Header Ads Widget

24 WACHUKUA FOMU SHINYANGA MJINI, 13 SOLWA, AHMED SALUM AIREJESHA BAADA YA MASAA 2



Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum (CCM) akirejesha fomu ya kuwania ubunge wa jimbo hilo leo Julai 14, 2020 masaa mawili baada ya kuichukua.

Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog
JUMLA ya wagombea 24 wakiwemo wanawake wawili wamechukua fomu za kuwania ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya zoezi la uchukauji fomu ndani ya chama hicho kufunguliwa leo Julai 14, 2020, huku 13 wakichukua katika jimbo la Solwa mkoani humo, ambapo Mbunge anayetetea kiti chake, Ahmed Salum akirejesha fomu baada ya masaa mawili.

Miongoni mwa waliochukua fomu katika jimbo la Shinyanga mjini hii leo ni Jeolojia Eunice Jackson na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Shinyanga, Dk. Kulwa Meshack.

Wengine ni Mkurugenzi wa asasi ya Kiraia TVMC, Mussa Ngangala, Mwanasheria wa kujitegemea, Hassan Fatiu, Mfanyabiashara, Bandora Milambo, Grace Antony Lyon na John Mlyambate.

Akizungumzia mchakato huo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Shinyanga Mjini, Said Bwanga amesema mchakato unaendelea vizuri na unaonyesha kwamba wanachama wana msisimko wa kutaka kugombea, pia hali ni shwari na wagombea wameelimishwa kutoshindana wao kwa wao kwa kufanyiana vurugu.

“Tumezuia maandamano wakati wa kuja kuchukua fomu, tunaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kunakuwa na amani wakati huu wa mchakato wa uchukuaji fomu na mgombea yeyote atakayehusika kwenye vitendo vya rushwa chama hakitosita kumchukulia hatua," amesema.

Kwa upande wa jimbo la Solwa, mbunge anayetetea kiti chake, Ahmed Salum alichukua fomu saa 2 asubuhi na kuirejesha saa 4 asubuhi katika ofisi ya chama hicho, ambapo wanachama wengine waliojitokeza kuchukua fomu ya ubunge ni Mhadhiri wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Christian Misobi.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Salum amesema anawashukuru viongozi wa chama hicho kwa kutengeneza mfumo mzuri wa kidemokrasia katika kupata wagombea ambao unatoa demokrasia ndani ya chama.

“Kikubwa tuchukue fomu tujaze tumtangulize Mungu, tusubiri mchakato ndani ya chama endapo jina langu likipendekezwa kama mgombea wa CCM ndipo nitazungumza zaidi,” amesema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini (Jimbo la Solwa), Erenestina Richard amesema wagombea 13 wamejitokeza baada ya zoezi hilo kufunguliwa hadi muda wa saa 4 asubuhi, ambapo ameeleza kuwa wanaamini kadri muda unavyokwenda watazidi kujitokeza wanachama wengi wenye nia ya kuchukua fomu, huku maelekezo ya chama yakifuatwa na wagombea hao.

Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Erestina Richard akimkabidhi fomu ya ubunge, Christian Misobi anayewania ubunge wa Jimbo la Solwa

Ahmed Salum akisalimiana na baadhi ya wanawake waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania udiwani (Viti maalum) jimbo la Solwa.

Jeolojia Eunice Jackson Wiswa akionyesha fomu yake ya kuwania ubunge jimbo la Shinyanga Mjini



Afisa Uhusiano halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani, John Mlyambate akionyesha fomu ya kuwania ubunge jimbo la Shinyanga mjini.
 
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Shinyanga, Kulwa Meshack akionyesha fomu ya kuwania ubunge jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya CCM baada kuchukua fomu leo.