Header Ads Widget

ALIKIBA, DIAMOND PLATINUMZ NA HARMONIZE WAKUTANA MEZA MOJA IKULU DODOMA, JPM APONGEZA
Na Damian Masyenene- Shinyanga Press Club Blog
Moja ya picha kubwa zilizonaswa leo ni Wasanii wakubwa na maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini (Bongofleva), Alikiba, Harmonize na Diamond Platinumz kuonekana wakiwa meza moja wakati wa hafla ya Chakula iliyofanyika leo Julai 12, 2020 Ikulu ya Chamwino, Jijini Dodoma.

Hafla hiyo iliandaliwa kwa Mwaliko wa Rais Dk. John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) maalum kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho na wasanii mbalimbali wa muziki nchini, ambapo imeelezwa kuwa zaidi ya watu 6,500 wamealikwa.

Wasanii Diamond Platinumz na Alikiba wamekuwa kwenye kile kinachotajwa kuwa ni uhasama wa muda mrefu kutokana na ushindani mkubwa ambao unatengeza uadui kutoka kwa mashabiki wao, hivyo hawajawahi kuonekana katika picha moja kwa miaka kadhaa sasa.

Wakati, Harmonize na Diamond Platinumz utengano ulianza kujengeka punde tu baada ya Harmonize kujiengua katika lebel ya WCB inayomilikiwa na Msanii Diamond Platinumz.

Mbali na picha za leo, huenda wasanii hao wakashuhudiwa zaidi katika jukwaa moja mwaka huu kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wakikipigia chapuo Chama Cha Mapinduzi (CCM), jambo ambalo halijashuhudiwa kwa muda mrefu sasa wasanii hao kutumbuiza katika jukwaa moja.

Akizungumzia hatua hiyo, Rais Magufuli amesema jambo hilo limemfurahisha kuona wasanii hao wanadumisha umoja na kuondoa uadui.

"Unapoona Diamond na Alikiba wamekaa meza moja huo ndiyo Utanzania na hicho ndicho ninachokiepnda, hongereni sana," amesema.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kushughulikia haraka suala la COSOTA kuhamishiwa wizara hiyo kutoka Biashara na Uwekezaji ili iweze kuwasaidia wasanii, huku akiahidi pia kulishughulikia suala la haki za wasanii.

TAZAMA PICHA

 Wasanii Harmonize, Alikiba, Diamond na Meneja, Babu Tale katika meza moja leo Ikulu, Chamwino.

 Wasanii hao wakiwa meza moja, katikati ni meneja wa Alikiba, Aidan Charlie