Header Ads Widget

ASKOFU MABUSHI AWATAHADHARISHA VIONGOZI WA KIROHO WANAOGOMBEA



Askofu wa Kanisa la IEAGT -Shinyanga, David Mabushi
Na Mwandishi Wetu – Shinyanga Press Club Blog  
WAKATI joto la uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu likizidi kupanda, baadhi ya viongozi wa dini wanaoonyesha kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho wametahadharishwa, huku wananchi na wanasiasa wakionywa kuepuka kampeni chafu zitakazozusha vurugu na kutoweka kwa amani.

Tahadhari hiyo imetolewa na Askofu wa Kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) lililopo mjini Shinyanga, David Mabushi ambaye ameiomba Serikali kuona uwezekano wa kuweka nafasi ya watumishi wa kiroho katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wawe na uwakilishi ili watoe mchango wao katika kutunga sheria.

Askofu Mabushi alitoa ombi hilo alipokuwa akizungumza na waumini wake wakati wa ibada ya Jumapili kanisani hapo, ambapo alitoa pia wito kwa viongozi wa kiroho wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo wawe mfano wa kuigwa kwa kuendesha siasa safi na za kistaarabu.

Mabushi pia aliwaasa wanawake wanaotarajia kutia nia katika uchaguzi huo kuhakikisha nchi haingii kwenye machafuko kwani wao ndiyo wahanga wakubwa na watoto wakati wa machafuko.

"Tumeona baadhi ya viongozi wa dini wametia nia ya kutaka uongozi kwenye huu uchaguzi, nawaomba wawe mfano katika siasa kwa kufuata taratibu za nchi na kuhakikisha wao wanakuwa mabalozi wa ustaarabu.

“Ni matarajio yangu kuwa wote watakao tia nia na kukubaliwa na vyama vyao wakumbuke kutii sheria za nchi kwa kuepuka siasa za kashfa bali watangaze sera za vyama vyao watafanya nini wakiteuliwa,” alisema Mabushi.
Kwa upande wa waumini wa kanisa hilo akiwemo Rucia Josefu na Joramu Mabula walisema kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kuwa wa amani kwani kwa muda wa miaka mitano kumekuwa na mabadiliko hususan katika nyanja ya usalama.

“Wanawake tumeonyesha uaminifu katika utumishi na upande wa kampeni za ustaarabu tuwe wa kwanza kwani sisi ni wazazi tuiunge mkono serikali kuhakikisha nchi haiingii kwenye machafuko,”alisema Rucia.
Waumini wa kanisa hilo wakisikiliza neno la Mungu
Askofu Mabushi akihubiri neno la Mungu