Header Ads Widget

CHADEMA YAMPITISHA MAGRETH KYAI UBUNGE WA NKENGE, CCM WAGOMBEA WAFIKA 46




Wanachama wa Chadema wilaya ya Missenyi wakiwa kwenye uchaguzi wa kura za maoni kumpitisha mgombea jimbo la Nkenge

Na Avitus Mutayoba -Missenyi
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Missenyi mkoani Kagera kimempitisha Magreth Kyai kugombea ubunge katika jimbo la Nkenge wilayani humo.

Akitangaza matokeo katika kikao kilicholenga kuwapigia kura za maoni wagombea, Katibu wa chama hicho wilayani Missenyi, Ruchius Joseph amesema kuwa Magreth amepitishwa baada ya mgombea mwenza aliyetajwa kwa jina la Hilda Luhikula kujiondoa katika mchakato ili kumpisha mwenzake aweze kuwatumikia wananchi.

Ruchius ameongeza kuwa mgombea huyo kwa sasa anasubiri kuidhinishwa katika vikao ngazi ya mkoa ili aweze kuanza rasmi kampeni pindi pazia la kampeni litakapofunguliwa.
Magreth Kyai
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Magreth Kyai amesema kuwa ameamua kugombea nafasi hiyo ili aweze kujenga hoja zitakazosaidia kuimarisha kilimo cha kahawa na kuwakomboa kiuchumi wananchi wa mkoa wa Kagera.

Aidha Magreth ameongeza kuwa anakusudia kuhakikisha anafungua milango na fursa za kiuchumi kwa jimbo la Nkenge kwa kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika kilimo na ufugaji wilayani humo.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Missenyi, Emmanuel Alex amesema kuwa jumla ya watia nia 46  ya ubunge katika jimbo hilo wamekwishajitokeza na kuchukua fomu ambapo kati ya hao, 43 ni wanaume na 3 ni wanawake.