote, sasa tunaenda kukaa chini na mwalimu kuona namna ya kuukabili mchezo wetu ujao wa nusu fainali ya kombe la shirikisho. tunataka tushinde tunajipanga hatuwezi kukubali kufungwa mara mbili,”.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala akimkabidhi kombe la ubingwa wa VPL, Nahodha wa Klabu ya Simba, John Bocco leo kwenye uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa. 
Picha kwa hisani ya Simba SC